KIRUSI CHA ZIKKA CHATINGA RASMI AFRIKA.


Serikali ya Guinea-Bissau imebuni kamati ya dharura ya afya baada ya kuripotiwa kesi tatu za kwanza za kirusi hatari cha Zika.

Taarifa ya Wizara ya Afrika ya nchi hiyo imesema kuwa, kesi za ugonjwa huo hatari zimeripotiwa katika eneo la Bijagos na kwamba serikali imebuni kamati maalumu inayoongozwa na Waziri Mkuu Baciro Dja ili kuzuia kusambaa kwa kirusi hicho, wakati huu ambapo nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika inajikusanya baada ya kukumbwa na ugonjwa wa Ebola.

Kirusi hatari cha Zika kiliripotiwa kuibuka barani Afrika kwa mara ya kwanza katika Visiwa vya Cape Verde magharibi mwa bara hilo mwezi uliopita. Mkrugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Afrika, Matshidisho Moeti alisema, kesi hiyo ya Cape Verde ni ushahidi kuwa kirusi cha Zika sasa kimesambaa hadi nje ya bara la Amerika na kuingia Afrika.

Kirusi cha Zika kuligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 1947 na hakikuhesabiwa kuwa hatari hadi kilipoibuka upya mwaka jana nchini Brazil na kusababisha wanawake walioambukizwa kuzaa watoto wenye ubongo mdogo.

RWANDA YAIPINGA MAREKANI KUIHUSISHA MAGENDO YA BINADAMU.


Serikali ya Rwanda imekadhibisha tuhuma za Marekani kuwa inahusika na magendo ya binaadamu.

Mathilde Mukantabana, balozi wa Rwanda nchini Marekani hapo jana aliitaja ripoti hiyo kuwa ya kisiasa ambayo iko kinyume na ukweli wa mambo katika jamii ya Wanyarwanda wenyewe. Bi, Mukantabana ameogeza kuwa, serikali ya Kigali ina uwezo kamili wa kuwalinda na kuwapa hifadhi wakimbizi hususan raia wa Burundi.

Balozi huyo amefafanua kuwa, kuwalinda raia wa Burundi mkabala na kufanya magendo ya binaadamu, ni suala linalopewa kipaumbele na serikali ya Rwanda. Katika ripoti yake ya mwaka 2015 iliyotolewa siku ya Alkhamisi, Juni 30 Marekani iliituhumu serikali ya Kigali kwamba inashiriki katika magendo ya binaadamu hususan raia wa Burundi.

Kadhalika ripoti hiyo iliashiria kwamba Rwanda imekuwa ikiwatumia watoto wadogo wa Kirundi kama askari. Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Rais Paul Kagame kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya ukandamizaji wa haki za binaadamu.

80 WAFA KWA MASHAMBULIZI YA MABOMU IRAQ.


Watu wasiopungua 80 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi pacha ya mabomu katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Hujuma ya kwanza imeripotiwa kufanyika alfajiri ya leo nje ya mgahawa mmoja katika wilaya ya Karada na muda mfupi baadaye shambulizi la pili likafuatia mashariki mwa Baghdad.

Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Baghdad awali ilisema watu zaidi ya 60 wameuawa na wengine 100 wamejeruhiwa. Kundi la kigaidi la IS limekiri kuhusika na mashambulizi hayo na kutoa takwimu tofauti na za serikali za wahanga wa hujuma hizo. IS wamesema watu 40 wameuawa katika mashambulizi hayo na wengine 80 wamejeruhiwa.

Mashambulizi hayo yamefanyika masaa machache baada ya Waziri Mkuu wa Iraq kuzionya pande zinazowaunga mkono IS. Haider al-Abadi aliyasema hayo jana Jumamosi katika kikao na waandishi wa habari mjini Baghdad, na kuongeza kuwa, wale walioanzisha kundi la kigaidi la IS au kuliunga mkono, hivi sasa wanateketea katika moto ambao waliuwasha wao wenyewe.

Hujuma hii inafanyika siku mbili baada ya watu 46 kuuawa na kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi dhidi ya msikiti mmoja katika kitongoji cha Abu Ghraib, viungani mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

ASSAD: MGOGORO SYRIA UTAISHA KWA MAZUNGUMZO SAMBAMBA NA KUPAMBANA NA UGAID.


