KISOGO MCHAWI?

KISOGO MCHAWI?

1.
Natoa kingilambago, nisikizwe kilingeni,
Simtaki jini kago, maalim Subiani,
Namtaka Mwinyimbago, kibokoye Makatani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
2.
Fundi kalia kibago, ufushe wako ubani,
Mpandishe Mwinyimbago, anipashe ya sirini,
Kichogo chake kigogo, aague kina nini,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
3.
Vile mchawi kichogo, imethibiti nadhani,
Kichogo huzua zogo, kwa jirani na nyumbani,
Lakini si cha mdogo, naomba zingatieni,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
4.
Akijitoa mdogo, hubaki poa kundini,
Tena hapeleki zogo, aendapo tambueni,
Kambare akina ngogo, hawastuki asilani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
5.
Tena hafanyi mikogo, hauziki gazetini,
Aishi pale Kigogo, soko lake Buguruni,
Hawamjui wa dago, hata walio shambani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
6.
Sasa katoka kigogo, ikazuka tafarani,
Wakubwa hata wadogo, wakafuata njiani,
Katangazwa si kidogo, luninga na redioni,
Vipe iwe tafarani, alipowapa kisogo.
7.
Kaondoka na mizigo, iliyo mwake kwapani,
Naeza kuita kago, isiyobebwa kichwani,
Kago limeleta zogo, alipolitua ndani,
Vipe iwe tafarani, alipowapa kisogo.
8.
Baadhi wakawa mbogo, hawamtaki mgeni,
Hasa mpenda mihogo, asiyetaka utani,
Akakusanya virago, akajitoa kundini,
Vipe iwe tafarani, alipowapa kisogo.
9.
Kigogo huyo kigogo, anatamba baharini,
Meli zimepata pigo, vihori viko shakani,
Hatari anayo chwago, nyangumi pia jodani,
Vipe iwe tafarani, alipowapa kisogo.
10.
Panda ewe Mwinyimbago, ili nipate yakini,
Ukiague kichogo, nikijue kina nini,
Kiasi kizue zogo, watu wakose amani,
Vipe iwe tafarani, alipowapa kisogo.
11.
Mkirika na mtogo, vimechomwa na ubani,
Kafurahi Mwinyimbago, ameshapanda rasini,
Ninawaacha kidogo, nisikilize madini,
Vipe iwe tafarani, alipowapa kisogo.


Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5)
784845394/715845394
Mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania