UKIONACHO NDOTONI.








  






        


UKIONACHO NDOTONI.

Kiona choo ndotoni, kiumbe sikitumie,
Haja iwe mlangoni, kazana ishikilie,
Tena fanya hukioni, shukani siyaachie.
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Kiona kiza ndotoni, mwenzangu usiumie,
Mfano mwanga uoni, pambana ukufikie,
Swali utoke shimoni, Rabi akuangazie
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Kiona simba ndotoni, naomba simkimbie,
Mrukie mgongoni, kipando ujifanyie,
Uwatazame usoni, maadui wazimie,
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Kiona swala ndotoni, kichale umnyatie,
Sije zama mtegoni, kijanja mkaribie
Mtazame pasi soni, asiwe chui ulie,
Yataka uzingatie, uyaonayo ndotoni.

Dotto Rangimoto Chamchua.(Njano5)
mzalendo.njano5@gmail.com
0762845394/0784845394
Morogoro Tanzania

NDUGU ZANGU NAWAJUA, SITAKI KUKUMBUSHWA.





                 NDUGU ZANGU NAWAJUA.
1.     Nimejifunza si haba, natambua ndugu zangu,
Kuna dhahabu na shaba, najua tamu na chungu,
Hasidi nimpe huba, sitathubutu wenzangu,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua.

2.     Nasema ninawajua, kwa marefu na mapana,
Nao pia wanijua, kwa usiku na machana,
Iwe mvua ama jua, wenyewe tunashikana,
Sihitaji kukumbushwa, somo zangu nawajua.

3.     Simung’unyi nawajua, leo niwape yakini,
Muwache kujizuzua, suhuba pake moyoni,
Mkome kujifutua, sifa zitawaueni
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

4.     Mjue vitendo vyenu, vizuri mseme navyo,
Tegeni sikio zenu, msikie msemwavyo,
Naogopa kula chenu, sitaki kusemwa ovyo,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

5.     Wa kushoto usijue, kuvuli katoa nini,
Hino ibada mjue, kwa mola wetu Manani,
Ushetani mtambue, kutangaza hadharani,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

6.     Mtoa kitu kwa ria, huvaa vazi la mungu,
Adhabu tamshukia, aja lia kwa uchungu,
Hapa kikomo natia, nafunga kitabu changu,
Sihitaji kukumbushwa, ndugu zangu nawajua

          Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5
          Mzalendo.njano5@gmail.com
          0784845394/0762845394
          Morogoro Tanzania


ORODHA YA WALIOKWEPA KULIPA KODI.














Orodha ya waliokwepa kulipa kodi makontena 329 yaliyoikosesha serikali 80b
1. Lotai Steel Tanzania Ltd iliyokuwa na makontena 100,
2. Tuff Tryes Centre Company 58,
3. Binslum Tyres Company Ltd 33,
4. Tifo Global Mart Company Limited 30,
5. Ips Roofing Company Limited 20,
6. Rushywheel Tyre Centre Co Ltd 12,
7. Kiungani Trading Co Ltd 10.
8. Homing International Limited (9),
10. Red East Building Materials Company Ltd (7),
11. Tybat Trading Co Limited (5),
12. Zing Ent Ltd (4),
13. Juma Kassem Abdul (3),
14. Salum Link Tyres (3),
15. Ally Masoud Dama (2),
16. Cla Tokyo Limited (2),
17. Farid Abdullah Salem (2),
18. Salum Continental Co (2),
19. Zuleha Abbas Ali (2)
20. Snow Leopard Building (2).

Wamiliki wengine wa makampuni ambayo yalikuwa na kontenta moja moja ni Abdulaziz Mohamed Ally, Ahmed Saleh Tawred, Ali Amer, Ally Awes Alhamdany, Awadhi Salim Saleh, Fahed Abdallah Said, Hani Said, Hassan Husrin Suleyman, Humud Suleiman Humud, Kamil Hussein Ali na Libas Fashion.
Wengine ni Nassir Salehe Mazrui, Ngiloi Ulomi Enterprises Co Ltd, Omar Hussein Badawy, Said Ahmad Hamdan, Said Ahmed Said, Salumu Peculier Tyres, Sapato N. Kyando, Simbo Yonah Kimaro, Strauss International Co. Ltd na Swaleh Mohamed Swaleh.
Orodha hiyo inafanya jumla ya makontena 329 ambayo yaliondolewa kinyume cha taratibu kutoka ICD ya Azam inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa And Company Limited.
Bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo ni pamoja na matairi ya magari, samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa zingine mchanganyiko.

LEO NAVUNJA KIBUBU!


















LEO NAVUNJA KIBUBU!
1
Leo navunja kibubu, pesa ninunue khanga,
Apendeze mahabubu, kama binti wa kitanga
Atokapo awe bubu, washindwe wano jigonga
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
2
Sasa navunja kibubu, nipate nunua kanga,
Ale ashibe muhibu, kitoweo si mchunga,
Usiku tule kababu, uji pilipilimanga,
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
3
Mimi navunja kibubu, nikagule kungumanga,
Nimpatie tabibu, mafusho toka Umanga,
Nimuenzi taratibu, niseme na zake nyonga
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
3
Mie navunja kibubu, habibi apate shanga,
Mapambo yake dhahabu, vidoleni na kitanga,
Sawa nipate adhabu, apendeze wangu ninga,
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba.
4
Njano navunja kibubu, lengo niweze kujenga,
Nyumba isiwe na tabu, mahaba yatie nanga,
Penzi lataka adabu, siwezi kulibananga,
Mniache nayajenga, mkome kunita zoba


Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
0784845394/0762845394
mzalendo.njano5
Morogoro Tanzania

RAIS AMSIMAMISHA KAZI KAMISHNA MKUU TRA























RAIS AMSIMAMISHA KAZI KAMISHNA MKUU TRA

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano - Ikulu imesema kuwa alasiri ya leo, Rais Dk. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Rished Bade.

Rais amemteua Kamishna Phillip Mpango kukaimu nafasi hiyo; na amemtaka Rished Bade kumpa ushirikiano Mpango hasa katika kutafuta ukweli kuhusu makontena 349 yenye thamani ya shilingi bilioni 80/= yaliyotoweka bandarini pasipo TRA kuwa na kumbukumbu zozote za makontena hayo.

VIGOGO WA TRA WAKUTANA NA MOTO WA MAJALIWA.












Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa leo ameamuru kukamatwa kwa maafisa kadhaa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wengine kufukuzwa kazi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza Bandarini na kukuta madudu ambayo hakuyafurahia.
Maafisa hao, ambao kwa sasa tunahifadhi majina ili Jeshi la Polisi liweze kuwashughulikia, wametakiwa pia kusalimisha hati zao za usafiri.

Hii imekuja baada ya kugundulika kwamba kuna makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 80 ambayo data za Mamlaka ya Bandari inazo lakini katika mtandao wa TRA hayaonekani.
Katika Ziara hiyo ya ghafla Waziri mkuu Kasim Majaliwa awasimamisha kazi kamishna wa kodi Tiagi Masamaki na Habibu Mpozya kitengo cha huduma kwa wateja kutokana ubadhilifu wa fedha kwa makontena zaidi ya 300 yaliyopotea.

Wengine ni Haruni Mpande -ICT, Hamisi Ali Omari na Eliachi Mrema incharge wa ICD na amemuru wote wakamatwe uchunguzi uendelee.

HUKUMU YA MAWAZO, MBOWE MPONGEZA JAJI.




HUKUMU YA MAWAZO, MBOWE MPONGEZA JAJI.
leo mahakama ya Tanzania imetenda haki kama ilivyo elezwa na mwenyekiti wa CHADEMA ndugu Freeman Freeman Aikaeli Mbowe.
Ndugu wa mawazo, marafiki, na wanachama wwnzake wameruhusiwa kutoa heshima zao za mwisho kwa mawazo, katika uwanja ambao watakubalina kati ya CHADEMA, ndugu na polis.
Kwa kwa muda wa siku mbili sasa kumekuwa majibishano ya kisheria kati ya jeshi la polis na familia ya Mawzo iliyo wakilishwa na wakili Mallya, majibishano hayo yalitangiliwa na sinto fahamu ya namna ya kuagwa na kuzikwa kwa Mawazo baada ya jeshi la polis kuzuia mkusanyiko mkubwa wa watu kwa sababu ya tishio la kipindupindu.

MARUFUKU KUTENGENEZA KADI ZA X MAS KWA GHARAMA ZA SERIKALI.


Sijui kesho tutasikia nini maana yake hii sasa imeshakuwa hatari, ofisi za umma zimekuwa kaa la moto kwa watumishi. Huyo ndio Magufuli,,, ni kazi tu.

URUSI YAZIDI KUONGEZA NGUVU SYRIA.



URUSI YAZIDI KUONGEZA NGUVU SYRIA.

Haya ni magari ya Jeshi la Urusi ya kubeba na kurusha makombora aina ya S-400 Triumf ambayo yanapiga toka ardhini kwenda angani , hivi sasa yanaelekea huko Latakia , Syria katika kambi ya Jeshi la Urusi inayohusika na mashambulio dhidi ya makundi ya kigaidi huko Syria na Ira qi .

Urusi imefanya hivyo baada ya ndege yake aina ya Sukhoi Su-24 kutunguliwa na Uturuki juzi.
Mfumo huu wa makombora unauwezo wa kupambana na maadui 300 kwa wakati mmoja , Pia wanapeleka Makombora yanayoongozwa na meli yanayoitwa Moskva karibu na pwani ya Syria sehemu ambayo ni Karibu kabisa na Uturuki .

AJIRA SERIKALINI SASA KWA MKATABA WA MUDA MAALUMU:


AJIRA SERIKALINI SASA KWA MKATABA WA MUDA MAALUMU:
Atakayefanya vizuri ataendelea na mkataba, atakayevurunda kufutwa kazi mara moja.
Taarifa kuhusu mpango wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano kuzifanyia mabadiliko makubwa sheria za Utumishi wa Umma kwa kuondoa kipengele cha Ajira ya Kudumu (Permanent Employment Contract) kimepokewa kwa hisia chanya na jamii.

Kwa miongo mingi utendaji katika sekta ya Utumishi wa Umma umekuwa ukilegalega, kuzorota na kutokuwa wa ufanisi kiasi sio tu mara kadhaa umepelekea kuingiza Serikali katika hasara ya mabilioni ya shilingi lakini pia imekuwa sababu ya kero kubwa kwa wananchi wanaokosa huduma na maamuzi stahiki katika ofisi za umma.

Sababu kuu inayotajwa kuchangia uzembe, utoro, uvivu, kutowajibika, ufujaji wa fedha za umma, manyanyaso kwa wananchi, ulevi, wizi, rushwa, ufisadi, undugunization n.k ni kwa kuwa baadhi ya watendaji hawa wa umma mikataba yao ya ajira ilikuwa ni ya kudumu na yenye pensheni (Permanent and Pensionable).

Kigezo hiki cha permanent and pensionable kimekuwa kikitumiwa vibaya sana na baadhi ya watendaji kwenye ofisi za umma kufanya kazi vile wanavyotaka wao. Hata inapobainika mfanyakazi ni mzembe kabisa kabisa ambaye hawezi kutimiza majukumu yake kumfukuza kazi linabaki kuwa jambo gumu sana ambalo hata Waziri hawezi na wengi huishia kuhamishwa vituo vyao vya kazi na kuendelea na matendo yao yasiyo na ufanisi katika utumishi.

Bunge kama chombo cha kutunga sheria kinapaswa bila woga kutimiza majukumu yake ikiwemo kurekebisha kwa kufuta vipengele vyote vya sheria ya Utumishi wa Umma ambavyo vimekuwa kichaka kwa baadhi ya watumishi kufanya mambo ya hovyo wakiamini hawagusiki.
Bunge likifanikiwa kuziboresha sheria hizi za Utumishi wa Umma tunaamini zitasaidia kurejesha Nidhamu Kazini, kuongeza ari ya Uwajibikaji, kuondoa migongano, migogoro, kupunguza hasara kwa Serikali zisizo za lazima, kutoa mwanya kwa watendaji wenye sifa kidhi kuajiriwa katika sekta ya umma na kusukumu mbele gurudumu la Maendeleo.

Miaka ya 1980's kulikuwa na kibao mashuhuri chenye maneno;
"Nidhamu ya Kazi ni msingi wa mafanikio mema kazini, viongozi na wafanyakazi, lazima wote muwe na nidhamu.
Migogoro na migongano makazini ni ukosefu wa nidhamu".
Katika kuifumua na kuisuka upya nchi yetu, tunaunga mkono juhudi zote njema zenye kulenga kuwa na Taifa lenye kuzingatia misingi ya Uzalendo, Uwazi, Uwajibikaji, Uadilifu, Umoja, Udugu, Utu na Utawala wa Sheria.
Viva Tanzania! Viva!

MAPENZI SI MAFURUSI.
















 MAPENZI SI MAFURUSI.
1.
Katu hapandi farasi, yule mzoea punda,
Mpenda kwenda kasi, mwendo pole humshinda,
Amezoweshwa fenesi, doriani lamshinda,
Sitokalifisha nafsi, nafanya ninayopenda,
Mie nina wasiwasi, kwa mambo yanavyo kwenda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
2.
Nipe gongo ya kiasi, nipate ipiga funda,
Na miraa ya Ramisi, kwa ubani naifunda,
Initoe wasiwasi, hata kipoe kidonda,
Niupate na wepesi, wa kumshukia nyonda,

Natambua si rahisi, kutamka "nakupenda"
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
3.
Niko na pepo za kusi, ni mbali ninapo kwenda,
Nausaka mdungusi, ukame 'sikose tunda,
Wenye kupendwa wakwasi, kila kiwanja hudunda,

Niache kikaragosi, nilo nayo yanishinda,
Mkononi sina tasi, n’nani atanipenda?
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
4.
Waja wataka fususi, hawana kitu kupenda,
Ubishi kama chunusi, natafuta pa kupanda,
Aso tabia za fisi, wallahi nitampenda,
Mwenye kujali nafsi, mafurusi kuyaponda,
Mapenzi ya wasiwasi, yatesa kama kidonda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
5.
Moyo una wasiwasi, akili i'njia panda,
Huyu mja Ibilisi, ni jini msaka tenda,
Kila siku alhamisi, kwake siku huganda,
Kuna siku za mafurusi, na za mifuko kukonda,
Si kuna siku nyepesi, na za kukaza mkanda?
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
6.
Hili jua la utosi, kila mtu humtenda,
Hata mwenye ukwasi, pia laweza mponda,
Ya jini kuhama rasi, kitie anapo konda,
Mwayaiga pasi wasi, ya majini mwayatenda,
Kwa talasimu za ngisi, mioyo mnaiwinda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
7.
Sina hofu sina wasi, tena nenda mwana kwenda,
Kisu changu kimepasi, hakiyumbi kimedinda,
Hupati tena nafasi, dagaa zangu kutanda,
Nimestushwa na unyasi, nyoka alinipa donda,
Nimestuka kirahisi, we endelea kutanda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5)
Mzalendo.njano5@gmail.com
784845394/764845394
Morogoro Tanzania.

SIASA MJUE NJIA, MAAMUZI KUFIKIA.












SIASA MJUE NJIA, MAAMUZI KUFIKIA.
1
Nimezama mwituni, kumtafuta mnyama,
Mwenye nguvu duniani, leo na kesho kiama,
Atajwa msikitini, kanisani wa msema,
Haliwi jambo mwituni, bila ya huyo mnyama.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
2
Naanzia shuleni, watoto wanaposoma,
Wanao soma vyuoni, na shahada za heshima,
Ngumbaru ipo kundini, unyago akina mama,
Elimu yetu nchini, huongozwa na mnyama.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
3
Uende sipitalini, na walipo wakulima,
Kwenye sekta ya madini, na kwa wapiga ngoma,
Utalii wa mbugani, uchezaji wa sinema,
Kote huko tambueni, mratibu ni mnyama.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
4
Siasa ndio mnyama, Lutumbo katuambia,
Siasa ni kitu chema, katika yetu dunia,
Siasa njia ya umma, maamuzi kufikia,
Siasa si kama sima, bali maji nawaambia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
5
Siasa kitu lazima, katu huwezi kimbia,
Waweza ikacha sima, maji huwezi susia,
Hata ngazi ya boma, siasa waitumia,
Siasa ukiitema, jua umeangamia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
6
Kuna siasa ya chama, kimoja nawaambia,
Kila shauri la umma, chama hujiamulia,
Bunge huwa maamuma, muhuri hushikilia,
Jambo lipite kwa Chama, bunge lalishadidia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
7
Zipo za demokrasia, vyama vingi nawambia,
Mfano za Tanzania, na uingereza pia,
Vyama hushindania, magogoni kuingia,
Rais kwa Tanzania, waziri kwa malikia
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
8
Siasa ndani ya vyama, huko hazikuanzia,
Ilianza toka zama, kabla ya hino dunia,
Furkani nimeisoma, sikuiacha biblia,
Malaika na Karima, pia wanaitumia,
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
9
Siasa za huko ahera, kiongozi ni Jalia,
Huongoza msafara, waja wakafuatia,
Mwenye kufanya harara, jeuri akajitia,
Atakuwa ni asira, wa shetani nawambia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
10
Muumba ndio kinara, wa mbinguni na dunia,
Maisha huyachora, na njia hutupangia,
Hupata njema ijara, mwenye kumsujudia,
Hupata kubwa hasara, mwenye kupuuzia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
11
Nani alipiga kura? Munguwe kumchagua,
Mjibu pasi kufura, kweli mpate ijua,
Hapana si masihara, si punde mtagundua,
Tena sifanye papara, siasa kuchambua.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
12
Siasa za kifalme, mfano za Saudia,
Mwana hasa wa kiume, kiti ndio hukalia,
Koo iloshika kome, dola huishikilia,
Mfalme ndio sime, na pia huwa pazia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
13
Zipo za kidikteta, kama zile za Mobutu,
Wengine panga hufuta, pia wapo wa mtutu,
Umma wote hufyata, mbele ya miungu watu,
Kila mwenye kutukuta, ni mbwa mbele ya chatu.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
14
Dikteta awe katili, mbona mtaumwa sana,
Siombe awe jahili, mtapoteza amana,
Tena akiwa bahili, wananchi hukondeana,
Kiongozi bahaluli, asiaminiwe tena.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
15
Samaki awape nyoka, mkate awape mawe,
Nani kashindwa ondoka, kisa halina mauwe?
Ya msingi wanataka, viongozi waelewe,
Wakichoka kuboboka, watawapopoa mawe.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
16
Dikteta awe rahimu, ndipo mtanufaika,
Rasini awe timamu, na tena mshaurika,
Mtakula keki tamu, mafurushi mtashika,
Tripoli yajilaumu, Gaddafi kudondoka.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
17
Nikitazama chupani, sioni kitu jamani,
Wino wangu wa thamani, ya manjano zafarani,
Niko mengi rasini, wino umetufitini,
Mwenye nao sinihini, naomba niuzieni
Mmeshindwa nidhamini, kwa kifupi kwaherini.

Dotto Chamchua Rangimoto (Njano5)
mzalendo.njano5@gmail.com
0715845394/0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania.