Binti wa Desmond Tutu, kiongozi mashuhuri wa Kikristo wa Afrika Kusini amevuliwa joho la Ukasisi baada ya kuoa mwanamke mwenzake.
Uongozi wa Kanisa la Anglikana nchini humo umesema, Mchungaji Mpho Tutu-van Furth, Padri wa kanisa hilo amepokonywa leseni ya kuendesha shughuli za kanisa hilo ikiwemo misa, ubatizaji, ndoa na maziko kwa kuwa kanuni za kanisa hilo haziruhusu ndoa za jinsia moja.
Binti huyo amesema babake Desmond Tutu, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Angilkana nchini humo na pia mwanamapambano mashuhuri wa sera za kibaguzi hajashangazwa na habari hizo ingawa hazijafurahia.
Mpho Tutu alifunga ndoa na raia wa Uholanzi kwa jina Marceline, ambaye ni Profesa wa Tiba ya Watoto huko jijini Amsterdam Disemba mwaka jana, huku sherehe za harusi zikifanyika mjini Cape Town nchini Afrika Kusini mapema mwezi huu. Wanandoa hao waliwahi kuolewa huku nyuma na wote wana watoto.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, licha ya kuwa Kanisa la Angilikana linapinga liwati na usagaji, lakini Afrika Kusini iliidhinisha ndoa za jinsia moja mwaka 2006.