MUNGU NI PUNGUANI?






MUNGU NI PUNGUANI?
1.
Nimezama fikirani,
Kumsaka Punguani,
Aliyezua tafrani,
Mbinguni na duniani,
Nimemjua jamani,
Huyo Bwana Punguani.
2.
Huyo Bwana Punguani,
Kaacha mkewe ndani,
Kajikunyata chumbani,
Mito yake ubavuni,
Yuko mpweke jamani,
Yeye kaenda kuzini.
3.
Yeye kaenda kuzini,
Mumewe yuko kazini,
Watoto wako shuleni,
Uchafu upo chumbani,
Paka kalala jikoni,
Huyu pia punguani,
4.
Huyu pia punguani,
Mshinda mtandaoni,
Mtu mvivu kazini,
Mwenye kibli moyoni,
Kapanga watu foleni,
Dharau iso kifani.
5.
Dharau iso kifani,
Kwa walimu mashuleni,
Kushinda maofisini,
Na visimu mikononi,
Hawaogopi jamani,
Hawaendi darasani.
6.
Hawaendi darasani,
Wanatoroka shuleni,
Wanashinda vijiweni,
Na msuba mkononi,
Hawafuzu mitihani,
Hawa ni mapunguani.
7.
Hawa ni mapunguani,
Wasoenda shambani,
Hivi waja vuna nini?
Mikono yao laini,
Macho yao utosini,
Vya wenzao watamani.
8.
Vya wenzao watamani,
Wawapore mkononi,
Hawana utu asilani,
Wamekuwa mahayawani,
Watoa roho mwilini,
Kama simba wa nyikani.
9.
Kama simba wanyikani,
Wanasiasa nchini,
Kondoo wa zizini,
Mwenye ngozi laini,
Wameivaa mwilini,
Wamekuwa mafanani,
10.
Wamekuwa mafanani,
Wapate kula maini,
Ni warongo si utani,
Wakiingia bungeni,
Wanaiponda ilani,
Hawa ni mapunguani.
11. 
Hawani mapunguani,
Imethibiti jamani,
Vikongwe wako shakani,
Tena wako hatarini,
Kwa hila zao jamani,
Roho zao zi shakani,
12.
Roho zao zi shakani,
Hawana tena amani,
Wenye wekundu machoni,
Kwa moshi wa jikoni,
Eti waruka angani,
Wachawi wa kilingeni,
13.
Wachawi wa kilingeni,
Wanga wapaa angani,
Watabana mafundoni,
Watia nuksi mwilini,
Hivi wana cheo gani?
Kama si mapunguani?
14.
Kama si mapunguani?
Basi ni mahayawani,
Uchawi ni kitu gani,
Mwenyewe hasa n’ nani?
Wa kuzuka uzeeni,
Asotoka ujanani?
15.
Asotoka ujanani,
Namtafuta jamani,
Alofika baharini,
Bila kupita mtoni,
Wachawi wa utotoni,
Mbonahawaonekani?
16.
Mbona hawaonekani?
Wachawi wa utotoni,
Tieni ndimi puani,
Utimu uhayawani,
Waso zama fikirani,
Mahala pao bomani,
17.
Mahala pao bomani,
Mavuno yao jaani,
Waende mbio porini,
Na wagagae upwani,
Ni jaza ya punguani,
Wali mkavu chanoni,
18.
Wali mkavu chanoni,
Wa kunata kiganjani,
Ni jaza ya punguani,
Alo muasi Manani,
Mchora nyota baoni,
Naye pia punguani?
19.
Naye pia punguani,
Mchora nyota baoni,
Mjenzi wa kisirani,
Mweledi wa ufatani,
Watu hawaelewani,
Kisa huyu maluuni.
20.
Kisa huyu maluuni,
Mjaza chuki moyoni,
Mke kalala chumbani,
Mume wake varandani,
Ndoa ziko hatarini,
Hawaishi kwa amani.
21.
Hawaishi kwa amani,
Wenye kufanya udini,
Ukabila ni tufani,
Kimbunga kiso kifani,
Hatujafika fukweni,
Utalazi wafaani?
22.
Utalazi wafaani,
Nawaomba zindukeni,
Yako mawili jueni,
Ni matatu tambueni,
Myashike akilini,
Myapambe ukutani.
23.
Myapambe ukutani,
Yalo tutia kashani,
Mosi damu ya mwilini,
Asiliye viunoni,
Inapitia tumboni,
Kisha yaja duniani.
24.
Kisha yaja duniani,
Na ng’aa ng’aa chumbani,
Sishangae aliani,
Ndio uzima eleweni,
Naomba nitajieni,
Asozaliwa jamani.
25.
Asozaliwa jamani,
Hayupo duniani,
Jambo la pili shikeni,
Ni kuzaliwa jueni,
Mama huwa taabani,
Baba yuko furahani.
26.
Baba yuko furahani,
Kapata mwana jamani,
Mtoto kitu thamani,
Ila si kwa punguani,
Ata mkana hadharani,
Alelewe umamani.
27.
Alelewe umamani,
Kwa simanzi na huzuni,
Baba aranda njiani,
Wajomba na usukani,
Huno ni upunguani,
Mahalapake jaani.
28.
Mahala pake jaani,
Zile chuki za kidini,
Popote ulimwenguni,
Naomba tafuteni,
Alafu nitajieni,
Aso na damu mwilini.
29.
Aso na damu mwilini.
Mtajeni wenzanguni,
Watu toka Marekani,
Na hata wa Arabuni,
Walo juu aridhini,
Wana damu mishipani.
30.
Wana damu mishipani,
Yenda mbio tambueni,
Hino damu ya thamani,
Imetuunga jamani,
Waja waso ithamini,
Wana matobo kichwani.
31.
Wana matobo kichwani,
Wataka kwenda vitani,
Hupenda zua tafrani,
Waivuruge amani,
Tuwashinde wenzanguni,
Popote ulimwenguni.
32.
Popote ulimwenguni,
Mwenye kwenda kanisani,
Biblia yake kwapani,
Na rozali mkononi,
Ana kitu cha thamani,
Damu yake ya mwilini.
33.
Damu yake ya mwilini,
Yule wa msikitini,
Ina tafauti gani?
Na ya mwenda kanisani?
Hata asiye na dini ,
Yuko na damu mwilini.
34.
Yuko na damu mwilini,
Mhindu na mpagani,
Watu walio na dini,
Na wale waso na dini.
Imewatia kashani,
Hinodamu ya thamani.
35.
Hino damu ya thamani,
Tunu toka kwa Manani,
Mwiko kuimwaga chini,
Kwa sababu za kihuni,
Mja sifanye utani,
Roho kutoka mwilini,
36.
Roho kutoka mwilini,
Muosha awe kazini,
Asikose mkafini,
Aswaliwe kanisani,
Mwili ubebwe tusini,
Ukazikwe kaburini,
37.
Ukazikwe kaburini,
Urejee mavumbini,
Uwe na hila tisini,
Kifo hakiwezekani,
Kifo la tatu jamani,
Yale mambo kumbukeni.
38.
Yale mambo kumbukeni,
Yano tutia kashani,
Hata uwe kama nani,
Huto dumu maishani,
Matano yalo kashani,
Kifo la tatu jamani.
39.
Kifo la tatu jamani,
La nne lipo njiani,
Tunu toka kwa Manani
Utanzania jamani,
Utaifa ni thamani,
Umeuzidi marijani.
40.
Umeuzidi marijani,
Na vito vya Merelani,
Semeni wa visiwani,
Twawatazama usoni,
Na mseme kwa yakini
Kipi chenye thamani?
41.
Kipi chenye thamani?
Kati ya hivi jamani,
Zanzibar ya Sultani,
Na Tanzania Amani,
Msiwe mapunguani,
Tanzania ni thamani.
42.
Tanzania ni thamani,
Thamani kubwa jamani,
Tanganyika itupeni,
Ni zao la mkoloni,
Waliishinda Berlini,
Kambarage na Amani.
43.
Kambarage na Amani,
Waliishinda Berlini,
Wakaipata thamani,
Ilo kubwa duniani,
Tuitunze kwa makini,
Tusiufanye utani.
44.
Tusiufanye utani,
Kutunza hino thamani,
Utanzania jamani,
Ni la nne tambueni,
Mkumbuke ya thamani,
Yanotutia kashani,
45.
Yano tutia kashani,
Yale matano jamani,
Rangi isitufitini,
Ukanda tuutupeni,
Ukabila na udini,
Mahala pake chooni.
46.
Mahala pake chooni,
Yanotutenga jamani,
Na tuyabebe tusini,
Tuyazike kaburini,
Si mwajua visirani,
Vita wanaitamani?
47.
Vita wanaitamani,
Hawa mapunguani,
Wallahi siwatukani,
Sindano tuwadungeni,
Hawajatimu kichwani,
Mkamilifu ni nani?
48.
Mkamilifu ni nani,
Aloumbwa na Manani,
Aishiye Duniani,
Asiye na walakini,
Upungufu mwilini,
Ni la tano tambueni.
49.
Ni la tano tambueni,
La kututia kashani,
Endapo tukiamini,
Sote tuna walakini,
Tutakumbuka hisani,
Tupuuze visirani.
50.
Tupuuze visirani,
Wasokinai moyoni,
Wanamshinda shetani,
Kwa silaha za ghalani,
Hivi kuwe na amani
Watamuuzia nani?
51.
Watamuuzia nani?
Silaha zao ghalani,
Dunia yetu jamani,
Yatikisika jueni,
Viumbe vya duniani,
Hakika vi hatarini.
52.
Hakika vi hatarini,
Viumbe vya baharini,
Maji taka ya mjini,
Na yale ya viwandani,
Huingizwa baharini,
Huu si upunguani?
53.
Huu si upunguani?
Kuua faru jamani,
Magogo ya msituni,
Na ndovu wa hifadhini,
Rasilimali hatarini,
Kupotezwa hifadhini.
54.
Kupotezwa hifadhini,
Na hawa mapunguani,
Kikulacho maungoni,
Cha ishi mwako nguoni,
Tunalala nao ndani,
Hawa mapunguani.
55.
Hawa mapunguani,
Tuna lala nao ndani,
Shime tuwafichueni,
Tulinde ndovu jamani,
Tuwatie kituteni,
Ahmadi kibindoni.
56.
Ahmadi kibindoni,
Silaha i mkononi,
Mdharau majirani,
Naye pia punguani,
Ataanza fika nani,
Ashikwapo chumbani?
57.
Ashikwapo chumbani?
Aanguke upenuni,
Awe na maiti ndani,
Au awe na tafrani,
Wa kwanza kufika nani?
Kama si wake jirani?
58.
Kama si wake jirani,
Silaha ya kibindoni,
Awe na ndugu Manyoni?
Naye yu Mkanyageni?
Watotongwa fikirini,
Tusidharau jirani.
59.
Tusidhara ujirani,
Ninawaasa jamani,
Tumuepuke fatani,
Aso ipenda amani,
Mdharau hasa nani?
Kama si punguani?
60.
Kama si punguani,
Niimpe cheo gani?
Mwenye ulevi kichwani,
Na miraa mkononi,
Ameshika usukani,
Abiria hatarini
61.
Abiria hatarini,
Roho zao zi shakani
Alama barabarani,
Hazioni si utani,
Dereva ni majinuni
Ana wazimu rasini.
62.
Ana wazimu rasini,
Mtumishi ofisini,
Hivi haki bei gani?
Anainadi sirini,
Hana haki masikini,
Penye rushwa si utani
63.
Penye rushwa si utani,
Hakuna haki asilani,
Tia kura sandukuni,
Mtu aende bungeni,
Kura itapigwa chini,
Mkwasi hawezekani.
64.
Mkwasi hawezekani,
Hata hospitalini,
Penye rushwa tambueni,
Katu hapangi foleni,
Mkwasi hawezekani
Hata pale bandarini,
65.
Hata pale bandarini,
Mkwasi hana foleni,
Hili la rushwa jamani,
Ni sifa ya punguani,
Tuipinge hadharani,
Nawaasa jamani.
66.
Nawaasa jamani,
Vijana wa vijijini,
Msiwe mapunguani,
Mkaamia mjini,
Mali nyingi za thamani,
Mtazipata shambani.
67.
Mtazipata shambani,
Mlizoota ndotoni,
Kubwa muwe na imani,
Na subira mtimani,
Kazi adimu mjini,
Wasomi wako jiweni.
68.
Wasomi wako jiweni,
Na vyeti toka chuoni,
Kazi adimu jamani
Hutangatanga njiani,
Huu si upunguani?
Kwa wa’lo madarakani?
69.
Kwa wa’lo madarakani,
Watunga sera nchini,
Wakuu serikalini,
Na viongozi bungeni,
Wanafanya kazi gani?
Vijana wako shakani.
70.
Vijana wako shakani,
Wenye kupenda kuzini,
Tena hawako makini,
Ni wazembe uwanjani,
Wana kiatu mguuni,
Hawana kinga kinywani.
71.
Hawana kinga kinywani,
Tena wana jiamini,
Wazee wamo kundini,
Wenye ashiki jununi,
Hawa pia wana nini?
Kama si upunguani?
72.
Kama si upunguani,
Sasa wana kitu gani,
UKIMWI upo jamani,
Nawambia si utani,
Ninyi mpo hatarini,
Vijana muwe makini.
73.
Vijana muwe makini,
Mliokuwa vyuoni,
Wale wa makazini,
Na mlio mashambani,
Joka litawashikeni,
Msipokuwa makini.
74.
Msipo kuwa makini,
Uchumi u hatarini,
Hujiwezi kitandani,
Kazini aende nani?
Kijana aso makini,
Naye pia punguani.
75.
Naye pia punguani,
Mzazi aso imani,
Mtupa mwana jaani,
Tumuweke kundi gani?
Mama huyu maluuni,
Hafai msikitini.
76.
Hafai msikitini,
Kisalata maluuni,
Hatakiwi kanisani,
Mtu mwenye kisirani,
Watu hawaelewani,
Sababu upunguani.
77.
Sababu upunguani,
Mtu huweza kubini,
Mtu mwenye ukunguni,
Shibe kwake yafaani?
Hawa ni mapunguani,
Wenye matobo kichwani.
78.
Wenye matobo kichwani,
Wako wengi tambueni,
Wanasinzia bungeni,
Hawafiki majimboni,
Ngazi za ghorofani,
Wamezifanya katuni.
79.
Wamezifanya katuni,
Hazina tena thamani,
Wamezitupa jaani,
Wasubiri kampeni,
Hawa nao wana nini?
Si bure upunguani.
80.
Si bure upunguani,
Kutenda uso amini,
Mchana atangaza dini,
Usiku yu kilingeni,
Viongozi wa dini,
Wanatufundisha nini?
81.
Wanatufundisha nini?
Kumbikumbi toka chini,
Kutamani vya angani,
Kavaa mbawa mwilini,
Kuwa ndege katamani,
Mchwa tamaa za nini?
82.
Mchwa tamaa za nini?
Cha mno hasa nini?
Kikutoe chuguuni,
Uranderande angani,
Windo la nyoka nyikani,
Mchwa umepata nini?
83.
Mchwa umepata nini?
Kwa hizo mbawa mwilini,
Tamaa huwa kichwani,
Mauti ni ya mkiani,
Mchwa naye punguani,
Mwenye matobo rasini.
84.
Mwenye matobo rasini,
Ndiye bwana punguani,
Jambo haliwezekani,
Kwanini walitamani?
Waja juta maishani,
Ya mchwa kuyatamani.
85.
Ya mchwa kuyatamani,
Kupata vuno angani,
Bandika mbawa begani,
Ka ndege wa angani,
Gundi iishe mwilini,
Puu uanguke chini.
86.
Puuu anguke chini,
Sijue ufanye nini,
Njano nawausieni,
Masikio yategeni,
Uwezo uwe shinani,
Tamaa iwe tawini.
87.
Tamaa iwe tawini,
Uwezo uwe shinani,
Mtafuzu mitihani,
Tamaa ikiwa chini,
Jamani upunguani,
Hivikauumba nani?
88.
Hivi kauumba nani?
Huu upunguani,
Nacho kiumbe jamani,
Kilichopo duniani,
Nimezama vitabuni,
NimeisomaQurani.
89.
Nimeisoma Qurani
Biblia kwa makini,
Kila kitu duniani,
Kimeumbwa na Manani,
Hivi upunguani,
Ameuumbanani?
90.
Ameuumba nani?
Huno upunguani,
Huwezi umba tufani,
Na usiwe majinuni,
Muumba upunguani,
Tuumpecheo gani?
91.
Tuumpe cheo gani,
Muumba upunguani,
Nimezama methalini,
Kwa mfalme Sulemani,
Mungu kafanya shetani,
Kwa siku ya ushetani,
92.
Kwa siku ya ushetani,
Mungu kaumba shetani,
Kula upepo kinywani,
Ziwe timamu kichwani,
Kama kifo kinjiani,
Akilizatufaani?
93.
Akili zatufaani,
Kama moja la zamani,
Lamfika punguani,
Mwenye akili makini,
Na mwenye jeshi makini,
Kifohumpiga chini,
94.
Kifo humpiga chini,
Mganga hospitalini,
Aso kufa ni Manani,
Ukweli utambueni,
Kuwa kaumba Manani,
Huuupunguani.
95.
Huu upunguani,
Hakuwa nao shetani,
Akatiwa ujununi,
Ibilisi rasini,
Akazua tafrani,
Mbingunina duniani.
96.
Mbinguni na duniani,
Muumba ni Manani,
Kilichopo rasini,
Mwa Ibilisi jamani,
Amekiumba nani?
Tafautina Manani.
97.
Tafauti na Manani,
Sasa kauumba nani?
Mungu ni punguani?
Baba wa huo jamani?
Naomba jibu makini,
Hasakwa wanazuoni
98.
Hasa kwa wanazuoni,
Wenye ilimu za dini,
Malenga wa wazamani,
Na wa sasa sogeeni,
Tutoe tongo machoni,
Tumjue punguani.
99.
Tumjue punguani,
Mwenye matundu kichwani,
Pia kamuumba nani,
Huyo bwana punguani,
Mungu ana cheo gani?
Kamasi punguani?
100.
Wino wa zafarani,
Umeisha chupani,
Ya manjano zafarani,
Iliyokwisha si utani,
Sasa niko mwishoni,
Ninasema kwahereni.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
mzalendo.njano5@gmail.com
784845394/762845394
Morogoro Tanzania