KUNA MANENO YENYE MENO.

KUNA MANENO YENYE MENO.
1.
Neno limekuwa neno, kiziwi kalisikia,
Neno liwe la mfano, tupate kujifunzia,
Neno lisiwe ndoano, kooni likanasia,
Kuna neno na maneno, kuna neno lenye meno,
2.
Lipo neno la uchungu, kiasi bubu aseme,
Mja apigwe kirungu, achapwe hata umeme,
Tayatoa kwa uvungu, na machungu ayateme,
Kuna neno na maneno, kuna neno lenye meno.
3.
Lipo neno la furaha, hata yatima acheke,
Neno jema ni tufaha, kiasi na lipendeke,
Kinyume chake karaha, wanangwa na mpulike,
Kuna neno na meneno, kuna neno lenye meno.
4.
Kuna neno la asili, kwa hilo tumeumbiwa,
Hilo neno ni Jalali, akisema kuwa huwa,
Neno hili ndio kweli, werevu wanatambuwa,
Kuna neno na maneno, kuna neno lenye meno.
5.
Kuna maneno makali, kuliko hata jambia,
Yanawaua makuli, watumwa na malikia,
Hayachagui jahili, na rahimu humshukia,
Kuna neno na maneno, kuna neno lenye meno.
6.
Kuna maneno matamu, asali iwe pembeni,
Tena hayaishi hamu, tayapenda ulimini,
Kuyakosa talaumu, ukose raha moyoni,
Kuna neno na maneno, kuna neno lenye meno.
7.
Kuna maneno hutibu, magonjwa yaso dawa,
Yanasemwa taratibu, maradhi yapate powa,
Humtuliza mahabubu, maneno akiambiwa,
Kuna neno na maneno, kuna neno lenye meno.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
mzalendo.njano@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania.