IJUE SARATANI(CANCER)















IJUE SARATANI(CANCER)

Saratani ni mkusanyiko wa magonjwa yanayo husiana ambayo huanza mara baada ya seli za mwili kuongezeka na kugawanyika kupita mahitaji ya mwili.
Kwa aina zote za kansa, hutokea pale baadhi ya seli za mwili kuanza kugawanyika bila kukoma na kusambaa katika tishu zingine kutoka pale zilipo anzia!
Saratani ikoje?

Awali ya yote vema mjue kuwa mwili wa mwanadamu una seli zaidi tirioni 37, na zote hizo zina kazi maalum, huchoka, huaribika, na hatimaye hufa! Seli zinapokufa zingine huzalishwa ili kuchukua nafasi ya seli zilizo kufa. Kwa hivyo ili mifumo ya mwili ifanye kazi zake vizuri ni lazima seli zilizochakaa na kuharibika zife.

Saratani huweza kuanza sehemu yoyote ya mwili wa mwanadamu. Saratani inapozuka ule mchakato wa kawaida unaotawala na kuratibu seli huacha kufanya kazi kama inavyotakiwa.
Matokeo ya mchakato kufeli, hupelekea seli kuwa si za kawaida(more and more abnormal). Seli zilizo zeeka, kuchakaa na zilizoharibika huendelea kuishi badala ya kufa kama ilivyo kawaida, na kubwa zaidi seli mpya kuzalishwa kwa wingi sana kuzidi mahitaji ya mwili.
Seli mpya hugawanyika kwa kasi na kwa wingi bila kukoma, na matokeo yake hufanya uvimbe(tumors)

Saratani nyingi hufanya uvimbe ambao ukiugusa huwa mgumu, si wenye kubonyea. Uvimbe huu huwa ni mkusanyiko wa tishu uliotokana na seli za saratani. Saratani ya damu kama vile leukemias huwa haifanyi uvimbe.

Kuna aina mbili za uvimbe wa saratani.
Kuna uvimbe wa saratani unaoitwa malignant: Uvimbe wa namna hii una uwezo kusambaa katika mwili mathalani kwa kupitia mfumo wa damu.

Kuna uvimbe unaoitwa benign ambao wenyewe seli zake hazisambai na kushambulia tishu zingine toka pale ulipozukia, uvimbe huu unaweza kuwa mkubwa lakini ukitolewa kwa upasuaji mara nyingi haurudi tena! uvimbe wa benign huweza kutokea sehemu yoyote ya mwili lakini isiwe tatizo isipokuwa tu kama ukitokea kwenye ubongo maisha ya mgonjwa huwa hatarini.
Kuna tafauti gani kati ya seli za saratani na seli za kawaida? Saratani huzuka vipi? Kuna uhusiano gani kati ya vinasaba na seli za saratani? Dalili za saratani ndio zipi? Matibabu ya saratani yakoje? Tunajikingaje na saratani?

Leo naomba niishie hapa, nikipata nafasi inshallah nitaendelea huku nikiongozwa na maswali hayo.
Nimeandika makala haya kwa msaada wa tovuti ya National Cancer Institute ya Marekani na tovuti ya American Cancer Society.
Dotto Rangimoto Chamchua (Njano5)
Admin
0622845394