SIASA MJUE NJIA, MAAMUZI KUFIKIA.












SIASA MJUE NJIA, MAAMUZI KUFIKIA.
1
Nimezama mwituni, kumtafuta mnyama,
Mwenye nguvu duniani, leo na kesho kiama,
Atajwa msikitini, kanisani wa msema,
Haliwi jambo mwituni, bila ya huyo mnyama.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
2
Naanzia shuleni, watoto wanaposoma,
Wanao soma vyuoni, na shahada za heshima,
Ngumbaru ipo kundini, unyago akina mama,
Elimu yetu nchini, huongozwa na mnyama.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
3
Uende sipitalini, na walipo wakulima,
Kwenye sekta ya madini, na kwa wapiga ngoma,
Utalii wa mbugani, uchezaji wa sinema,
Kote huko tambueni, mratibu ni mnyama.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
4
Siasa ndio mnyama, Lutumbo katuambia,
Siasa ni kitu chema, katika yetu dunia,
Siasa njia ya umma, maamuzi kufikia,
Siasa si kama sima, bali maji nawaambia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
5
Siasa kitu lazima, katu huwezi kimbia,
Waweza ikacha sima, maji huwezi susia,
Hata ngazi ya boma, siasa waitumia,
Siasa ukiitema, jua umeangamia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
6
Kuna siasa ya chama, kimoja nawaambia,
Kila shauri la umma, chama hujiamulia,
Bunge huwa maamuma, muhuri hushikilia,
Jambo lipite kwa Chama, bunge lalishadidia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
7
Zipo za demokrasia, vyama vingi nawambia,
Mfano za Tanzania, na uingereza pia,
Vyama hushindania, magogoni kuingia,
Rais kwa Tanzania, waziri kwa malikia
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
8
Siasa ndani ya vyama, huko hazikuanzia,
Ilianza toka zama, kabla ya hino dunia,
Furkani nimeisoma, sikuiacha biblia,
Malaika na Karima, pia wanaitumia,
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
9
Siasa za huko ahera, kiongozi ni Jalia,
Huongoza msafara, waja wakafuatia,
Mwenye kufanya harara, jeuri akajitia,
Atakuwa ni asira, wa shetani nawambia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
10
Muumba ndio kinara, wa mbinguni na dunia,
Maisha huyachora, na njia hutupangia,
Hupata njema ijara, mwenye kumsujudia,
Hupata kubwa hasara, mwenye kupuuzia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
11
Nani alipiga kura? Munguwe kumchagua,
Mjibu pasi kufura, kweli mpate ijua,
Hapana si masihara, si punde mtagundua,
Tena sifanye papara, siasa kuchambua.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
12
Siasa za kifalme, mfano za Saudia,
Mwana hasa wa kiume, kiti ndio hukalia,
Koo iloshika kome, dola huishikilia,
Mfalme ndio sime, na pia huwa pazia.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
13
Zipo za kidikteta, kama zile za Mobutu,
Wengine panga hufuta, pia wapo wa mtutu,
Umma wote hufyata, mbele ya miungu watu,
Kila mwenye kutukuta, ni mbwa mbele ya chatu.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
14
Dikteta awe katili, mbona mtaumwa sana,
Siombe awe jahili, mtapoteza amana,
Tena akiwa bahili, wananchi hukondeana,
Kiongozi bahaluli, asiaminiwe tena.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
15
Samaki awape nyoka, mkate awape mawe,
Nani kashindwa ondoka, kisa halina mauwe?
Ya msingi wanataka, viongozi waelewe,
Wakichoka kuboboka, watawapopoa mawe.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
16
Dikteta awe rahimu, ndipo mtanufaika,
Rasini awe timamu, na tena mshaurika,
Mtakula keki tamu, mafurushi mtashika,
Tripoli yajilaumu, Gaddafi kudondoka.
Siasa mjue njia, maamuzi kufikia.
17
Nikitazama chupani, sioni kitu jamani,
Wino wangu wa thamani, ya manjano zafarani,
Niko mengi rasini, wino umetufitini,
Mwenye nao sinihini, naomba niuzieni
Mmeshindwa nidhamini, kwa kifupi kwaherini.

Dotto Chamchua Rangimoto (Njano5)
mzalendo.njano5@gmail.com
0715845394/0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania.