MUUNGANO WETU NA NENO

MUUNGANO WETU NA NENO                                        

1
Neno limeota meno, naiona tafarani,
Siyaoni mapatano, sote vipembe kichwani,
Mwana ashikwe mkono, asipotee njiani,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.

2
Hakika nimekubali, heshima kwa muungano,
Usitafute kibali, hubiri utengamano,
Tuwashinde majahili, wanotaka utengano,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
3
Hekima zao wahenga, zimenikumbusha mbali,
Nimezikumbuka ngenga, za wenzetu majahili,
Wanawaza kujitenga, sasa wamekuwa nduli,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
4
Niambie yafaani, maneno ya utengano,
Liwapi yenye thamani, nataka yako maono,
Zanzibar ya Sultani, au wetu Muungano?
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
5
Zanzibar si thamani, kuuzidi muungano,
Tanganyika izikeni, hatutaki utengano,
Mipaka ya wakoloni, isilete mapambano,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno,
6
Tanganyika ni Berlini, ni zao la wakoloni,
Zenj mno ithamini, ni fahari ya Sultani,
Tanzania ya Amani, na Nyerere tambueni,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
7
Tanzania imefuta, mipaka ya wakoloni,
Pomoya imetuleta, wa bara na visiwani,
Waasisi mwawateta, mna wazimu rasini?
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
8
Kila nikiyatazama, naona yako na meno,
Na kinywa mmehasama, ndimi kama msumeno,
Chombo chaenda mrama, chungeni yenu maneno,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.

Dotto Rangimoto Chamchua.(Njano5)
255762845394/255784845394
mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania