ARAFA, SASA NAJA KILUNGA

ARAFA, SASA NAJA KILUNGA                       1.
Mie napenda mkembe, na mbuku wa kubanika,
Sipendi sima ya sembe, hata kuku wa kupaka,
Kisha nipate maembe, yenyewe yalo dondoka,
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika.
2.
Nitaanzia kwa Kwembe, anaye ishi Kiroka,
Sizipendi zake pombe, sema nimemkumbuka,
Ngoja nifike atambe, nduguye si amefika?
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika.
3.
Sitamuacha Msimbe, ndugu yangu mpendeka
Nyumba yake aipambe, afurahi wake kaka,
Kibwaya kwenye miembe, kiuliza umefika,
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika
4.
Kinole yuko Mtimbe, itanipasa kushuka,
Nyimbo za mbeta aimbe, na ngadu aende shika,
Kisha usiku atambe, ngano za kusadikika,
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika.
5.
Tegetero yuko Pembe, kwa uganga asifika,
Anaujua usembe, yu fundi wa kuzindika,
Memletea msembe, hisani nimekumbuka
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika.
6.
Luhangazi niwaombe, mwaka huu sitafika,
Nakichelea kimbembe, cha mlima na vichaka,
Nawataka msigombe, ipo siku nitafika,
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika.
7.
Rubwe aishi Kagombe, kwa uhuni asifika,
Hawezi kushika jembe, na vitamu avitaka,
Sasa kizungu aimbe, utakufa kwa kucheka,
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika.
8.
Karibu nafika ambe, mtambue nimechoka,
Nataka nikute embe, na ndizi za kuvundika,
Na mihogo mkachimbe, arafa nilo andika,
Mwenzenu naja Kilunga, Nyachilo nataka fika.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania