SASA HAMSINI RASI, HAMSINI MAJINUNI.






















SASA HAMSINI RASI, HAMSINI MAJINUNI
                                               
1.
Niko na wino chupani, na ujiti mkononi,
Naandika ya moyoni, yalo nifika jamani,
Sikuwahi kuamini, kuna viumbe majini,
Visasili vya zamani, ndivyo nilivyodhani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni
2.
Naanzia mwishoni, nilipokaa jamvini,
Fatma bint Subiani, akipandishwa rasini,
Niliketi kitangani, na chano kiko pembeni,
Lewa iko kilingeni, yanapungwa malohani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
3.
Mloketi upenuni, na wa mbali sogeeni,
Muingie uwanjani, tuyapunge malohani,
Kiti apate amani, imtoke mitihani,
Alisema hadharani, Kachiki bint Ngonyani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
4.
Kachiki bint Ngonyani, aso mjua ni nani,
Wanasiasa nchini, na wauzaji sokoni,
Hufika kwake nyumbani, wapate ndele usoni,
Anaishi Magomeni, pale Kilosa Mjini,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
5.
Mshike vya mikononi, vilaji vya malohani,
Kitezo na zafarani, na udi wa malohani,
Manenane na ubani, na uvumba wa majini,
Shime viwepo chanoni, ni muhimu si utani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
6.
Maji ya zamda chupani, sanamaki ya kusini,
Uzire, giligilani, na vizimba vya barani,
Mafuta ya asumini, na mkongojo wa jini,
Ada za bint Sultani, visikose kitangani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni
7.
Rabi Mola Sultani, Muumba wa mitihani,
Raha, dhiki na huzuni, majaliwa ya Manani,
Ameumba mashetani, kwa siku ya ushetani?
Kaweka mwiba njiani, ili umchome nani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
8.
Niwe na mbawa tisini, nipae hata mbinguni,
Na nifike arshini, nitabaki kuwa chini,
Kudura haiwi chini, huwa juu tambueni?
Upatalo duniani, limeandikwa zamani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
9.
Fatma mwana wa jini, ndio wangu mtihani.
Kwani niko shubuani, sijui nifanye nini,
Habanduki ubavuni, wala hatoki rasini.
Nifanyeje wenzanguni, initoke mitihani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
10.
Nimezama vitabuni, kazi za wanazuoni,
Biblia na furukani, maandishi ya zamani,
Naitafuta yakini, iliyopo vitabuni.
Hukumu yake n’ nini, sijaipata jamani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
10.
Fatma wewe ni nani, na hasa wataka nini?
Vilaji vipo chanoni, sema sasa ya moyoni,
Au nichore baoni, nijue ya ghaibuni?
Wewe ni wa baharini, au wale wa barani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
11.
Haya sasa sogeeni, msikie ya moyoni,
Ninayo mengi mtimani, yalo nifika zamani,
Sitochora ubaoni, kusema ya kifuani,
Haya yangu ya nguoni, wa kuyasema jirani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
12.
Ninayo mengi mtimani, yalo nifika zamani,
Nilikuwa darasani, mwaka ule wa huzuni,
Nikapigwa kichogoni, kiza nikawa sioni,
Kisunzu tele mwilini, puu nikabwagwa chini.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
13.
Kabla sijabwagwa chini, nilimuuliza jirani,
Aliyenipiga nani, cha mno hasa ni nini?
Nimewakera nini, hata nipigwe kichwani.
Wakanicheka jamani, nikaihisi tafrani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
14.
Dotto uko na nini? Akanishika begani,
Aliyekupiga nani? amekupiga na nini?
Una mawazo gani? Una wazimu kichwani?
Akaiomba amani, nisiizue tafrani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
16.
Nilipoanguka chini, Nikawa niko ndotoni,
Niko mwenyewe njiani, nchi ya ughaibuni,
Nakimbizwa na manyani, wenye mawe mikononi,
Nikasemea moyoni, Lile si Joka jamani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
17.
Joka hili joka gani? Mwenye kipembe kichwani,
Ana shanga shingoni, pete tano mkiani,
Mwale wa moto machoni, moshi watoka puani,
Akazichochea kuni, kwa kuungana na nyani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
18.
Nilisoma vitabuni, habari ya maluuni,
Mwenye kipembe kichwani, ndiye huyo maluuni?
Aliyezua tafrani, duniani na mbinguni,
Ana matobo kichwani, hana jema asilani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
19.
Mwenye pembe kichwani, alifukuzwa mbinguni,
Akashuka duniani, kama Amiri jeshini,
Watu hawaelewani, kisa huyu punguani,
Nilo soma vitabuni, leo dhahiri machoni,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
20.
Mwenye kipembe kichwani, likaungana na nyani,
Loo! niko hatarini, kutolewa duniani.
Na hawa mahayawani, watia ndimi puani,
Nikamuomba Manani, anitoe hatarini.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
21.
Jasho likanimwaika, na miguu ikachoka,
Manyani wakanifika, Joka likanizunguka,
Hakika nilitishika, mwili ukatetemeka,
Mama nikamkumbuka, na yowe likanitoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
22.
Mkojo ukanitoka, bila mwenyewe kutaka,
Mwili wote ukachoka, nikahisi kuanguka,
Li Joka likajisuka, mwili akauzunguka,
Mwili ukasisimka, na woga ukanishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
23.
Sauti zikasikika, ya mifupa kuvunjika,
Nyani wakaongezeka, sijui walipotoka,
Wakawa wakinicheka, vile ninavyoteseka,
Tena wakirukaruka, duara wakizunguka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
24.
Miguu ilinyooka, ulimi ukanitoka,
Shingo ilivutika, koo likakabika,
Mwili ukatetemeka, baridi ikanishika,
Ningeweza kuanguka, ni joka lilonishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
25.
Roho iliangaika, nikahisi yanitoka,
Pumzi ziliathirika, kuruzo lilinitoka,
Mishipa ilipasuka, damu zikachuruzika,
Koo lilinikauka, na kiu ilinishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
26.
Mambo yaso kufika, masikio huyachoka,
Vigumu kuaminika, hadi yata’po kufika,
Kweli nimeona Joka, Baada ya kuzimika,
Hata nilipozinduka, kichwani hakunitoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
27.
Ndotoni nikiteseka, Kwa waja nilizimika,
Nyuso zilifadhaika, huku wakiangaika,
Wapo walonishika, wakisema pepo toka,
Visomo vilifanyika, ili nipate zinduka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
28.
Waliomba kwa Rabuka, ili nipate ponyeka,
Maneno yakanitoka, sauti ikachujika,
Mimi si mwenye kutoka, hapa ndio nimefika,
Fanyeni mnalotaka, katu si mwenye kutoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
29.
Watu waliongezeka, sauti iliwafika,
Dotto nataabika, joka limenizunguka,
Kumbe hovyo naboboka, na sauti zabadilika,
Macho yalinitoka, na shingo ilipindika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
30.
Mrembo aloumbika, sijui alipotoka,
Manyani wakatishika, ajabu wakatoweka,
Joka likafokafoka, na ndimi ilimtoka,
Kipembe kikatamka, mambo yasoelezeka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
31.
Hatua akairuka, haraka akanifika,
Vitisho vyote vya joka, Mrembo hakutishika,
Machoni alinishika, nikayafumba haraka,
Macho yalipofumbuka, nikawa nimezinduka.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
32.
Loo amezinduka, mmoja akasikika,
Damu zinamtoka, ulimi umechanika,
Taratibu kapashika, damu zinaponitoka,
Kumbe hapajachimbika, ni kama amechubuka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
33.
Kivivu nikainuka, tayari kwa kuondoka,
Nguo zilivyochafuka, rangi zilibadilika,
Nyumbani nilifika, si kama niloanguka,
Wale walonipeleka, wala hawakusumbuka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
34.
Wala sikupumzika, nyumbani nilipofika,
Ndugu walonizunguka, niliwatoa mashaka,
Jinsi nilivyoanguka, kuwaficha sikutaka,
Yale yaliyo nifika, wala sikuyafutika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
35.
Wala sikuyafutika, yote yaliyo nifika,
Kisunzu na kuanguka, kiza na kuzimika,
Habari za yule joka, na bint aloumbika,
Wale nyani walozuka, mwisho nilivyozinduka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
36.
Wote walifadhaika, huzuni iliwashika,
Hasa walipokumbuka, Bibi alivyoondoka,
Alianza kudondoka, na kisha akazimika,
Naye aliweweseka, na macho yalimtoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
37.
Kitu alichotamka, Bibi alipozinduka,
Nilizingirwa na Joka, na nyani walonicheka,
Mwanamke alipozuka, machoni akanishika,
Roho nahisi yatoka, akaaga na kuwatoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
38.
Bibi aliyependeka, ndivyo alivyowatoka,
Kifo chake cha mashaka, sasa wakakikumbuka,
Wenzangu hawakutaka, yaleyale kunifika.
Hatimaye wakatoka, nami nikapumzika.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
39.
Jinsi walivyotishika, wala hapakukalika,
Nyumbani wakaondoka, wote wamehamanika
Hofu iliyowashika, mganga wakamsaka,
Wallahi hawakutaka, yale yale kunifika.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
40.
Majani ya mkirika, mizizi ya msanaka,
Buni zilizokauka, na mafuta ya mbarika,
Ndivyo vilivyotumika, mwili wangu kuzindika,
Lengo nipate epuka, matatizo kunifika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Dotto Chamchua Rangimoto.(Njano5.)
255762845394/255762845394
mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania.