IWEJE KIMBUNGA KILE, KISHINDWE ZUA PAA.

IWEJE KIMBUNGA KILE,
KISHINDWE ZUA PAA.                                                            

1.
Msije dhani natunga, wala sisemi uwongo,
Nimekiona kimbunga, kimetikisa mjengo,
Samani zilijigonga, haukupona mlango,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
2.

Hewa ikawa mchanga, vumbi ndani ya jengo,
Watu wakatangatanga, kama wanasaka fungo,
Si pakazuka kisanga, fupa kapewa mapengo,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
3.

Uhodari wa kuchunga, na kupeta kwa ungo,
Sima imejaa chenga, umethibiti urongo,
Mtoto kapewa mwanga, shetwani ataka pungo,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
4.

Miti ilipoanguka, mwenyewe nikanong’ona
Paa lililotoboka, hivi leo litapona?
Bora lipate dondoka, kwani halifai tena,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
5.

Mwenzenu niliboboka, dua mbaya nikaomba,
Paa lipate dondoka, tuezeke upya nyumba,
Mzigo hautafika, kamba hizi za mgomba,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
6.

Pepo zimezoa nguo, hadi za maungoni,
Juba na mitandio, haikubaki mwilini,
Watu wakaanza mbio, za kujistiri jamani,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
7.

Ni sharia kuchutama, zinapokuvuka nguo,
Juha aweza inama, aende kim-binuo,
Tangu zama ni hekima, kuyastiri maeneo,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
8.

Chui wamekuwa ndama, kenge amekuwa swila,
Mla wali kala sima, aliyemacho kalala,
Shilingi haikuzama, meli ikawa chakula,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
9.

Nyoka kapata miguu, jongoo kapata macho,
Wajaenda lango kuu, moyoni hawana kicho,
Watateta na mkuu, tena pasina kificho,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
10.

Lile sikio la kufa, si limepata mganga,
Moto umeshika sofa, hando liko na mchanga,
Hino yangu falsafa, kwa hoja nimeijenga,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania