MAMA, TAMBIKO LIMESHAPITA.

MAMA, TAMBIKO LIMESHAPITA.
1.
Hapa azaliwa mama, na bibi alomzaa,
Si mnaiona milima, kuipanda si mzaa,
Hata waliponituma, kupanda nilikataa,
Mizimu sasa ilale, tambiko limeshapita.
2.
Nimekuja himahima, na moyo ukinipaa,
Metoka Dar salama, na viatu sijavaa,
Nikapanda na mlima, yaani kama kichaa,
Mizimu sasa ilale, tambiko limeshapita.
3.
Sikiza eeh mama, mwanao niko na baa,
Mambo yaenda mrama, niendapo hujikwaa,
Sipati pesa ya sima, kodi yanipa fazaa,
Mizimu sasa ilale, tambiko limeshapita.
4.
Nina pombe ya mtama, mbuzi yu ndani ya chaa,
Nina mkuki na ngoma, na kaniki nimevaa,
Tambiko liende vema, hata nipate shufaa,
Mizimu sasa ilale, tambiko limeshapita.
5.
Mkembe pokea mama, na mwidu niloandaa,
Togwa na gimbi mlima, ngadu sio chanjagaa,
Nyote malale salama, mnikinge na balaa,
Mizimu sasa ilale, tambiko limeshapita.
6.
Hapa sasa kaditama, narudi kwa mikandaa,
Naenda tarudi mama, kutembea sitakaa,
Malengo nipate sima, isokuwa na budaa,
Mizimu sasa ilale, tambiko limeshapita.


Dotto Chamchua Rangimoto. (Njano5)
0762845394/0784845394
mzalendo.njano5@gmail.com