YU WAPI RAIS KIKWETE? NAMTAKA HAPA. 50

YU WAPI RAIS KIKWETE? NAMTAKA HAPA. 50
1.
Makabwela na wakwasi, tuchunge tulipotoka,
Mi naona utwesi, nachelea kuanguka,
Hashituki kwa unyasi, aso gongwa na nyoka,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
2.
Siku zimeenda kasi, miezi sasa miaka,
Japo si kazi rahisi, yapo yalo kamilika,
Tumeona ufanisi, udhaifu kadhalika,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
3.
Tuhoji bila tetesi, tushike yenye hakika,
Tusitukane matusi, tuepuke kuboboka,
Tufanye na udadisi, kama twataka kufika,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
4.
Tuanze kuhoji kasi, na nguvu ilo sifika,
Hari kupita kiasi, wallahi alipambika,
Mliuona wepesi, ama shida na mashaka?
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
5.
Nauliza hiyo kasi, kwayo tulifaidika?
Ama ndio wasiwasi, kwa watu wa kila rika?
Ziwapi zile nafasi, za watu kuajirika?
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
6.
Nguvu mpya na halisi, kweli ilihitajika,
Haya shime tudadisi, kama ndo ilotumika,
Maisha yana akisi, nguvu iliyotumika,.
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake
7.
Hari mpya wasiwasi, hili limethibitika,
Nimeiona nakisi, ya mambo yalotendeka,
Si walimu si manesi, wote wanahangaika,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake
8.
Unadhifu wa ukosi, kwakweli wanipa shaka,
Akiondoshe kinyesi, bila hata kuchafuka,
Mie naona utasi, kwa jamali msifika,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake
9.
Tulitaka mwendo kasi, ili tufike haraka,
Tena tupate wepesi, tufike bila kuchoka,
Kumbe tuna mkakasi, firigisi yenye taka,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
10.
Elfu mbili na kumi, aliupata ushindi,
Kwa ahadi kumikumi, si kwa pishi za mahindi,
Ilani ikawa ngumi, kiasi awe mshindi,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
11.
Kuna ahadi ya reli, Dar kanda ya ziwa,
Zipo ahadi za meli, katika yetu maziwa,
Na wajasiriamali, benki kuanzishiwa,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
12.
Mwenzenu sioni reli, werevu wameelewa,
Naona ubahaluli, ufisidi mabehewa,
Huenda ndio reli, ile tulo ahidiwa,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
13.
Zile shauku za meli, katika yetu maziwa,
Tuongee ukweli, iwapi hata ngalawa?
Na wajasiriamali, benki yao wamepewa?
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
14.
Ahadi za sipitali, hadhi kupandishiwa,
Naomba tuwe wakweli, hili limefanikiwa,
Tatizo lazikabili, upungufu wa madawa,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
15.
Umeme kila mahali, kaya nyingi kufikiwa,
REA yafanya kweli, kiasi twafanikiwa,
Vijiji mbalimbali, umeme vimewekewa,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
16.
Lindi mkumbuke hili, gridi kuunganishiwa,
Kwa Kigoma imefeli, gridi kuu kupewa,
Ruvuma nawakejeli, naona mmefikiwa,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
17.
Rukwa dhohofu l’hali, gridi ahadi hewa,
Kagera hawana hali, gridi yasubiriwa,
Tumefanywa majahili, wanyonge tumeonewa,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
18.
Wakulima kila mahali, pembejeo watapewa,
Mrijo kuna kiwili, trekta washanunuliwa?
Jembe la mkono dhuli, na bado linatumiwa.
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
19.
Kiongozi bulibuli, hakika hutegemewa,
Ati Jakaya fidhuli, asojua kuelewa,
Kikwete katika hili, wallahi anaonewa,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
20.
Barabara zenye lami, na ujengaji wa stendi,
Kwazo tukuze uchumi, sinambie hampendi,
Sasa ni miaka kumi, mambo yetu hayaendi,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
21.
Tanga sifanye harara, naomba nichagueni,
Viwanda na barabara, nitawapa tambueni,
Mtafanya biashara, naomba mniamini,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
22.
Watanga wana hasira, viwanda hawavioni,
Wamepata barabara, Horohoro Ngamiani,
Vijana wana zurura, wana vyeti mkononi,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake
23.
Mnisikize Kagera, oktoba nichagueni,
Leo nawapa bishara, masikio yategeni,
Tajenga kiwanja bora, ndege zipae angani,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake
24.
Wamezinduka Kagera, kutoka usingizini,
Nawaona wamefura, kiwanja hawakioni,
Ati wafanye subira, ngumu haiwezekani,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake
25.
