SIONE UKADHANI.

SIONE UKADHANI.
1.
Sione nimenyamaza, mwenzio sina furaha,
Mambo ulo yatangaza, mie yanipa karaha,
Allah aniongoza, ulidhani nitahaha,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.
2.
Sione nimetulia, moyoni nahangaika,
Mwenzio nafikiria, namna ya kuongoka,
Ubaya wanifanyia, inshallah tastirika,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.
3.
Sione natabasamu, moyoni naungulika,
Nikiwaza sina hamu, mambo yalivyo pinduka,
Mie nimepigwa bomu, najuta kumchunuka,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.
4.
Sione nimeduwaa, ujue ninayajenga,
Hata niipate taa, lipendeze langu anga,
Wajashikwa na butwaa, zipotee zako ngenga,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.
5.
Sione sijakujibu, sidhani sijalipata,
Umetumwa si ajabu, fikisha umenikuta,
Sema halinipi tabu, si joto likafukuta,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.
6.
Sione abwata juu, yupo alo mpandisha,
Hata kwa yake miguu, na ngazi ya kuegesha,
Mgude sio chuguu, kobe hawezi pandisha,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi. 


Dotto Rangimoto Chamchua.(Njano5)
255762845394/255784845394
mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania