MOHAMMAD PAKPOUR: MAREKANI NA SAUDIA ZILITUMA MAGAIDI KUSHAMBULIA IRAN.

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC amesema wanachama wa magenge ya kigaidi waliokamatwa hivi karibuni hapa nchini wakipanga njama za kutekeleza mashambulizi ya bomu wamekiri kwamba walipokea ufadhili kutoka Saudi Arabia na Marekani.

Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour, kamanda wa kikosi cha ardhini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran amesema magaidi hao wamekiri kuwa walifadhiliwa na nchi mbili hizo ili kujenga ngome hapa nchini na haswa katika maeneo ya mipakani kwa shabaha ya kutekeleza hujuma za kigaidi katika kona mbali mbali ya nchi.

Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema Washington na Riyadh zimekuwa zikiyafadhili na kuyaunga mkono magenge ya kigaidi kwa lengo la kuyumbisha usalama wa nchi sambamba na kusambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu, njama ambazo amesema hazitazaa matunda.

Amongeza kuwa, mmoja wa magaidi hao waliokamatwa wiki jana katika mji wa Khash mkoani Sistan-Baluchistan ameaga dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa operesheni ya kusambaratisha ngome yao.

Waziri wa Usalama Iran Mahmoud Alavi siku chache zilizopita alisema magaidi wakufurishaji waliokamatwa hivi karibuni walipanga kutekeleza mashambulizi katika maeneo 50 kote Iran na haswa mji mkuu Tehran.

Amesema kuwa magaidi hao walikuwa wameshaainisha maeneo 50 ya kutega mabomu na kwamba tayari walikuwa na kilo 100 za mada za miripuko; huku vikosi vya usalama vikifanikiwa kuzuia tani mbili za mada hizo ambazo magaidi walipanga kuingiza nchini.

Mbali na kukamata magaidi 10 miongoni mwao, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC liliangamiza magaidi watano wa kundi la kigaidi la PJAK kaskazini magharibi mwa nchi. Vikosi vya usalama na ulinzi nchini vimetibua mashambulizi kadhaa ya kigaidi katika muda wa siku chache zilizopita.