WanaMisenyi Kagera, sijui wampe nini,
Hawaioni mikwara, ya kutolewa ranchini,
Imekuwa manusura, wafukuzwe si utani,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
26.
Bado ningali Kagera, hasa kule mpakani,
Hakuna japo ishara, ya umeme wenzanguni,
Mtukula wana hasira, Uganda si Marekani,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
27.
Mkoa wetu wa Mtwara, na Lindi nisikieni,
Viwanda na barabara, sasa tawajengeeni,
Tena sifanye harara, gesi itawafaeni,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
28.
Wakati wenu Mtwara, kutoka usingizini,
Zile siku za ujura, zimefika ukingoni,
Shime mkapige kura, mchague kwa makini,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
29.
Msidaganywe na gwara, mzingatie ilani,
Msikubali kangara, na fedha za mwafulani,
Mtaipata hasara, nawambia si utani,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
30.
Naomba mnipe mimi, sote tupate ushindi,
Mjue sina umimi, ubinafsi siupendi,
Mie ni mtu wa nyemi, na sina makurubundi,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
31.
Kuulinda usalama, wa Ziwa Victoria,
Nyasa liwe salama, na Tanganyika pia,
Sasa ni lala salama, ahadi zimetimia?
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
32.
Ndugu zangu wa Kigoma, vema mkanisikia,
Ondoa shaka Kigoma, Dubai tawapatia,
Nitawatendea mema, mji wenu tavutia,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
33.
Muda ndo wayoyoma, Kigoma inajutia,
Malagarasi ndo jema, kwalo wanafurahia,
Sasa wasaka neema, iliyopotea njia,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
34.
Longido na nchi nzima, maji nitawapatia,
Maji ni kitu lazima, hivyo sitapuuzia,
Mie naona nakama, maji yametufikia?
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
35.
Ardhi yazua hasama, ya mitutu na jambia,
Chagueni changu chama, tupate shughulikia,
Naapa nitajituma, hata liwe historia,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
36.
Mie naona nakama, nchi yaangamia,
Wana tabu wakulima, na wafugaji pia,
Unazidi uhasama, msidhani natania,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
37.
Tatizo halijakoma, halijawa historia,
Ya Kilosa na Dodoma, wote tumeyasikia,
Yaani kama wanyama, watumiavyo jambia,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
38.
SHIRECU sishike tama, muache kulialia,
Hayo madeni ya chama, mie nitawalipia,
Nawauliza wanachama, madeni kawalipia?
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
39.
Pangani haitazama, ahadi nawapatia,
Hatari taitazama, tena tafuatilia,
Bahari ifanye hima, kisiwa kitabakia,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
40.
Mkulima wa pale Wami, na mvuvi wa Malindi,
Hali zao sizisemi, sio wao hata mafundi,
Kaupandisha uchumi, mambo yao hayaendi,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
41.
Geita kuwa mkoa, ahadi kaitimiza,
Lipo linalo sonoa, huenda likatatiza,
Kuongeza Mikoa, na gharama huongeza,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
42.
Lililomtia doa, operesheni tokomeza,
Nyumba wakazibomoa, mazao wakaunguza,
Tembo mnawaokoa, watu mwawaangamiza,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
43.
Meli tunaitoboa, kwa michezo tunocheza,
Utulivu una doa, amani twaipoteza,
Mjue twajikomoa, dira tukiipoteza,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
44.
Leo Njano na dondoa, sidhani nimeongeza,
Ahadi alizotoa, si zote katekeleza,
Sihitaji chokonoa, zipo alizotimiza,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
45.
Hachukii yuko poa, ajua kubembeleza,
Hata wakimzodoa, ni mzito kudakiza,
Akipakwa mnokoa, ubani ajifukiza,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
46.
Kinamama taokoa, pia tawaendeleza,
Bajaji kila Mkoa, wilayani kusambaza,
Wazae wakiwa poa, vifo tutavipunguza,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
47.
Siseme namboboa, mwenzenu anishangaza,
Swali nataka litoa, hivi nini aliwaza?
Nyachiro sio Kondoa, bajaji hizi zaweza?
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
48.
Shida hajaiondoa, maa mwanga maa giza,
Macho tunayakodoa, stima inavyotatiza,
Mfano uanze nyoa, uache hujamaliza.
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
49.
Mengi nimedondoa, naendea kumaliza,
Ka’ lipo nilopotoa, mfano kwa kuongeza,
Siache kunikosoa, kwa lile nilopunguza,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.
50.
Sasa nakata ulimi, kusema sana sipendi,
Naenda okoa ami, mezama katika lindi,
Ifike mwezi wa kumi, haki ipate ushindi,
Yu wapi Rais Kikwete, zi wapi ahadi zake.

Dotto Chamchua Rangimoto (Njano5)
255762845394/255784845394
mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania.