MCHAFUA WATU, HUCHAFUKA.

MCHAFUA WATU, HUCHAFUKA.                                                            
Kojoa ukojoavyo, hautafika mbinguni,
Na ufanye ufanyavyo, tone la mwisho guuni,
Wende mbio utakavyo, baya hurudi nyumbani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

Boboka ubobokavyo, mkono wangu shavuni,
Sitaonekana ovyo, mithili ya majinuni,
Sitashuka upendavyo, labda nipande thamani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

Chafua uchafuavyo, pasi na haya usoni,
Tabaki vile nilivyo, sichafuki asilani,
Dunia ndivyo ilivyo, hayana budi jamani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

We fusa ufusavyo, sikimbii mwangu ndani,
Sitaacha hivyohivyo, nitauchoma ubani,
Harufu ndivyo ilivyo, takuganda maungoni,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

We dhani udhaniavyo, sina baya mtimani,
Waelewa ndivyo sivyo, ungauliza nadhani,
Ninakujua ulivyo, hunipi tabu fatani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

Dotto Chamchua Rangimoto (Njano5)
255762845394/255784845394
Mzalendo.njano5@gmail.com