KIRUSI CHA ZIKKA CHATINGA RASMI AFRIKA.


Serikali ya Guinea-Bissau imebuni kamati ya dharura ya afya baada ya kuripotiwa kesi tatu za kwanza za kirusi hatari cha Zika.

Taarifa ya Wizara ya Afrika ya nchi hiyo imesema kuwa, kesi za ugonjwa huo hatari zimeripotiwa katika eneo la Bijagos na kwamba serikali imebuni kamati maalumu inayoongozwa na Waziri Mkuu Baciro Dja ili kuzuia kusambaa kwa kirusi hicho, wakati huu ambapo nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika inajikusanya baada ya kukumbwa na ugonjwa wa Ebola.

Kirusi hatari cha Zika kiliripotiwa kuibuka barani Afrika kwa mara ya kwanza katika Visiwa vya Cape Verde magharibi mwa bara hilo mwezi uliopita. Mkrugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Afrika, Matshidisho Moeti alisema, kesi hiyo ya Cape Verde ni ushahidi kuwa kirusi cha Zika sasa kimesambaa hadi nje ya bara la Amerika na kuingia Afrika.

Kirusi cha Zika kuligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 1947 na hakikuhesabiwa kuwa hatari hadi kilipoibuka upya mwaka jana nchini Brazil na kusababisha wanawake walioambukizwa kuzaa watoto wenye ubongo mdogo.

RWANDA YAIPINGA MAREKANI KUIHUSISHA MAGENDO YA BINADAMU.


Serikali ya Rwanda imekadhibisha tuhuma za Marekani kuwa inahusika na magendo ya binaadamu.

Mathilde Mukantabana, balozi wa Rwanda nchini Marekani hapo jana aliitaja ripoti hiyo kuwa ya kisiasa ambayo iko kinyume na ukweli wa mambo katika jamii ya Wanyarwanda wenyewe. Bi, Mukantabana ameogeza kuwa, serikali ya Kigali ina uwezo kamili wa kuwalinda na kuwapa hifadhi wakimbizi hususan raia wa Burundi.

Balozi huyo amefafanua kuwa, kuwalinda raia wa Burundi mkabala na kufanya magendo ya binaadamu, ni suala linalopewa kipaumbele na serikali ya Rwanda. Katika ripoti yake ya mwaka 2015 iliyotolewa siku ya Alkhamisi, Juni 30 Marekani iliituhumu serikali ya Kigali kwamba inashiriki katika magendo ya binaadamu hususan raia wa Burundi.

Kadhalika ripoti hiyo iliashiria kwamba Rwanda imekuwa ikiwatumia watoto wadogo wa Kirundi kama askari. Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Rais Paul Kagame kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya ukandamizaji wa haki za binaadamu.

80 WAFA KWA MASHAMBULIZI YA MABOMU IRAQ.


Watu wasiopungua 80 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi pacha ya mabomu katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Hujuma ya kwanza imeripotiwa kufanyika alfajiri ya leo nje ya mgahawa mmoja katika wilaya ya Karada na muda mfupi baadaye shambulizi la pili likafuatia mashariki mwa Baghdad.

Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Baghdad awali ilisema watu zaidi ya 60 wameuawa na wengine 100 wamejeruhiwa. Kundi la kigaidi la IS limekiri kuhusika na mashambulizi hayo na kutoa takwimu tofauti na za serikali za wahanga wa hujuma hizo. IS wamesema watu 40 wameuawa katika mashambulizi hayo na wengine 80 wamejeruhiwa.

Mashambulizi hayo yamefanyika masaa machache baada ya Waziri Mkuu wa Iraq kuzionya pande zinazowaunga mkono IS. Haider al-Abadi aliyasema hayo jana Jumamosi katika kikao na waandishi wa habari mjini Baghdad, na kuongeza kuwa, wale walioanzisha kundi la kigaidi la IS au kuliunga mkono, hivi sasa wanateketea katika moto ambao waliuwasha wao wenyewe.

Hujuma hii inafanyika siku mbili baada ya watu 46 kuuawa na kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi dhidi ya msikiti mmoja katika kitongoji cha Abu Ghraib, viungani mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

ASSAD: MGOGORO SYRIA UTAISHA KWA MAZUNGUMZO SAMBAMBA NA KUPAMBANA NA UGAID.


Rais Bashar Assad wa Syria amesema kuwa, haiwezekani kupatikana njia ya ufumbuzi halisi wa mgogoro wa nchi hiyo bila ya kuwepo mapambano ya kweli dhidi ya ugaidi.

Rais Assad amesema kuwa, kuna ishara za kukomeshwa mgogoro wa Syria na kuongeza kuwa, utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo unafungamana na mazungumzo ya Wasyria kuhusu mchakato wa kisiasa lakini sambamba na hayo mapambano dhidi ya ugaidi yanapaswa kudumishwa.

Kuhusu mwendo wa kinyonga wa mchakato wa kutafuta suluhisho la mogoro wa Syria, Rais Bashar Assad amesema: Waungaji mkono wa magaidi wa Magharibi na nchi kama Saudi Arabia, Uturuki na Qatar hazitaki kusitisha misaada yao kwa makundi hayo ya kigaidi. Rais wa Syria amesema iwapo misaada hiyo itasitishwa na Wasyria wakashauriana kuhusu katiba, mustakbali wa nchi na mfumo wa utawala basi hapana shaka kutapatikana utatuzi wa mgogoro huo hivi karibuni.

Baada ya kupita miaka 5 sasa tangu nchi ya Syria itumbukizwe katika mgogoro wa ndani, na kudumishwa misaada ya pande zote ya nchi za Magharibi na vibaraka wao kwa wapinzani na makundi ya kigaidi kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Assad, sasa kumeanza kujitokeza ishara za kukomeshwa mgogoro huo.

Tangu mgogoro huo ulipoanza Marekani, Uturuki, Saudi Arabia na Qatar zilifanya kila liwezekanalo kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria na kuwasaidia wanachama wa makundi ya kigaidi kuingia nchini humo. Ushirikiano wa miaka 5 wa nchi hizo na makundi ya kigaidi haujaweza kutimiza sehemu ndogo ya malengo yaliyoainishwa kwa ajili ya mgogoro wa Syria na hadi sasa Rais Bashar Assad angali anaongoza nchi hiyo huku makundi ya kigaidi yakidhoofika siku baada ya siku.

Inaonekana kuwa moja kati ya matunda ya uwekezaji wa nchi kama Uturuki katika mgogoro wa Syria ni kuhatarisha usalama wa Uturuki yenyewe ambayo miji yake mingi imekuwa ikikukmbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya milipuko ya kigaidi. Shambulizi la hivi karibuni kabisa ni lile la Jumanne iliyopita lililolenga uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul na kuua watu karibu 50. Watu wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa.

Matokeo kinyume na matarajio ya mradi wa nchi za Magharibi na vibaraka wao katika mgogoro wa Syria yamezilazimisha nchi hizo kuanza kuamiliana na serikali ya nchi hiyo kama alivyosisitiza rais Assad kwamba nchi za Magharibi zinawatuma maafisa wao hususan maafisa wa masuala ya usalama huko Damascus ili kushirikiana na kufanya mazungumzo ya siri na Syria.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amewaambia waandishi habari katika mji wa Sochi nchini Russia kwamba nchi yake inataka kutatuliwa mgogoro wa Syria kwa njia za kisiasa. Mevlüt Çavuşoğlu amesema Uturuki ilikuwa na mitazamo tofauti kuhusu suala la kubakia madarakani Rais Bashar Assad huko Syria lakini sasa iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu mitazamo mingine.

Hata hivyo na kama alivyosisitiza Rais Bashar Assad wa Syria, matamshi matupu ya kutaka kuwepo utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria hayatoshi na hapana shaka kuwa, mapambano ya kweli dhidi ya makundi ya kigaidi nchini Syria ni miongoni mwa masharti muhimu ya utatuzi wa kisaisa wa mgogoro huo.

Mafanikio ya Syria katika vita dhidi ya ugaidi ikishirikiana na Iran na Russia, yameimarisha nafasi ya Rais Assad na hapana shaka kuwa, usalama na amani ya nchi jirani vitaimarishwa kwa kuyaangamiza kikamilifu makundi ya kigaidi nchini humo.