WAAFRIKA TUNA MAMBO.

WAAFRIKA TUNA MAMBO.                                            
1.
Mwajua mimi sijambo, namshukuru manani,
Nimeamka kitambo, shafika kibaruani,
Ila kuna kubwa jambo, kuuliza natamani,
Hivi nyie hamjambo? Mliopo kisimani.
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
2.
Mambo yakiwa si mambo, siweke fundo moyoni,
Kubwa sicheke utumbo, kwa maini ya jirani,
Sitaki ule makombo, kwa hamu ya biriani,
Bure taitwa mtambo, mwenye wazimu rasini.
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
3.
Kuna mambo ya mkumbo, kuyafuata acheni,
Mambo mengine urimbo, mchunge siwanaseni,
Kijana kimbie ng'ambo, nchini abaki nani?
Mwisho apigwe taimbo, kwa bata za ghaibuni.
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
4.
Memkumbuka Setembo, babu yangu wa moyoni,
Aliniusia mambo, kuwaambia natamani,
Rijali haumwi tumbo, wala chango kinenani,
Hakika hafanyi tambo, bila vitendo jueni,
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
5.
Nawasema wa kiambo, hata wale wa mjini.
Mlioamkia tembo, mloiota ndotoni,
Hamkuogeshwa jimbo, wakati wa utotoni,
Sawa mfanye utumbo, subuhi mko hewani,
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
6.
Twasisitiza kimombo, kiswahili taabani,
Vizuri kuiga mambo, si kila kitu jamani,
Sawa kuacha kiyombo, kwa suti za Marekani,
Kukiabudu kimombo, ni wazimu jueni.
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
7.
Kanisani kuna mambo, pia na msikitini,
Tuna itukana gombo, nalia utamaduni,
Miungu kutoka ng'ambo, Ulaya na Arabuni,
Imetupiga kikumbo, jadi haina thamani,
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani,
8.
Tufani yapiga sambo, istizai yafaani,
Mjue twaenda kombo, naomba zindukeni,
Sote tumelewa tembo, kutoka ughaibuni,
Sasa ni wana wa kambo, baba wa kijerumani
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
9.
Nimesema kimafumbo, hilo kwanza lijueni,
Maneno haya si shombo, ukutani andikeni,
Msiyafiche kwa rambo, hadharani yawekeni,
Jeuri ataka fimbo, awekwe sawa jamani,
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.
10.
Nimeliza la mgambo, lengo mtoke shimoni,
Ninawaita kwa wimbo, wahafidhina njooni,
Mwanagenzi nina mambo, majagina nifunzeni,
Naomba nifunge gombo, nilosema yashikeni,
Waafrika tuna mambo, nawambia si utani.


Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania.