SINA HIYARI,SIKO MWENYEWE.

SINA HIYARI,SIKO MWENYEWE.
1
Swadakta kaka Mwimbe,kongole rafiki yangu,
Kwanza karibu mkembe,mlenda na nyanya chungu,
Sharubati ya maembe,yakungoja ndugu yangu.
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
2
Hiyo heshima ya kwetu,ndugu nilokupatia,
Chakula hicho ni utu,na mahaba asilia,
Kukupa nimethubutu,ujue menivutia,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
3
Upupu uloniweka,leo nautia kucha,
Mama aliponitoka, naye baba kuniacha,
Ndipo mengi yakazuka, yasolitosha pakacha,
Natunga yalo nisibu, mengine nabahatisha.
4
Mambo yakawa magumu,hakuna mfano wake,
Kila nifanyalo sumu,niso jua ponyo lake,
Nikaomba kwa Karimu,anihafu mja wake,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
5
Ukaja umaamumu,niso jua chanzo chake,
Vidonge na talasimu,nikapewa usitoke,
Hivyo ikanilazimu,masomo nipumzike,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
6
Kichwa cha chezo chauma,wallahi kinatatiza,
Nikaanza kulalama,na fahamu kupoteza,
MoroSeko nilisoma,kwa tabu nilimaliza,
Natunga yalo nisibu,mengine na bahatisha.
7
Haya yote si urongo,ni kweli yajulikana,
Pale shule ya Mazengo,vitimbi vikaja tena,
Nikatumbukia nyongo,kusoma sitaki tena,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
8
Sijui mauzauza,ama uwendaazimu,
Mrembo ajitokeza,asema shika kalamu,
Tena akasisitiza,asemayo ni muhimu,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
9
Peke yangu namuona,akizileta habari,
Nikaziandika sana,bila kuhisi hatari,
Kusoma alicho nena,kumbe ule ushairi,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
10
Sasa hamsini rasi,hamsini majinuni,
Ni kisa kichoakisi,yalotokea zamani,
Namshukuru Qudusi,bado niko duniani,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
11
Mimi sio mshairi,leo nataka mjue,
Napelekwa ka tairi,natamani nijiue,
Kufanya yaso hiyari,yataka moyo mjue,
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.
12
Swali ulio uliza,nahisi nimelijibu,
Kama sijatosheleza,sema usione tabu,
Dunia yaeleleza, kucheka usithubutu.
Natunga yalo nisibu,mengine nabahatisha.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5)
mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania.