NDUGU ZANGU NAWAJUA, SITAKI KUKUMBUSHWA.





                 NDUGU ZANGU NAWAJUA.
1.     Nimejifunza si haba, natambua ndugu zangu,
Kuna dhahabu na shaba, najua tamu na chungu,
Hasidi nimpe huba, sitathubutu wenzangu,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua.

2.     Nasema ninawajua, kwa marefu na mapana,
Nao pia wanijua, kwa usiku na machana,
Iwe mvua ama jua, wenyewe tunashikana,
Sihitaji kukumbushwa, somo zangu nawajua.

3.     Simung’unyi nawajua, leo niwape yakini,
Muwache kujizuzua, suhuba pake moyoni,
Mkome kujifutua, sifa zitawaueni
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

4.     Mjue vitendo vyenu, vizuri mseme navyo,
Tegeni sikio zenu, msikie msemwavyo,
Naogopa kula chenu, sitaki kusemwa ovyo,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

5.     Wa kushoto usijue, kuvuli katoa nini,
Hino ibada mjue, kwa mola wetu Manani,
Ushetani mtambue, kutangaza hadharani,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

6.     Mtoa kitu kwa ria, huvaa vazi la mungu,
Adhabu tamshukia, aja lia kwa uchungu,
Hapa kikomo natia, nafunga kitabu changu,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

          Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5
          Mzalendo.njano5@gmail.com
          0784845394/0762845394
          Morogoro Tanzania