Rais Bashar Assad wa Syria amesema kuwa, haiwezekani kupatikana njia ya ufumbuzi halisi wa mgogoro wa nchi hiyo bila ya kuwepo mapambano ya kweli dhidi ya ugaidi.

Rais Assad amesema kuwa, kuna ishara za kukomeshwa mgogoro wa Syria na kuongeza kuwa, utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo unafungamana na mazungumzo ya Wasyria kuhusu mchakato wa kisiasa lakini sambamba na hayo mapambano dhidi ya ugaidi yanapaswa kudumishwa.

Kuhusu mwendo wa kinyonga wa mchakato wa kutafuta suluhisho la mogoro wa Syria, Rais Bashar Assad amesema: Waungaji mkono wa magaidi wa Magharibi na nchi kama Saudi Arabia, Uturuki na Qatar hazitaki kusitisha misaada yao kwa makundi hayo ya kigaidi. Rais wa Syria amesema iwapo misaada hiyo itasitishwa na Wasyria wakashauriana kuhusu katiba, mustakbali wa nchi na mfumo wa utawala basi hapana shaka kutapatikana utatuzi wa mgogoro huo hivi karibuni.

Baada ya kupita miaka 5 sasa tangu nchi ya Syria itumbukizwe katika mgogoro wa ndani, na kudumishwa misaada ya pande zote ya nchi za Magharibi na vibaraka wao kwa wapinzani na makundi ya kigaidi kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Assad, sasa kumeanza kujitokeza ishara za kukomeshwa mgogoro huo.

Tangu mgogoro huo ulipoanza Marekani, Uturuki, Saudi Arabia na Qatar zilifanya kila liwezekanalo kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria na kuwasaidia wanachama wa makundi ya kigaidi kuingia nchini humo. Ushirikiano wa miaka 5 wa nchi hizo na makundi ya kigaidi haujaweza kutimiza sehemu ndogo ya malengo yaliyoainishwa kwa ajili ya mgogoro wa Syria na hadi sasa Rais Bashar Assad angali anaongoza nchi hiyo huku makundi ya kigaidi yakidhoofika siku baada ya siku.

Inaonekana kuwa moja kati ya matunda ya uwekezaji wa nchi kama Uturuki katika mgogoro wa Syria ni kuhatarisha usalama wa Uturuki yenyewe ambayo miji yake mingi imekuwa ikikukmbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya milipuko ya kigaidi. Shambulizi la hivi karibuni kabisa ni lile la Jumanne iliyopita lililolenga uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul na kuua watu karibu 50. Watu wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa.

Matokeo kinyume na matarajio ya mradi wa nchi za Magharibi na vibaraka wao katika mgogoro wa Syria yamezilazimisha nchi hizo kuanza kuamiliana na serikali ya nchi hiyo kama alivyosisitiza rais Assad kwamba nchi za Magharibi zinawatuma maafisa wao hususan maafisa wa masuala ya usalama huko Damascus ili kushirikiana na kufanya mazungumzo ya siri na Syria.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amewaambia waandishi habari katika mji wa Sochi nchini Russia kwamba nchi yake inataka kutatuliwa mgogoro wa Syria kwa njia za kisiasa. Mevlüt Çavuşoğlu amesema Uturuki ilikuwa na mitazamo tofauti kuhusu suala la kubakia madarakani Rais Bashar Assad huko Syria lakini sasa iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu mitazamo mingine.

Hata hivyo na kama alivyosisitiza Rais Bashar Assad wa Syria, matamshi matupu ya kutaka kuwepo utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria hayatoshi na hapana shaka kuwa, mapambano ya kweli dhidi ya makundi ya kigaidi nchini Syria ni miongoni mwa masharti muhimu ya utatuzi wa kisaisa wa mgogoro huo.

Mafanikio ya Syria katika vita dhidi ya ugaidi ikishirikiana na Iran na Russia, yameimarisha nafasi ya Rais Assad na hapana shaka kuwa, usalama na amani ya nchi jirani vitaimarishwa kwa kuyaangamiza kikamilifu makundi ya kigaidi nchini humo.

MOHAMMAD PAKPOUR: MAREKANI NA SAUDIA ZILITUMA MAGAIDI KUSHAMBULIA IRAN.

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC amesema wanachama wa magenge ya kigaidi waliokamatwa hivi karibuni hapa nchini wakipanga njama za kutekeleza mashambulizi ya bomu wamekiri kwamba walipokea ufadhili kutoka Saudi Arabia na Marekani.

Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour, kamanda wa kikosi cha ardhini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran amesema magaidi hao wamekiri kuwa walifadhiliwa na nchi mbili hizo ili kujenga ngome hapa nchini na haswa katika maeneo ya mipakani kwa shabaha ya kutekeleza hujuma za kigaidi katika kona mbali mbali ya nchi.

Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema Washington na Riyadh zimekuwa zikiyafadhili na kuyaunga mkono magenge ya kigaidi kwa lengo la kuyumbisha usalama wa nchi sambamba na kusambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu, njama ambazo amesema hazitazaa matunda.

Amongeza kuwa, mmoja wa magaidi hao waliokamatwa wiki jana katika mji wa Khash mkoani Sistan-Baluchistan ameaga dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa operesheni ya kusambaratisha ngome yao.

Waziri wa Usalama Iran Mahmoud Alavi siku chache zilizopita alisema magaidi wakufurishaji waliokamatwa hivi karibuni walipanga kutekeleza mashambulizi katika maeneo 50 kote Iran na haswa mji mkuu Tehran.

Amesema kuwa magaidi hao walikuwa wameshaainisha maeneo 50 ya kutega mabomu na kwamba tayari walikuwa na kilo 100 za mada za miripuko; huku vikosi vya usalama vikifanikiwa kuzuia tani mbili za mada hizo ambazo magaidi walipanga kuingiza nchini.

Mbali na kukamata magaidi 10 miongoni mwao, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC liliangamiza magaidi watano wa kundi la kigaidi la PJAK kaskazini magharibi mwa nchi. Vikosi vya usalama na ulinzi nchini vimetibua mashambulizi kadhaa ya kigaidi katika muda wa siku chache zilizopita.

NIMETAFAKARI SANA.

Kumekucha ni salama, ahsante mungu wangu,
Japo dede nasimama, na tete hatua zangu,
Nina kuomba Karima, nifike safari yangu
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.

Jana sikupe hasira, leo sipate karaha,
Tena sifanye harara, kesho upate furaha,
Kiumbe fanya subira, kama wazitaka raha.
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.

Aliyeumba kinyonga, ndiye kaumba farasi,
Lumbwi siwezi jinyonga, kulilia kwenda kasi,
Karima ndiye hupanga, ndogo nyingi na kiasi,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.

Namtazama jongoo, kunako miguu yake,
Ilivyo kama pongoo, ajabu ni mwendo wake
Kamzidi kangaroo, lakini si mbio zake,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.

Sijaona uwaridi, lisilo kuwa na miba,
Ama jambo maridadi, baya liwate kubeba,
Jua kuna kujirudi, ndio ikawepo toba,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.

Mja usiwe bahili, pia usifanye ria,
Ila sianguke chali, asama kusaidia,
Moyo usizidi hali, Mola alokujalia,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.

Kaditama namaliza, hapa natia kikomo,
Shika nilo yawaza, huenda tapata somo,
Kuuliza unaweza, zingatia yaliyomo,
Nimezama fikirani, nawaza mie nawaza.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Whatspp/call 0622845394 Morogoro

MAPENZI, NDOA, ROHO, MAJINI NA BINADAMU.

Ndoa nyingi huvunjika, na wapenzi wengi huachana kabla hata hawajafunga ndoa. Kabla ya ndoa kuvunjika na wapenzi kuachana hutokea visa vingi vya usaliti, ukigeugeu na chuki.

Mapenzi nini? Mahala pake hasa ni wapi? Asili yake wapi?Wakati gani usaliti hutokea? Wakati gani mtu anakuwa kigeugeu? Nini hasa chanzo cha chuki kwa wapenzi?

Hakuna maana moja ya mapenzi, ila vyovyote iwavyo mapenzi ni ile hali ya kuvumilia na kukubali mapungufu, udhaifu na karaha za mtu yoyote au hali yeyote au kitu chochote.

Mapungufu, udhaifu na karaha zinapokuwa za kiwango kikubwa na bado ile hali ya uvumilivu na kukubali ikaendelea kuwepo,basi hapo ujue kuwa kiwango cha mapenzi kiko juu sana, na kinyume chake ni kweli. Ukiona mtu yuko na mapungufu na mbaya zaidi ni kero kwako lakini bado wampenda basi ujue kuwa uko na mapenzina huyo mtu.

Mapenzi mahala pake ni moyoni; ambapo si lile pande la nyama lenye vyumba na mishipa ya kutoa na kuingiza damu, bali ni ile roho ambayo ndio asili ya nguvu zote zinazopatikana ndani ya mwili wa mwanadamu. Mwili wa mwanadamu tunaweza kufananisha na kompyuta.

Kopyuta imeundwa na mifumo miwili yenye kutegemeana ambavyo ni hardware na software. Vile vitu tunavyoweza kuvishika na kuviona ndio hardware na vile ambavyo hatuwezi kuviona wala kuvishika ni software. Software ndio huilazimisha hardware nini ifanye, na hardaware hupokea command toka kwa software.

Kwa upande wa mwanadamu kuna roho na mwili. Roho ndio huamuru kitu cha kufanya na katu mwili hauwezi kuiamuru roho kitu cha kufanya. Roho ni kama OS[Operating System] kwa kompyuta.

Kwa mujibu wa mapokeo ya dini za kikristo na kiislamu, mwili wa mwanadamu umeumbwa kutokana udongo, kisha mungu akupulizia pumzi yake kwenye hilo dongo hata likawa mwanadamu mwenye uhai.

Kama nilivyosema awali kuwa roho ni kama OS, na ndani ya OS huweza kuongezwa programu mbalimbali kulingana na uhitaji wa mtumiaji wa kompyuta, pia kwa mwanadamu pia huwa kuna viprogramu vidogodogo vinavyopatikana ndani ya ROHO.

Viproglamu hivyo vidogo vidogo ni kama vile vya kucheka,kununa, kuchukia, kutamani, kupenda, nk, Kila ROHO si lazima iwe na viprogramu hivi vyote, bali zingine huwa na hizi na hukosa zile na zingine hupata zile na hukosa hizi.

Kikubwa cha kufahamu ni kuwa mwanadamu hawezi kucheka kama hana hicho kiprogramu cha kumuwezesha kucheka, kama vile huwezi kuchezesha video kwenye kompyuta yako kama hauna programu ya kukuwezesha kuchezesha video. Watu wengine hawajui kununa na wengine hawajui kucheka pia, hiyo ni kwasababu hakuna kitu hicho cha kununa au kucheka kwenye roho zao. Upendo na chuki ni moja kati ya viprogramu vilivyopo kwenye roho.

SOUL MATE? Class mate humaanisha ni mtu ambaye umesoma naye darasa moja, naam, mlikutana huko darasani. Nini maana ya SOUL MATE? Hivi roho hukutana? Kwa mujibu wa dini ya kiislamu M/Mungu alianza kuziumba roho za viumbe vyote kabla hata ya kuumbwa ulimwengu na ziliishi miaka mingi kabla hata hazijatiwa au kupuliziwa kwenye miili ya viumbe hivyo. Hivyo basi huenda hizo roho zilikutana huko kwa mara ya kwanza.

Katika filamu ya kihindi inayoitwa Dil To Pagal Hai mtunzi ametueleza kuwa roho zimeumbwa katika jozi, yaani mbili mbli huku zikiwa zimenatana. Wakati wa kutiwa kwenye miili ya viumbe zikatenganishwa, moja ikatiwa kwa mwanaume na nyingine ikatiwa kwa mwanamke. Hizi roho mbili lazima zikutane, na kukutana kwenyewe ni kwa watu waliobeba roho hizo kuoana, na ndoa iliyofungwa na watu wenye hizi roho mbili[soulmate] katu hawawezi kuachana.

Usaliti? Kigeugeu? Mara baada ya M/mungu kupulizia pumzi yake kwenye mwili wa mwanadamu, baadaye na hii mara baada ya kutokea uasi mbinguni zikaingia pumzi zingine ngeni kwenye miili ya wanadamu. Pumzi hizi ni majini, au mashetani au mapepo. Hizi pumzi hufanya kazi kama roho ndani ya mwili. Nilisema huko juu kuwa roho huamuru mwili cha kufanya, hivyo na haya majini pia huamuru mwili cha kufanya.

Mkumbuke Hawa na Adamu hawakuwahi kufikiria japo kuusogelea ule mti wa kati, lakini baada ya pumzi mpya kumuingia hawa, si kwamba waliusogolea tu, lakini pia wakala na lile tunda. Roho ya mtu iliumbwa kwa mfano wa Mungu, na kiasilika haiwezi kutenda dhambi au kuacha kumtii Mungu, ila roho ngeni zilizo muingia ndio humfanya atende dhambi, ndio maana twaambiwa kuna pepo la uzinifu, uongo, wizi, na kubwa zaidi roho zetu halaumiwi kwa kutenda dhambi bali zinalaumiwa kwa kushindwa vita na shetani.

Kwakuwa ndani ya mwili tayari kuna roho, na kwakuwa hizi roho ngeni[majini] nazo huamrisha mwili, hivyo basi huwa panatokea mashindano mengi ya kiroho ndani ya mwili wa mwanadamu. Vita???

Mwili siku zote hutii ile roho iliyoshinda haijalishi hiyo roho ni ngeni au ile aloumbiwa mwanadamu. Mfano mwanadamu waweza kutoka kuoga kisha ukajikuta uko katika mtihani wa kuchagua nguo ya kuvaa, wakati mwingine waweza kuvaa nguo kabisa kisha ukajikuta waivua na kuivaa nyingine, ila hali ya kuchagua nivae hii au ile ni matokeo ya mashindano ya kiroho ndani ya mwili, Vita?

Hata katika kuchagua mpenzi pia hutokea mashindano ya kiroho ndani ya mwili. Unapochagua mpenzi na kuamua kuishi naye jua kuwa kuna roho imekushinikiza kufanya hivyo na si vinginevyo. Kwakuwa watu wote tuko na roho ngeni nyingi kwenye miili yetu, kwakuwa hizi roho hutofautiana nguvu kulinganana nyakati, na kwakuwa roho yenye nguvu kwenye wakati fulani ndio hutawala kipindi hicho, hivyo basi kiwango cha “mapenzi” ya mwanadamu kwa mwenza wake hubadilika kadiri roho zinazotawala mwili wa mwanadamu huyo zinavyobadilika;hapa ndipo usaliti na kigeugeu vinapozaliwa.

Wakati wampenda mwajuma elewa kuna kiprogramu[roho] ndani ya mwili wako kimekufanya umpende huyo mwajuma, hiyo roho ikizidiwa nguvu hata ikaingia roho ya kumpenda Asha lazima utamuacha mwajuma na kuanza kumpenda Asha. Hizi roho ngeni ndio hupelekea “soulmate” wakati mwingine zisikutane. Kama ile roho ya inayompenda Asha ikiendelea kutawala kwa muda mrefu hata mauti, basi huyo mtu atendelea kumpenda Asha hadi kifo chake.

Cha kuzingatia, ile roho inayomfanya John ampende Asha haiwezi kufaulu hadi Asha awe na roho inayompenda John. Ikiwa roho hizi ni "SOULMATE" basi mapenzi ya Asha na John hudumu daima, kama hizi roho si "soulmate" na hivyo mapenzi yao ni matokeo ya roho ngeni[majini] zilizopendana, kwa hivyo mapenzi hayo yatachuja na kupotea kabisa mara baada ya roho hizo kutolewa kwenye utawala na roho zingine.

Roho ngeni namaanisha majini au mapepo. Kila mwanadamu ana majini wengi na kila jini kuna mambo anapenda na kuna mambo anachukia, na kila jina kuna siku yake, mwaka wake na hata muongo wake wa kutawala. Pia kila jini ana nguvu zake za kikawaida alizoumbwa nazo na kuna majini wengine wana nguvu za ziada(uchawi)

MWISHO:
katika yote hayo juu, naomba rejea kitendo cha Kefa kumkana Yesu mara tatu, rejea usaliti wa Yuda Iskariote kwa Yesu, rejea vita vya maswahaba baada kifo cha Mtume Muhammad(s.a.w), pia rejea maisha yako kila siku. Utabaini bila jelezi kuwa usaliti, kigeugeu, mapenzi, urafiki, nk vinatawaliwa na majini na roho, na kwasababu hiyo miili yetu haina hiyari hata kidogo.

Siku nyingine nitafafanua uhusiano kati ya majina yetu na mahusiano mapenzi na ndoa. Kwanini watu wengine huchezesha herufi za majina yao au hubadili majina kabisa kwa lengo la kuimarisha ndoa na mahusiano.

