KUHOFIA MASHAMBULIZ YA DAESH, VISIMA VYA MAFUTA VYAFUNGWA LIBYA.

KUHOFIA MASHAMBULIZ YA DAESH, VISIMA VYA MAFUTA VYAFUNGWA LIBYA.

Maafisa usalama wa Libya wanaolinda visima vya mafuta nchini humo wamelazimika kufunga visima vitatu vya mafuta kutokana na wafanyakazi katika visima hivyo kugoma kwenda kazini kwa kuhofia mashambulio ya genge la kigaidi la Daesh.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kutoka mjini Benghazi kuwa, hivi sasa kumeenea wasiwasi nchini Libya kuwa, kundi la kigaidi la Daesh litadhibiti visima vya mafuta vya nchi hiyo na kusababisha hasara kubwa za mali na roho kwa wananchi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Hii ni katika hali ambayo katika miezi ya hivi karibuni, kundi la kigaidi la Daesh limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika visima vya mafuta vya nchi hiyo, ingawa limeshindwa hadi hivi sasa kudhibiti maeneo hayo.

Uzalishaji wa mafuta nchini Libya umepungua mno hivi sasa. Kiwango hicho ni cha chini ya khumusi moja ya kiwango kilichokuwa kikizalishwa nchini humo mwaka 2011, kabla ya kuanza kampeni ya kumg'oa madarakani Kanali Muammar Ghaddafi.

Hadi mwaka 2011, Libya ilikuwa inazalishaji mapipa milioni moja na laki sita kwa siku.