SIDHARAU, KAZI NI KAZI.

SIDHARAU, KAZI NI KAZI.
                                   
Uza dagaa mchele, piga na kibakubaku,
Wala hupigi kelele, puyanga huko na huku,
Mkeo apike mle, mwidu sitamani kuku.
Sidharau kazi yako, mie sikufai kitu.

Piga debe kwa matatu, mchana hata usiku,
Kwa mbwembwe uite watu, kwa taxi na tukutuku,
Wana wapate viatu, sisaahu na mabuku,
Sidharau kazi yako, mie sikufai kitu.

Lima shamba bila haya, sisononeke moyoni,
Kwa ngiri hupati paya, msufi hauna buni,
Sitegemee cha mbuya, wala sikitumaini,
Sidharau kazi yako, mie sikufai kitu.

Wizi si kazi jamani, utapeli wafaani?
Si kitamu ulimini, cha kuiba kwa jirani,
Hakistiri maungoni, cha kupora madukani,
Kazi ile ya halali, yenye kufaa jamii.


Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania