MAPENZI SI MAFURUSI.
















 MAPENZI SI MAFURUSI.
1.
Katu hapandi farasi, yule mzoea punda,
Mpenda kwenda kasi, mwendo pole humshinda,
Amezoweshwa fenesi, doriani lamshinda,
Sitokalifisha nafsi, nafanya ninayopenda,
Mie nina wasiwasi, kwa mambo yanavyo kwenda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
2.
Nipe gongo ya kiasi, nipate ipiga funda,
Na miraa ya Ramisi, kwa ubani naifunda,
Initoe wasiwasi, hata kipoe kidonda,
Niupate na wepesi, wa kumshukia nyonda,

Natambua si rahisi, kutamka "nakupenda"
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
3.
Niko na pepo za kusi, ni mbali ninapo kwenda,
Nausaka mdungusi, ukame 'sikose tunda,
Wenye kupendwa wakwasi, kila kiwanja hudunda,

Niache kikaragosi, nilo nayo yanishinda,
Mkononi sina tasi, n’nani atanipenda?
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
4.
Waja wataka fususi, hawana kitu kupenda,
Ubishi kama chunusi, natafuta pa kupanda,
Aso tabia za fisi, wallahi nitampenda,
Mwenye kujali nafsi, mafurusi kuyaponda,
Mapenzi ya wasiwasi, yatesa kama kidonda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
5.
Moyo una wasiwasi, akili i'njia panda,
Huyu mja Ibilisi, ni jini msaka tenda,
Kila siku alhamisi, kwake siku huganda,
Kuna siku za mafurusi, na za mifuko kukonda,
Si kuna siku nyepesi, na za kukaza mkanda?
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
6.
Hili jua la utosi, kila mtu humtenda,
Hata mwenye ukwasi, pia laweza mponda,
Ya jini kuhama rasi, kitie anapo konda,
Mwayaiga pasi wasi, ya majini mwayatenda,
Kwa talasimu za ngisi, mioyo mnaiwinda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.
7.
Sina hofu sina wasi, tena nenda mwana kwenda,
Kisu changu kimepasi, hakiyumbi kimedinda,
Hupati tena nafasi, dagaa zangu kutanda,
Nimestushwa na unyasi, nyoka alinipa donda,
Nimestuka kirahisi, we endelea kutanda.
Ukipendwa kwa pesa, taachwa kwa kuzikosa.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5)
Mzalendo.njano5@gmail.com
784845394/764845394
Morogoro Tanzania.