UKIONACHO NDOTONI.








  






        


UKIONACHO NDOTONI.

Kiona choo ndotoni, kiumbe sikitumie,
Haja iwe mlangoni, kazana ishikilie,
Tena fanya hukioni, shukani siyaachie.
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Kiona kiza ndotoni, mwenzangu usiumie,
Mfano mwanga uoni, pambana ukufikie,
Swali utoke shimoni, Rabi akuangazie
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Kiona simba ndotoni, naomba simkimbie,
Mrukie mgongoni, kipando ujifanyie,
Uwatazame usoni, maadui wazimie,
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Kiona swala ndotoni, kichale umnyatie,
Sije zama mtegoni, kijanja mkaribie
Mtazame pasi soni, asiwe chui ulie,
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Dotto Rangimoto Chamchua.(Njano5)
mzalendo.njano5@gmail.com
0762845394/0784845394
Morogoro Tanzania

NDUGU ZANGU NAWAJUA, SITAKI KUKUMBUSHWA.





                 NDUGU ZANGU NAWAJUA.
1.     Nimejifunza si haba, natambua ndugu zangu,
Kuna dhahabu na shaba, najua tamu na chungu,
Hasidi nimpe huba, sitathubutu wenzangu,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua.

2.     Nasema ninawajua, kwa marefu na mapana,
Nao pia wanijua, kwa usiku na machana,
Iwe mvua ama jua, wenyewe tunashikana,
Sihitaji kukumbushwa, somo zangu nawajua.

3.     Simung’unyi nawajua, leo niwape yakini,
Muwache kujizuzua, suhuba pake moyoni,
Mkome kujifutua, sifa zitawaueni
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

4.     Mjue vitendo vyenu, vizuri mseme navyo,
Tegeni sikio zenu, msikie msemwavyo,
Naogopa kula chenu, sitaki kusemwa ovyo,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

5.     Wa kushoto usijue, kuvuli katoa nini,
Hino ibada mjue, kwa mola wetu Manani,
Ushetani mtambue, kutangaza hadharani,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

6.     Mtoa kitu kwa ria, huvaa vazi la mungu,
Adhabu tamshukia, aja lia kwa uchungu,
Hapa kikomo natia, nafunga kitabu changu,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

          Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5
          Mzalendo.njano5@gmail.com
          0784845394/0762845394
          Morogoro Tanzania


ORODHA YA WALIOKWEPA KULIPA KODI.














Orodha ya waliokwepa kulipa kodi makontena 329 yaliyoikosesha serikali 80b
1. Lotai Steel Tanzania Ltd iliyokuwa na makontena 100,
2. Tuff Tryes Centre Company 58,
3. Binslum Tyres Company Ltd 33,
4. Tifo Global Mart Company Limited 30,
5. Ips Roofing Company Limited 20,
6. Rushywheel Tyre Centre Co Ltd 12,
7. Kiungani Trading Co Ltd 10.
8. Homing International Limited (9),
10. Red East Building Materials Company Ltd (7),
11. Tybat Trading Co Limited (5),
12. Zing Ent Ltd (4),
13. Juma Kassem Abdul (3),
14. Salum Link Tyres (3),
15. Ally Masoud Dama (2),
16. Cla Tokyo Limited (2),
17. Farid Abdullah Salem (2),
18. Salum Continental Co (2),
19. Zuleha Abbas Ali (2)
20. Snow Leopard Building (2).

Wamiliki wengine wa makampuni ambayo yalikuwa na kontenta moja moja ni Abdulaziz Mohamed Ally, Ahmed Saleh Tawred, Ali Amer, Ally Awes Alhamdany, Awadhi Salim Saleh, Fahed Abdallah Said, Hani Said, Hassan Husrin Suleyman, Humud Suleiman Humud, Kamil Hussein Ali na Libas Fashion.
Wengine ni Nassir Salehe Mazrui, Ngiloi Ulomi Enterprises Co Ltd, Omar Hussein Badawy, Said Ahmad Hamdan, Said Ahmed Said, Salumu Peculier Tyres, Sapato N. Kyando, Simbo Yonah Kimaro, Strauss International Co. Ltd na Swaleh Mohamed Swaleh.
Orodha hiyo inafanya jumla ya makontena 329 ambayo yaliondolewa kinyume cha taratibu kutoka ICD ya Azam inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa And Company Limited.
Bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo ni pamoja na matairi ya magari, samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa zingine mchanganyiko.

LEO NAVUNJA KIBUBU!


















LEO NAVUNJA KIBUBU!
1
Leo navunja kibubu, pesa ninunue khanga,
Apendeze mahabubu, kama binti wa kitanga
Atokapo awe bubu, washindwe wano jigonga
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
2
Sasa navunja kibubu, nipate nunua kanga,
Ale ashibe muhibu, kitoweo si mchunga,
Usiku tule kababu, uji pilipilimanga,
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
3
Mimi navunja kibubu, nikagule kungumanga,
Nimpatie tabibu, mafusho toka Umanga,
Nimuenzi taratibu, niseme na zake nyonga
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
3
Mie navunja kibubu, habibi apate shanga,
Mapambo yake dhahabu, vidoleni na kitanga,
Sawa nipate adhabu, apendeze wangu ninga,
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
4
Njano navunja kibubu, lengo niweze kujenga,
Nyumba isiwe na tabu, mahaba yatie nanga,
Penzi lataka adabu, siwezi kulibananga,
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba


Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
0784845394/0762845394
mzalendo.njano5
Morogoro Tanzania