AJIRA SERIKALINI SASA KWA MKATABA WA MUDA MAALUMU:


AJIRA SERIKALINI SASA KWA MKATABA WA MUDA MAALUMU:
Atakayefanya vizuri ataendelea na mkataba, atakayevurunda kufutwa kazi mara moja.
Taarifa kuhusu mpango wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano kuzifanyia mabadiliko makubwa sheria za Utumishi wa Umma kwa kuondoa kipengele cha Ajira ya Kudumu (Permanent Employment Contract) kimepokewa kwa hisia chanya na jamii.

Kwa miongo mingi utendaji katika sekta ya Utumishi wa Umma umekuwa ukilegalega, kuzorota na kutokuwa wa ufanisi kiasi sio tu mara kadhaa umepelekea kuingiza Serikali katika hasara ya mabilioni ya shilingi lakini pia imekuwa sababu ya kero kubwa kwa wananchi wanaokosa huduma na maamuzi stahiki katika ofisi za umma.

Sababu kuu inayotajwa kuchangia uzembe, utoro, uvivu, kutowajibika, ufujaji wa fedha za umma, manyanyaso kwa wananchi, ulevi, wizi, rushwa, ufisadi, undugunization n.k ni kwa kuwa baadhi ya watendaji hawa wa umma mikataba yao ya ajira ilikuwa ni ya kudumu na yenye pensheni (Permanent and Pensionable).

Kigezo hiki cha permanent and pensionable kimekuwa kikitumiwa vibaya sana na baadhi ya watendaji kwenye ofisi za umma kufanya kazi vile wanavyotaka wao. Hata inapobainika mfanyakazi ni mzembe kabisa kabisa ambaye hawezi kutimiza majukumu yake kumfukuza kazi linabaki kuwa jambo gumu sana ambalo hata Waziri hawezi na wengi huishia kuhamishwa vituo vyao vya kazi na kuendelea na matendo yao yasiyo na ufanisi katika utumishi.

Bunge kama chombo cha kutunga sheria kinapaswa bila woga kutimiza majukumu yake ikiwemo kurekebisha kwa kufuta vipengele vyote vya sheria ya Utumishi wa Umma ambavyo vimekuwa kichaka kwa baadhi ya watumishi kufanya mambo ya hovyo wakiamini hawagusiki.
Bunge likifanikiwa kuziboresha sheria hizi za Utumishi wa Umma tunaamini zitasaidia kurejesha Nidhamu Kazini, kuongeza ari ya Uwajibikaji, kuondoa migongano, migogoro, kupunguza hasara kwa Serikali zisizo za lazima, kutoa mwanya kwa watendaji wenye sifa kidhi kuajiriwa katika sekta ya umma na kusukumu mbele gurudumu la Maendeleo.

Miaka ya 1980's kulikuwa na kibao mashuhuri chenye maneno;
"Nidhamu ya Kazi ni msingi wa mafanikio mema kazini, viongozi na wafanyakazi, lazima wote muwe na nidhamu.
Migogoro na migongano makazini ni ukosefu wa nidhamu".
Katika kuifumua na kuisuka upya nchi yetu, tunaunga mkono juhudi zote njema zenye kulenga kuwa na Taifa lenye kuzingatia misingi ya Uzalendo, Uwazi, Uwajibikaji, Uadilifu, Umoja, Udugu, Utu na Utawala wa Sheria.
Viva Tanzania! Viva!