RIZIKI NI MAJALIWA.

RIZIKI NI MAJALIWA                                                                  
1Haku muumba kilema, akamkosesha mwendo,
Huyo ni Mola Karima, mfalme wa vishindo,
Usijifanye yatima, fungua yako mafundo,
Rauka fanya hima, nyumbani haliji windo.
Riziki nimajaliwa, kuipata si ngekewa.
2.
Mwenye kupewa ukwasi, katu hakupendelewa,
Masikini hasi asi, wallahi hakuonewa,
Mitihani ya Qudusi, mola wa majaliwa,
Alichopewa pungusi, chaa hakuruzukiwa.
Riziki nimajaliwa, kuipata si ngekewa.
3.
Rauka wahi kazini, upate yako ijara,
Changamoto za windoni, na zikufanye imara,
Toa simanzi moyoni, tena sifanye harara,
Bosi avimbe kichwani, tuli sipoteze dira.
Riziki nimajaliwa, kuipata si ngekewa.
4.
Ukiri mwenzangu kiri, hebu acha kusonona,
Wazoee waajiri, kama wataka kunona,
Shetwani asikughuri, ingawa dhiki waona,
Subiri ndugu subiri, lisilo mwisho hakuna.
Riziki nimajaliwa, kuipata si ngekewa.
5.
Niseme na waajiri, wenye pembe vichwani,
Wana kifanya kiburi, hawana heri moyoni,
Mbaya hawana habari, shida haina maskani,
Tabu haina tajiri, wala si ya masikini.
Riziki nimajaliwa, kuipata si ngekewa.
6.
Ewe ndugu mwajiriwa, sema na wako moyo,
Jukumu ulilopewa, litimize pasi choyo,
Ridhika na unachopewa, huno wangu mgogoyo,
Rushwa katu si ngekewa, yataka ushinda moyo.
Riziki nimajaliwa, kuipata si ngekewa.
7.
Wote wategemeana, mwajiri na mwajiriwa,
Kubwa kuheshimiana, mwerevu kanielewa,
Pia mkiaminiana, kazi haitachezewa,
Tara mkifanyiana, lengo halitafikiwa,
Riziki ni majaliwa, kuipata si ngekewa.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania