TAMKO LA MUFTI JUU YA TUKIO LA KIGAIDI UFARANS













Matukio ya Ufaransa,
Mufti (BAKWATA) atoa tamko.

Assalaam alaykum warahmatullahi wabarakaatuh
Kwa niaba ya waislamu wa Tanzania, napenda kutoa rambi rambi na pole kwa watu wa Ufaransa ambao ndani yake wapo waislamu na wasio waislamu, wenye dini na wasio na dini.

Napenda kutoa pole sana kwao kwa tukio la kihalifu na kigaidi lililotokea huko hivi karibuni na kuwaathiri wakazi wa huko Ufaransa na kiukweli kabisa tukio hili pia limetuathiri sote ulimwenguni.
Hapa napenda kusema kwamba tukio lolote la kihalifu dhidi ya raia wasio na hatia popote pale ulimwenguni ni tukio la kihalifu dhidi ya wasio na hatia ulimwenguni kote.
Ulinzi na usalama na zawadi iliyo kubwa mno kutoka kwa Mwenye ezi Mungu kwa wanadamu popote pale walipo. Kwani kwa kuwepo ulinzi na usalama ndio tunaweza kuendesha sughuli zetu za ibada,uchumi na maendeleo mbalimbali katika nchi zetu.

Hivyo basi yeyote yule anaejaribu kuchezea Ulinzi na Usalama wetu huyo anafanya kitendo cha kumfurahisha Shetani na kamwe hafanyi kitendo cha kumfurahisha Mwenye ezi Mungu.
Natambua katika kipindi hiki wapo watakaojaribu kuhalalisha kitendo hiki kwa visingizio mbalimbali ambavyo kwa hakika hakuna njia yeyote ya kuhalalisha vitendo vya namna hii kwani hakuna mafundisho yeyote ya dini yanayohalalisha kuuwawa watu wasio na hatia.
Wajibu wetu katika kipindi hiki ni sote kwa pamoja na kuungana na wenzetu waliopoteza ndugu na jamaa katika tukio lile la kihalifu.

Kama ambavyo tunatoa pole kwa waathirika wa tukio hili huko ufaransa vilevile tunatoa pole kwa waathirika wa matukio ya namna hii popote pale ulimwenguni.
Kwani natambua wapo wanadamu ambao wamo ndani ya mateso na shida mbalimbali katika sehemu mbalimbali ulimwenguni. Sehemu kama vile Syria, Yemen, Afrika ya kati, Myanmar, Palestine, Libya, Mali, Somalia nk.
Na mwisho niwakumbushe waislamu wa Tanzania na watanzania wenzangu kwa ujumla umuhimu wa kuilinda Amani ya nchi yetu na kuendelea kushikamana katika kuilinda kwa nguvu zetu zote Amani hii.
Wabillahi ttawfiiq.
MUFTI WA Tanzania
Sheikh Abu Bakari Zubeir