NDONDO SI CHURURU

NDONDO SI CHURURU.                                  
 1
Ndondondo sio chululu, najua maneno yao,
Waona wamefaulu, ati silingani nao,
Tena waniita mbulu, nisitie guu kwao,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.

2
Nasemwa mvaa moja, mi kauka nikuvae,
Kutoka kwangu si haja, tuli nyumbani nikae,
Ati tafanya kiroja, kiasi wanikatae,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
3
Nami nitajikusuru, nitalima na miraba,
Kikubwa sitakufuru, tamuomba mungu baba,
Hata hivyo nashukuru, ninachopata si haba,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
4
Huwezi kupata kenda, bila kuanza moya,
Sijitii mbio kwenda, nachelea vunja taya,
Lolote waweza tenda, kwa paka hupati paya,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
5
Sikitaki cha kuiba, kilijaze tumbo langu,
Silipendi la kahaba, lisonisha hamu yangu,
Maovu hayawi tiba, kutibu kichomi changu,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
6
Ingawa sijakinai, cha mtu sikitamani,
Hata niwe na nishai, sirukii cha jirani,
Nina dhiki sikatai, na mungu yupo jueni,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania