MISRI: MAANDAMANO YA WANANCHI TISHIO KWA SERIKALI.


Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetaka polisi kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kuzima kwa njia yoyote ile, maandamano ya wananchi wanaopinga hatua ya Rais Abdel Fattah el-Sisi kumpa visiwa viwili vya nchi hiyo Mfalme Salman wa Saudi Arabia.

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema kuwa, kufuatia amri hiyo, polisi wameimarisha doria katika kila kona na barabara kubwa, kwa lengo la kuzuia maandamano hayo ya wananchi. Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita, Wizara hiyo ya Mambo ya ndani ya Misri ilionya juu ya kuendelezwa maandamano hayo ya kupinga kitendo cha rais wa nchi hiyo cha kuipa Saudia visiwa viwili vya Sanafir na Tiran vilivyoko katika Ghuba ya Aqaba.

Jana pia maandamano makubwa yalifanyika katika maeneo tofauti ya Misri, ambapo polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Inafaa kuashiria hapa kwamba, hivi karibuni serikali ya majenerali wa kijeshi ya Misri imeipa serikali ya Saudia visiwa hivyo viwili vya Bahari Nyekundu kwa madai kuwa, upimaji mipaka uliofanywa umeonyesha kuwa, tangu awali visiwa hivyo vilikuwa katika maji ya Saudia, suala ambalo limetajwa na Wamisri kuwa ni usaliti. Tayari vyama na harakati za kisiasa nchini Misri kwa pamoja vimelaani vikali udhaifu wa Rais Abdel Fattah el-Sisi mbele ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia.