NATAKA KURA! NATAKA KULA!

NATAKA KURA! NATAKA KULA!                               
1
Siku ya kupiga kura, naona imewadia
Zile kukuru kakara, ukingoni zafikia,
Zile siku za subira, ujue zajiishia,
Jumapili piga kura, mwenzangu nakuusia,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
2.
Kwa kila masika tano, siku hii iko moja,
Hutangulia pambano, la hoja pia vihoja,
Hufanyika mikutano, watu wasikize hoja,
Kisha makubaliano, ya umma wote pamoja,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
3.
Hiyo siku ni adhimu, bilashaka mnajua,
Ni siku yetu muhimu, viongozi kuchagua,
Ina mambo maalumu, vizuri tukayajua,
Sheria yatulazimu, kuzifata mwatambua,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
4.
Taratibu kwa mstari, chumba utakifikia,
Muepuke kutafiri, hiyo siku nawambia,
Msianze kuhubiri, huko kuvunja sheria,
Tena silete habari, ya nani wampigia,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
5.
Ukiwa kwa kituturi, sicheze pata potea,
Uzikumbuke ghururi, na kweli za wagombea,
Ndipo ukate shauri, pa vema kujiwekea,
Kura yako iwe siri, piga majibu ngojea,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
6.
Sikiza msimamizi, sifanye upendeleo,
Tena sifanye ajizi, kutangaza matokeo,
Ulete maangamizi, sababu yenyewe cheo,
Tuvikumbuke vizazi, isitughururi leo
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
7.
Vema tufanye subira, hiyo siku ya uchaguzi,
Tena tusije wakera, wenzetu wasimamizi,
Ndugu sifanye harara, tusifanye uchochezi,
Polisi acha hasira, silete maangamizi,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
8.
Pamoja na wangu usi, pana jambo tujadili,
Tuumize zetu rasi, kwa yanayo tukabili,
Nimeshikwa wasiwasi, kwa jambo la jumapili,
Kutawepo ufanisi, katika zoezi hili?
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
9.
Imekuwa kawaida, watu kutopiga kura,
Hawaioni faida, wanachojua hasara,
Wallahi waona shida, kuzifunga biashara,
Mtu atafuta ada, wataka apige kura?
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
10.
Tatizo hasa ni nini? hata watu wasitoke?
Wanaona tabu gani? vituoni wasifike?
Ama polisi semeni, ndio kisa watishike?
Pamoja tujadilini, tongotongo zitutoke,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
11.
Niseme na wagombea, wenye kuomba kura,
Ninyi hupelekea, watu wasipige kura,
Yale wanotegemea, kuletwa na hizo kura,
Hakika yakitokea, watapenda piga kura.
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
12.
Naomba nichagueni, niwe wenu kiongozi,
Nina malengo jueni, ya kuwafuta machozi,
Hima hima kapigeni, ninyi ndio waamuzi,
Watu kwa kubwa imani, wana mpa uongozi,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
13.
Akipewa usukani, anageuka bazazi,
Jimboni haonekani, anahama na makazi,
Haya sitoi kichwani, nimewahoji wakazi,
Heri pepo za kusini, kuliko za kaskazi,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
14.
Anakifanya kiburi, akishakuwa kitini,
Hataki tena habari, za watu wake jimboni,
Kumbe zote ni ghururi, ahadi za kampeni,
Tena haoni hatari, kuikanyaga ilani,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
15.
Hivi kura yafaani? kama hawafaidiki,
Masoko hawayaoni, ya mahindi na hiriki,
Wawindaji wa porini, na wavuvi wa samaki,
Nawaomba tambueni, uchaguzi hawataki.
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
16.
Nyumbani hakuna sima, paka acheza jikoni,
Tumbo linatomatoma, taweza panga foleni?
Tena yataka simama, jua lapiga usoni,
Hawaendi wamegoma, nadhani jichagueni,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
17.
Kilio cha wakulima, ni hifadhi ya jamii,
Wavuvi pale Musoma, hawana hifadhi hii,
Hivyo hawapati bima, nisemacho sitanii,
Hakika wameshasoma, viongozi wasanii,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
18.
Uchaguzi ulopita, ni kama vile hasara,
Watu wengi walipata, kadi za mpigakura,
Nini kilichowapata, hata wasipige kura?
Kipo walichotafuta, ni nyenzo ya biashara,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
19.
Kikubwa kitambulisho, cha kuombea mkopo,
Tena na uthibitisho, wa mahala atokapo,
Hili ndio sababisho, la hicho chao kiapo,
Hata mfanye vitisho, hawata ligusa kopo.
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
20.
Kura moja ina nini? swali lataka jawabu,
Tena itabadili nini? hata ziniishe tabu,
Kura itafanya nini? apate kauli bubu,
Tena ina nguvu gani? hata fisadi atubu
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
21.
Maswali hayo makini, mwananchi tumjibu,
Kura moja ni thamani, ina nguvu ya ajabu,
Yaweza kupa Amani, au ikupe adhabu,
Ukose chakula ndani, la ununue kasabu,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
22.
Punguzeni hasira, wananchi nawaomba,
Tena sifanye harara, sikio sitie pamba,
Wala sifanye papara, mafisadi kuwatimba,
Kuzila kuna hasara, walewale watatamba,
Hawa wanataka kula, wengine wasaka kura.
23.
Wino wangu wa thamani, ni wa njano tambueni,
Umekwisha wenzanguni, hata tone silioni,
Mwenye nao sinihini, naomba niazimeni,
Ya manjano zafarani, ndio ilo tufitini
Kama hamniamini, nawaaga kwaherini.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
0784845394/0762845394
Mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania