YU WAPI ASKARI MBEBA GHARAMA ZAKE?

YU WAPI ASKARI MBEBA GHARAMA ZAKE?           
 1
Anunue makombati, kwa pesaze mfukoni,
Vifaru na guruneti, vitoke mwake kwapani,
Yaani hata mabuti, na silaha za vitani,
Mnitajie askari, mbeba gharama zake.
2
Pesa zake za manati, anunue darubini,
Familia si thabiti, pesa ziende vitani,
Nimeshikwa kibuhuti, dunia iko rasini,
Mnitajie askari, mbeba gharama zake.
3
Watoto hawana njuti, wako peku miguuni,
Hawana hata mashati, wala ada ya shuleni,
Tena pana hatihati, kukosa pango jueni,
Mnitajie askari, mbeba gharama zake.
4
Hazipikwi kalimati, wala hando si utani,
Wana chai hawapati, paka kalala jikoni,
Hawachezi na ukuti, chango zalia tumboni,
Mnitajie askari, mbeba gharama zake.
5
Sinunue utondoti, na vivalo vya mwandani,
Kitanda kikose shiti, baba uende vitani,
Si bure uko na shoti, hazijatimu kichwani,
Mnitajie askari, mbeba gharama zake.
6
Waume na mabanati, walimtoa mkoloni,
Walishikana mashati, kubeba walo vitani,
Nyerere kapewa hati, akaruka Marekani,
Mnitajie askari, mbeba gharama zake.
7
Kuna kufuja wakati, kubeba vita begani,
Nadhani hawanipati, subuhi sio jioni,
Sijakunywa spiriti, sina ulevi kichwani,
Nimeijaza sleti, siko na wino chupani.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
mzalendo.njano5@gmail.com
0762845394/0784845394
Morogoro Tanzania.