AMNESTY YATAKA UGANDA IMKAMATE RAIS OMAR AL BASHIR.


Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameitaka serikali ya Uganda kumkamata Rais Omar al-Bashir wa Sudan na kumkabidhi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kwa tuhuma za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yameitaka serikali ya Uganda kutekeleza wajibu wake wa kimataifa na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC, Rais wa Sudan ambaye alienda mjini Kampala kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais Yoweri Museveni.

Muthoni Wanyeki, Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na eneo la Maziwa Makuu amesema Uganda ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na hivyo, iwapo itafeli kumkabidhi Rais wa Sudan, itakuwa imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, baada ya kula kiapo hapo jana, Rais Museveni aliikashifu ICC na kusema kuwa mahakama hiyo imegeuka na kuwa chombo cha kuwadhalilisha viongozi wa Kiafrika huku ikiwasaza viongozi makatili wa nchi za Magharibi. Kauli ya Museveni iliwaghadhabisha wajumbe wa Marekani na Umoja wa Ulaya waliokuwa wamehudhuria sherehe za kuapishwa kwake katika Viwanja vya Kololo jijini Kampala na kuwafanya kuondoka kwenye hafla hiyo.

Itakumbukwa kuwa, serikali ya Afrika Kusini ilikataa kumkamata Rais Omar al-Bashir ambaye alishiriki mkutano wa viongozi wa Afrika uliofanyika mjini Johannesburg Julai mwaka jana. Aidha Kenya ilipuuza wito wa kumkamata na kumkabidhi kiongozi huyo kwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ICC anakotakiwa kujibu tuhuma za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu; alipohudhuria sherehe za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki mwaka 2013.

HIZBULLAH YACHUNGUZA KIFO CHA KAMANDA WAKE.


Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah imesema imeanzisha uchunguzi kubaini namna kamanda wake mwandamizi alivyouawa katika kile kilichotajwa kuwa hujuma ya jeshi la utawala wa Israel.

Taarifa ya Hizbullah imesema kuwa, harakati hiyo imeanzisha uchunguzi kubaini iwapo Mustafa Badruddin aliuawa katika hujuma ya anga ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika moja ya kambi za harakati hiyo karibu na uwanja wa ndege wa Damascus au la.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, uchunguzi wao unalenga kujua iwapo kamanda huyo mwandamizi aliuawa katika shambulizi la kombora au roketi, baada ya sauti kubwa ya kishindo kusikika jana katika kambi hiyo.

Ripoti za awali zilikua zimearifu kuwa Mustafa Badruddin, kamanda mwandamizi wa Hizbullah ya Lebanon aliuawa katika hujuma ya anga ya ndege ya utawala wa Israel.

Badruddin mwenye umri wa miaka 55 na ambaye alikua mkuu wa tawi la kijeshi la Harakati ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah, alikuwa akiongoza kikosi kinachoisaidia serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria kupambana na makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Kamanda huyo ambaye pia alikua mshauri wa Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah na mkuu wa kitengo cha kiintelijensia, alikua binamu ya Imad Mughniyah, kamanda mwandamizi wa zamani wa Hizbullah ambaye aliuawa na kitengo cha ujasusi cha utawala wa Israe Mossad, mwaka 2008 katika mji mkuu wa Syria.

MAGAID WA DAESH WAUA WANAJESHI 17 WA IRAQ.


Takriban askari 17 wa jeshi la Iraq wameuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi  la Daesh katika mkoa wa Anbar, magharibi mwa nchi hiyo.

Duru za kijeshi zinaarifu kuwa, magaidi hao jana Alkhamisi walilishambulia kwa mabomu gari la kijeshi katika wilaya ya Jarayshi, yapata kilomita 10 kutoka Ramadi, makao makuu ya mkoa wa Anbar na kuua askari 17 wa jeshi la serikali.

Imearifiwa kuwa, lengo la hujuma hiyo ya magaidi wa Daesh ni kukata mawasiliano kati ya eneo la Ramadi na Tharthar, lililoko kilomita 120 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Baghdad ili kuwazuia wanajeshi wa Iraq kusonga mbele na kukomboa maeneo ambayo yanadhibitiwa na kundi hilo la kigaidi.

Aidha raia wawili waliuawa jana Alkhamisi katika hujuma tofauti ya kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la al-Obeidi, mashariki mwa Baghdad.

Hujuma za jana zimefanyika siku moja baada ya magaidi hao kutekeleza shambulizi jingine lililosababisha makumi ya watu kupoteza maisha.

Siku ya Jumatano, watu wasiopungua 64 waliuawa na wengine zaidi ya 85 kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea karibu na soko la Urayda katika kitongoji cha Sadr mashariki mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

RAIS WA GUINEA BISSAU AMFUTA KAZI WAZIRI MKUU.


Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amempiga kalamu Carlos Correia, Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kutangaza kuivunja serikali.

Akilihutubia taifa jana Alkhamisi, Rais Vaz alisema serikali ya Correia imeshindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliopo na kubuni taasisi zinazoendana na matakwa ya utawala wake.

Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amevitaka vyama vya siasa kushauriana na kumteua Waziri Mkuu mpya.

Correia alipewa jukumu la kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika mwezi Oktoba mwaka jana, akiwa ni kiongozi wa tatu kushikilia wadhifa huo ndani ya muda wa miezi mitatu. Correia kama wenzake wawili waliomtangulia, alitazamiwa na utawala wa Rais Vaz kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaotokota nchini humo unaodaiwa kuripuka kuanzia ndani ya chama tawala cha PAIGC.

Mapema mwezi Machi mwaka huu, Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioitembelea nchi hiyo kwa ajili ya kuchunguza hali ya mambo, umeyasema hayo wakati wa mazungumzo na Rais wa Guinea-Bissau, José Mário Vaz, Spika wa Bunge na viongozi wa vyama vya kisiasa.

Mgogoro wa kisiasa nchini Guinea-Bissau umekuwa mkubwa kiasi cha kufanya upatanishi wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kireno (CPLP) kushindwa kumaliza mivutano hiyo ya kisiasa

KAMANDA WA HEZBOLLAH AMEUAWA.

Kundi la wapiganaji la Hezbollah limesema kuwa kamanda wake wa juu,Mustafa Badreddine ameuawa katika shambulio la anga la Israel nchini Syria,Vyombo vya habari vimeripoti.Mustafa Badreddine anadaiwa kuhusika na mauaji ya Waziri mkuu wa Israel Rafiq Hariri mwaka wa 2005.

VIRUS VYA EBOLA HUJIFICHA HUISHI KATIKA SHAHAWA.


Utafiti waonesha kuwa virusi vya Ebola vinaweza kuishi katika shahawa ya wagonjwa wanaopona kwa mwaka mzima

Taasisi ya Pasteur ya Ufaransa imetoa taarifa ikisema, utaifiti moja uliofanywa na watafiti wa Ufaransa na Guinea unaonesha kuwa virusi vya Ebola vinaweza kuishi katika shahawa (sperms) za wagonjwa wanaopona kwa mwaka mzima.

Utafiti huo unafanywa na taasisi ya Pasteur, Taasisi ya maendeleo ya Ufaransa, Taasisi ya afya na matibabu ya Ufaransa na mashirika ya utaifi ya Guinea. Matokeo ya utafiti huo yametolewa katika jarida la “Maradhi ya kuambukiza” la Marekani.
Watafiti waliwachunguza wagonjwa 450 wa Ebola waliopona kwa mwaka mazima, na kuchambua majimaji ya mwili wao, yakiwemo machozi, mate na shahawa.

Uchambuzi wa sampuli za shahawa 98 ya wagonjwa 68 waliopona unaonesha kuwa kufuatia ongezeko la uponaji wa wagonjwa hao, idadi ya virusi vya Ebola katika shahawa zao inapungua. Katika mwezi mmoja hadi mitatu baada ya kupona kwa wagonjwa, asilimia 28.5 ya shahawa ina virusi vya Ebola; Baada ya miezi 7 hadi 9, kiwango hicho kinapungua hadi asilimia 6.5; baada ya miezi 12, virusi vya Ebola vikatoweka katika shahawa.

Hivyo, watafiti wanapendekeza wagonjwa wa Ebola wanopona katika miezi kadhaa baada ya kupona wanatumia mpira wakati wa ngono, na kushauri masharika husika kufuatilia afya za wagonjwa hao, ili kuepuka maambukizi ya virusi hivyo kuibuka tena.

NEWCASTLE NA NORWICH ZIMESHUKA DARAJA.


Ushindi wa Sunderland wa 3-0 dhidi ya Everton Jumanne uliwafikisha hadi alama 38 na kwa kuwa Norwich na Newcastle hawawezi kuwafikia, moja kwa moja klabu hizo mbili zikashushwa daraja.

Kwa sasa Norwich wana alama 34 sawa na Newcastle. Klabu nyingine iliyoshushwa daraja ni Aston Villa iliyo na alama 17 kwa sasa.
Troy Deeney alikuwa amewapa Watford uongozi mechi hiyo iliyochezewa Carrow Road lakini Norwich wakajibu kupitia bao la Nathan Redmond.

Dieumerci Mbokani aliwafungia Norwich la pili naye Craig Cathcart akawaongezea la tatu kwa kujifunga.

Odion Ighalo alikomboa bao la pili lakini Mbokani akawafungia Norwich bao la nne.
Baada ya kushushwa daraja, Norwich sasa watakuwa wakichezea tu fahari mechi yao ya mwisho dhidi ya Everton Jumapili.

WA KIMATAIFA KUIFUATA ESPERANCA JUMAPILI.


Yanga itaondoka Dar es Salaam siku moja tu baada ya kukabidhiwa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara katika mchezo dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeidhinisha mchezo Ndanda na Yanga kuchezwa Uwanja wa Taifa, badala ya Nangwanda Sijaona, Mtwara baada ya klabu hizo kukubaliana.

Yanga inatarajiwa kucheza na wapinzani wao, Sagrada Esperanca ya Angola kati ya Mei 17 au 18 mwaka huu Katika mchezo wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam Jumamosi iliyopita ambapo Yanga iliwafunga wageni wake mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga inahitaji ama sare, ushindi na kama kufungwa basi si zaidi ya bao moja ili kuindoa Esperanca katika hatua ya awali, ili kuingia hatua ya makundi katika kusonga mbele.

Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF Jamal Emil Malinzi ameipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.

Hii ni mara ya 26 kwa Yanga kutwaa taji tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965, ikifuatiwa na Simba iiliyotwaa mara 18 na Mtibwa Sugar ya Morogoro mara mbili.

Yanga imefikia rekodi hiyo baada ya kutwaa ubingwa katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992,1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006 na misimu ya 2007-2008, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013, 2014-15 na 2015-16.

Kwa upande mwingine Malinzi pia amezikumbusha na kuhamamisha klabu zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu wa 2016/17 kutoa maoni na mapendekezo, ili kuboresha kanuni za uendeshaji wa ligi hiyo kwa msimu ujao.

Yanga imetwaa ubingwa huo ikiwa na mechi mbili mkononi, dhidi ya Ndanda Jumamosi na Majimaji Mei 22 Uwanja wa Majimaji, Songea.

POPE: MASHABIKI WA SIMBA WAMEHARIBU TIMU.


Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba Zacharia Hanspope amewashutumu mashabiki kuwa ndio chanzo cha timu hiyo kufanya vibaya.

Hans pope amesema, kwa upande wa mechi za Simba na Yanga haziangalii ubora wa timu kwani zinamambo yake mengi sana na wao kama Simba walijiamini kuchukua ubingwa kutokana na mwenendo wa timu ulivyokuwa tangu mwanzo wa Ligi.

Pope amesema, kufanya vibaya kwa timu kumeanza katika mchezo wa Robo fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara waliyocheza dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam suala lililoonyesha moja kwa moja kuwa kunajambo ambalo lipo ndani ya timu na kuifanya timu kuwa hivyo.

Pope amesema, anaamini kunawatu wanawashika wachezaji ili wacheze chini ya kiwango na matokeo yake wanashindwa kushindwa mechi mbalimbali hivyo wanalifanyia uchunguzi jambo hilo ili kujua ni watu gani na wanafanya hivyo kwa sababu gani.

Pope amesema, ilionekana dhahiri wanauwezo wa kuchukua ubingwa wa msimu huu lakini walipofika katika hatua nzuri ya kuwania ubingwa wa msimu huu ndipo pale kiwango cha baadhi ya wachezaji kilipoanza kushuka.

Pope amesema, kwenye siasa za Simba na Yanga fujo huanza pale mashabiki wanapotaka kumtoa kiongozi na uongozi ukishatoka huwa wanakuwa na mtu wao wanataka aingie.

Pope amesema, fujo za safari hii zimeandaliwa kabisa na baadhi ya watu kwani imefikia hatua mpaka baadhi ya wachezaji kupiga wachezaji wenzao kwa sababu wanajua kilichofanyika katika mchezo dhidi ya Toto ambapo Simba ilipoteza kwa bao 1-0 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Pope amesema, mashabiki wanatakiwa kuangalia timu na wachezaji wanachokifanya na sio kushambulia viongozi kwani wachezaji ndio chanzo na kama wangewafuata na kuwaambia wangeweza kubadilika katika mechi zinazofuata.

Kwa upande mwingine Hans Pope amesema, kwa upande wa wachezaji kugoma wakishinikiza kulipwa mishahara yao sio sahihi kwani wanajua kabisa muda wa kulipwa mshahara ni kati ya tarehe tano au 10 sasa suala la kugoma kati ya tarehe sita na saba inaonekana ni msukumo kabisa.

Pope amesema, mshahara mara zote inatoka kwa wadhamini kwani wadhamini watatoa pesa wiki ya kwanza ya mwisho wa mwezi au wiki ya pili hivyo inaonekana kugoma kwa wachezaji ni shinikizo kutoka kwa baadhi ya mashabiki ambao hawana nia nzuri na timu hiyo.

Pope amesema, msimu huu walikuwa na timu bora kuliko misimu yote ambayo ineweza kuchukua Ubingwa lakini anaamini mashabiki wasio na nia nzuri na timu ndio chanzo cha kuiharibu timu mpaka imefikia hatua iliyopo sasa.

Simba imesaliwa na michezo miwili ikiwa na pointi 59 huku ikiendelea kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.