PENZI JINI HATARI.
1
Penzi ni jini hatari, wa kutesa na kuua,
Huzibeba zote shari, za kiangazi na mvua,
Nina kuomba Qahari, miye asije niua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
2
Penzi mganga mzuri, huponya wanougua,
Hukusanya nyingi heri, za mwezi hata za jua,
Kwa idhini Ya Jabari, aponye changu kifua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
3
Mapenzi istiimari, hakika nimetambua
Baridi naona hari, meli mwenzenu mashua,
Asali kwangu shubiri, ninajuta kuyajua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
4
Mapenzi ni zingifuri, kwa mja anayejua,
Narauka Alfajiri, naswali naomba dua,
Yarabi penzi la siri, lisije kuniumbua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
5
Penzi si kama johari, huwezi kulinunua,
Si mchanga wa bahari, bure ukalichukua,
Thamaniye si mahari, mkaja hata jazua.
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
6
Penzi halina jabari, si chuma la kuinua,
Uwe bondia hodari, pia laweza sumbua,
Huba zataka sukari, moyo upate kutua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
7
Mapenzi jua qadari, uwaze na kuwazua
Alo lipanga Ghafuri, hakuna wa kupangua,
Hivyo hatuna hiyari, hata kama twaamua
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
8
Mapenzi si kibatari, ni mshumaa tambua,
Nyonda apate fahari, mwenyewe unaungua,
Yengekuwa samsuri, wallahi ningeyavua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Whatspp/call 0622845394

BINT WA DESMOND TUTU AVULIWA UKASISI KWA KUOA MWANAMKE MWENZAKE.

Binti wa Desmond Tutu, kiongozi mashuhuri wa Kikristo wa Afrika Kusini amevuliwa joho la Ukasisi baada ya kuoa mwanamke mwenzake.

Uongozi wa Kanisa la Anglikana nchini humo umesema, Mchungaji Mpho Tutu-van Furth, Padri wa kanisa hilo amepokonywa leseni ya kuendesha shughuli za kanisa hilo ikiwemo misa, ubatizaji, ndoa na maziko kwa kuwa kanuni za kanisa hilo haziruhusu ndoa za jinsia moja.

Binti huyo amesema babake Desmond Tutu, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Angilkana nchini humo na pia mwanamapambano mashuhuri wa sera za kibaguzi hajashangazwa na habari hizo ingawa hazijafurahia.

Mpho Tutu alifunga ndoa na raia wa Uholanzi kwa jina Marceline, ambaye ni Profesa wa Tiba ya Watoto huko jijini Amsterdam Disemba mwaka jana, huku sherehe za harusi zikifanyika mjini Cape Town nchini Afrika Kusini mapema mwezi huu. Wanandoa hao waliwahi kuolewa huku nyuma na wote wana watoto.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, licha ya kuwa Kanisa la Angilikana linapinga liwati na usagaji, lakini Afrika Kusini iliidhinisha ndoa za jinsia moja mwaka 2006.

NDEGE YA MISRI ILIDUNGULIWA NA ISRAELI?

Uwezekano kuwa ndege ya abiria ya Misri iliyotoweka hivi karibuni ilitunguliwa na ndege za kivita za Israel, umezidi kupata nguvu.

Gazeti la al Misri al Yaum limeandika kuwa, uchunguzi unaonesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa ndege ya abiria ya Egypt Air ilitunguliwa na ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Matamshi rasmi ya viongozi wa Ugiriki kuhusiana na ajali ya ndege ya abiria ya Misri na sababu zake, yamekwepa kwa makusudi kutaja mazoezi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni yaliyokuwa yanafanyika kusini mwa kisiwa cha Crete cha Ugiriki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mazoezi hayo ya kijeshi yalifanyika katika kalibu ya mpango wa mafunzo ya ndege za kivita za Israel kwa kutumia mipaka ya angani ya Ugiriki na katika mpaka wa Misri na Libya. Israel iliiomba pia Uturuki iruhusu kutumia anga yake, lakini Uturuki ilikataa.

Gazeti hilo la Misri limeongeza kuwa, ramani ya eneo la mazoezi hayo ya ndege za Israel inaonesha kuwa, ndege hiyo ya Misri ilipita katika eneo hilo wakati mazoezi yakiwa yanaendelea na ilitoweka katika rada dakika 27 baada ya kuanza mazoezi hayo ya kijeshi ya Israel.