KABILA KUENDELEA KUWA RAIS WA DRC HATA BAADA YA MUHULA WAKE KUPITA.

Mahakama ya Juu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema kuwa huenda Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo akasalia madarakani hata baada ya kumalizika muhula wake iwapo uchaguzi mkuu utakosa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Katika uamuzi wake jana Jumatano, mahakama hiyo ilisema katiba hairuhusu kuwepo ombwe la uongozi nchini na kwa msingi huo, iwapo uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu utakosa kufanyika kutokana na sababu yoyote ile, basi Rais Kabila hatakuwa na budi ila kuendelea kuwa uongozini hadi mgogoro huo upatiwe ufumbuzi.

Kabila anapaswa kuondoka madarakani Novemba 19 mwaka huu baada ya kumalizika duru ya pili ya urais.

Kwa miezi kadhaa sasa, jamii ya kimataifa imekuwa ikisisitizia umuhimu wa kufanyika uchaguzi mkuu katika tarehe iliyopangwa huko Kongo DR, huku waungaji mkono wa Rais Joseph Kabila wakitaka zoezi hilo lisogezwe mbele wakisisitiza kuwa mazingira ya sasa hayaruhusu kufanyika uchaguzi. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena katika uchaguzi ujao. Machi 31 mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2277 kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kupitia azimio hilo, Baraza la Usalama lilimtaka Rais Joseph Kabila kuhakikisha kuwa uchaguzi wa rais unafanyika katika muda uliopangwa.

DAESH LIMEUA WAITHIOPIA 16 LIBYA.

Kundi la kigaidi la Daesh limetoa kanda mpya ya video ya kuogofya inayoonyesha namna magaidi hao wanavyowaua kinyama raia wa Ethiopia nchini Libya.

Kanda hiyo ya video ya dakika 29 hivi inaonyesha namna magaidi hao wa Daesh ambao walikuwa wamefunika nyuso zao walivyowaua raia wa Ethiopia kwa kuwamininia risasi kichwani huku wakiwa wamefungwa mikono na kupigishwa magoti.

Baadhi ya raia 16 wa Ethiopia waliouawa na Daesh kwa kufyatuliwa risasi walikuwa wamefungwa chini ya miti na wengine wakauawa kwenye ufuo wa bahari. Habari zinasema kuwa, raia hao wa Ethiopia waliouawa na Daesh katika ardhi ya Libya ni waumini wa dini ya Kikristo.

Kabla ya kutekeleza ukatili huo, mmoja wa magaidi hao alisoma ujumbe unaosema: "Hawa ni wafuasi wa msalaba kutoka Kanisa la maadui huko Ethiopia, ambao wamekataa kulipa kodi ya kidini au kusilimu."

Hii sio mara ya kwanza kwa kundi la kigaidi la Daesh kutekeleza unyama wa aina hii dhidi ya raia wa Ethiopia nchini Libya.

Mwezi uliopita wa Aprili, magaidi hao wenye misimamo ya mikali na hatari walitoa kanda nyingine ya video iliyoonyesha wakiua raia 30 wa Ethiopia wafuasi wa dini ya Kikristo kwa misingi hiyo hiyo eti ya kukataa kulipa kodi au kujiunga na Uislamu. Baadhi yao waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na wengine kwa kukatwa vichwa.

MAKAASISI 71 WA MAREKANI WATUHUMIWA KULAWITI WATOTO.

Dayosisi Kuu ya Kanisa Katoliki katika mji wa Baltimore jimboni Maryland nchini Marekani imefichua majina ya makasisi 71 wanaotuhumiwa kuwalawiti watoto wadogo.

Sean Caine, Msemaji wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo amesema tayari wamechapisha katika tovuti ya kanisa hilo majina ya makasisi hao wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya kuwadhulumu kimapenzi watoto wadogo.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwashajiisha waathiriwa wa vitendo vya ulawiti kujitokeza na kulizungumzia swala hili ikizingatiwa kuwa, kesi nyingi za liwati zinazohusisha viongozi wa Kanisa Katoliki zimekuwa zikifumbiwa macho huku wahusika wakikosa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Marekani, takriban makasisi 6,900 wa Kanisa Katoliki la Roma wanadaiwa kuwalawiti watoto wadogo 16,900 kati ya mwaka 1950 na 2011.

NI SAWA KWA MJAMZITO KUINUA VYUMA VIZITO KWA MAZOEZI?

Huyu ni mjamzito mwenye nguvu kubwa zaidi!

Bibi Emily Watson mwenye umri wa miaka 31 anayeishi nchini Marekani anapenda kufanya mazoezi ya viungo, hata baada ya kuwa na mimba, anaendelea kufanya mazoezi ya kunyanyua uzito kwa mara sita kila wiki. Watu wengi hawaungi mkono kitendo chake, wanasema kufanya mazoezi kupita kiasi kutaathiri vibaya mimba changa. Una maoni gani kuhusu kitendo cha mama huyu?

RAIS WA TAFF AZUNGUMZIA KIFO CHA KINYAMBE.

Akiongea na EATV Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Simon Mwakifwamba, amesema ameongea na baba mzazi wa marehemu na kuthibitisha kifo hicho, ambacho kimesababishwa kwa ugonjwa wa mapafu kujaa maji.

Mwakifwamba amesema taratibu za mazishi zinaendelea mkoani Mbeya ambako ndio nyumbani kwao marehemu, na wanaangalia kama kuna uwezekano wa wasanii wenzake kuhudhuria.
RIP Kinyambe

WALIOKUFA KWA BOMU BAGHDAD WAFIKIA 64

Idadi ya vifo kutokana na shambulizi la bomu lililotokea katika soko moja lililoko mashariki mwa mji mkuu wa Baghdad,Iraq,vimeongezeka hadi 64 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia 87,taarifa kutoka kwa Wizara ya Mambo ya ndani alisema.

Mlipuko huo mkubwa ulitokea asubuhi wakati gari lililokuwa limenaswa lililipuka katika soko maarufu katika ngome ya Shiite katika wilaya ya Sadr City,taarifa hiyo ilisema.

IRAN: HATUHITAJI RUHUSA YA MTU KUJIHAMI.

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa radiamali kuhusiana na matamshi ya msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani aliyotoa kuhusiana na mpango wa makombora wa Iran na kusema kuwa, taifa hili halihitaji kupata ruhusa ya mtu yeyote kwa ajili ya kujihami.

Ali Akbar Velayati amesema kuwa, baadhi ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama Russia inaamini kwamba, hatua hii ya Iran ya kufanya majaribio ya makombora haipingani na azimio la Baraza la Usalama.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa, Washington inayachukulia majaribio ya makombora ya balistiki ya Iran kwamba, ni hatua ya kichochezi na yenye lengo la kuvuruga uthabiti.

Iran hivi karibuni ilifanyia majaribio kombora la balistiki lenye uwezo wa kuruka masafa ya kilomita 2,000 na kulenga shabaha kwa ustadi mkubwa.

Nchi za Magharibi hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimekuwa zikikosoa majaribio ya makombora ya balisitiki Iran na kudai eti majaribio hayo yanakiuka azimio nambara 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa baada ya mapatano ya nyuklia ya Iran yaliyofikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.

GAMBIA NA SENEGAL ZIKO KATIKA MGOGORO WA MPAKA.

Mgogoro umezuka baina ya Gambia na Senegal, kutokana na kuwania mpaka kati yao.

Habari kutoka nchini Gambia zinaripoti kuwa, hali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa imezidi kuzorota nchini humo ikiwa imesalia miezi saba kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais kutokana na mgogoro huo wa kimipaka na Senegal.

Mgogoro huo uliibuka kufuatia hatua ya Rais Yahya Jammeh wa Gambia ya kuongeza kiwango cha ushuru kwa ajili ya wafanyabiashara wa magari ya mizigo kutoka Farank CFA elfu nne hadi laki nne. Hata hivyo Rais Jammeh ameituhumu serikali ya Senegal kuwa muhusika mkuu wa mgogoro huo. Inafaa kuashiria kuwa, Rais Yahya Jammeh amekuwa madarakani nchini Gambia kwa kipindi cha miaka 24 sasa.

Wapinzani wa chama tawala cha UDP, ambao wanataka kuachiliwa huru makumi ya wanasiasa wanaoshikiliwa na polisi ya Gambia, wameutaja utawala wa rais huyo kuwa usio wa kisheria. Licha ya juhudi za Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) kuzitaka Senegal na Gambia kufanya mazungumzo kwa ajili ya kutatua mgogoro huo, lakini serikali ya Dakar imesema mazungumzo hayo hayawezi kufanyika.

POLIS DRC YATUMIA MABOMU YA MACHOZI KUTAWANYA WAFUASI WA KATUMBI.

Askari polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya maelfu ya wafuasi wa kiongozi mkuu wa upinzani Moise Katumbi ambaye anahojiwa na polisi kwa tuhuma za kukodi mamluki wa kigeni.

Katumbi ambaye ametangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Novemba anapewa nafasi kubwa ya kumrithi Rais Joseph Kabila ambaye anapaswa kuondoka madarakani baada ya uchaguzi huo. Wafuasi wa kiongozi huyo wa upinzani wanasema tuhuma zilizotolewa dhidi yake ambazo zinaweza kusababisha ahukumiwe kifungo jela zimezushwa kwa lengo la kuvuruga kampeni yake ya kuwania urais.

Serikali ya DRC imesema ina ushahidi kuwa Moise Katumbi alihusika katika kusajili mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wastaafu wa Kimarekani kwa lengo la kutekeleza njama dhidi ya Jamhuri.

Kwa mujibu wa mashuhuda, polisi jana iliwatia nguvuni watu wasiopungua 10 nje ya ofisi ya Mkuu wa Mashtaka katika mji wa pili kwa ukubwa wa nchi hiyo wa Lubumbashi waliokuwa wanaelekea kwenye ofisi hiyo ambako Katumbi aliwasili wakati wa saa tano mchana ili kusailiwa kwa siku ya pili.

Moise Katumbi alikuwa Gavana wa jimbo la Katanga lililoko kusini mashariki mwa Kongo DR kuanzia mwaka 2007 hadi Septemba mwaka jana alipojitoa katika chama tawala cha Rais Kabila cha PPRD akikituhumu kuwa kinapanga njama ya kuendelea kumweka kiongozi huyo madarakani.