VIRUS VYA EBOLA HUJIFICHA HUISHI KATIKA SHAHAWA.


Utafiti waonesha kuwa virusi vya Ebola vinaweza kuishi katika shahawa ya wagonjwa wanaopona kwa mwaka mzima

Taasisi ya Pasteur ya Ufaransa imetoa taarifa ikisema, utaifiti moja uliofanywa na watafiti wa Ufaransa na Guinea unaonesha kuwa virusi vya Ebola vinaweza kuishi katika shahawa (sperms) za wagonjwa wanaopona kwa mwaka mzima.

Utafiti huo unafanywa na taasisi ya Pasteur, Taasisi ya maendeleo ya Ufaransa, Taasisi ya afya na matibabu ya Ufaransa na mashirika ya utaifi ya Guinea. Matokeo ya utafiti huo yametolewa katika jarida la “Maradhi ya kuambukiza” la Marekani.
Watafiti waliwachunguza wagonjwa 450 wa Ebola waliopona kwa mwaka mazima, na kuchambua majimaji ya mwili wao, yakiwemo machozi, mate na shahawa.

Uchambuzi wa sampuli za shahawa 98 ya wagonjwa 68 waliopona unaonesha kuwa kufuatia ongezeko la uponaji wa wagonjwa hao, idadi ya virusi vya Ebola katika shahawa zao inapungua. Katika mwezi mmoja hadi mitatu baada ya kupona kwa wagonjwa, asilimia 28.5 ya shahawa ina virusi vya Ebola; Baada ya miezi 7 hadi 9, kiwango hicho kinapungua hadi asilimia 6.5; baada ya miezi 12, virusi vya Ebola vikatoweka katika shahawa.

Hivyo, watafiti wanapendekeza wagonjwa wa Ebola wanopona katika miezi kadhaa baada ya kupona wanatumia mpira wakati wa ngono, na kushauri masharika husika kufuatilia afya za wagonjwa hao, ili kuepuka maambukizi ya virusi hivyo kuibuka tena.

NEWCASTLE NA NORWICH ZIMESHUKA DARAJA.


Ushindi wa Sunderland wa 3-0 dhidi ya Everton Jumanne uliwafikisha hadi alama 38 na kwa kuwa Norwich na Newcastle hawawezi kuwafikia, moja kwa moja klabu hizo mbili zikashushwa daraja.

Kwa sasa Norwich wana alama 34 sawa na Newcastle. Klabu nyingine iliyoshushwa daraja ni Aston Villa iliyo na alama 17 kwa sasa.
Troy Deeney alikuwa amewapa Watford uongozi mechi hiyo iliyochezewa Carrow Road lakini Norwich wakajibu kupitia bao la Nathan Redmond.

Dieumerci Mbokani aliwafungia Norwich la pili naye Craig Cathcart akawaongezea la tatu kwa kujifunga.

Odion Ighalo alikomboa bao la pili lakini Mbokani akawafungia Norwich bao la nne.
Baada ya kushushwa daraja, Norwich sasa watakuwa wakichezea tu fahari mechi yao ya mwisho dhidi ya Everton Jumapili.

WA KIMATAIFA KUIFUATA ESPERANCA JUMAPILI.


Yanga itaondoka Dar es Salaam siku moja tu baada ya kukabidhiwa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara katika mchezo dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeidhinisha mchezo Ndanda na Yanga kuchezwa Uwanja wa Taifa, badala ya Nangwanda Sijaona, Mtwara baada ya klabu hizo kukubaliana.

Yanga inatarajiwa kucheza na wapinzani wao, Sagrada Esperanca ya Angola kati ya Mei 17 au 18 mwaka huu Katika mchezo wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam Jumamosi iliyopita ambapo Yanga iliwafunga wageni wake mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga inahitaji ama sare, ushindi na kama kufungwa basi si zaidi ya bao moja ili kuindoa Esperanca katika hatua ya awali, ili kuingia hatua ya makundi katika kusonga mbele.

Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF Jamal Emil Malinzi ameipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.

Hii ni mara ya 26 kwa Yanga kutwaa taji tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965, ikifuatiwa na Simba iiliyotwaa mara 18 na Mtibwa Sugar ya Morogoro mara mbili.

Yanga imefikia rekodi hiyo baada ya kutwaa ubingwa katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992,1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006 na misimu ya 2007-2008, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013, 2014-15 na 2015-16.

Kwa upande mwingine Malinzi pia amezikumbusha na kuhamamisha klabu zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu wa 2016/17 kutoa maoni na mapendekezo, ili kuboresha kanuni za uendeshaji wa ligi hiyo kwa msimu ujao.

Yanga imetwaa ubingwa huo ikiwa na mechi mbili mkononi, dhidi ya Ndanda Jumamosi na Majimaji Mei 22 Uwanja wa Majimaji, Songea.

POPE: MASHABIKI WA SIMBA WAMEHARIBU TIMU.


Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba Zacharia Hanspope amewashutumu mashabiki kuwa ndio chanzo cha timu hiyo kufanya vibaya.

Hans pope amesema, kwa upande wa mechi za Simba na Yanga haziangalii ubora wa timu kwani zinamambo yake mengi sana na wao kama Simba walijiamini kuchukua ubingwa kutokana na mwenendo wa timu ulivyokuwa tangu mwanzo wa Ligi.

Pope amesema, kufanya vibaya kwa timu kumeanza katika mchezo wa Robo fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara waliyocheza dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam suala lililoonyesha moja kwa moja kuwa kunajambo ambalo lipo ndani ya timu na kuifanya timu kuwa hivyo.

Pope amesema, anaamini kunawatu wanawashika wachezaji ili wacheze chini ya kiwango na matokeo yake wanashindwa kushindwa mechi mbalimbali hivyo wanalifanyia uchunguzi jambo hilo ili kujua ni watu gani na wanafanya hivyo kwa sababu gani.

Pope amesema, ilionekana dhahiri wanauwezo wa kuchukua ubingwa wa msimu huu lakini walipofika katika hatua nzuri ya kuwania ubingwa wa msimu huu ndipo pale kiwango cha baadhi ya wachezaji kilipoanza kushuka.

Pope amesema, kwenye siasa za Simba na Yanga fujo huanza pale mashabiki wanapotaka kumtoa kiongozi na uongozi ukishatoka huwa wanakuwa na mtu wao wanataka aingie.

Pope amesema, fujo za safari hii zimeandaliwa kabisa na baadhi ya watu kwani imefikia hatua mpaka baadhi ya wachezaji kupiga wachezaji wenzao kwa sababu wanajua kilichofanyika katika mchezo dhidi ya Toto ambapo Simba ilipoteza kwa bao 1-0 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Pope amesema, mashabiki wanatakiwa kuangalia timu na wachezaji wanachokifanya na sio kushambulia viongozi kwani wachezaji ndio chanzo na kama wangewafuata na kuwaambia wangeweza kubadilika katika mechi zinazofuata.

Kwa upande mwingine Hans Pope amesema, kwa upande wa wachezaji kugoma wakishinikiza kulipwa mishahara yao sio sahihi kwani wanajua kabisa muda wa kulipwa mshahara ni kati ya tarehe tano au 10 sasa suala la kugoma kati ya tarehe sita na saba inaonekana ni msukumo kabisa.

Pope amesema, mshahara mara zote inatoka kwa wadhamini kwani wadhamini watatoa pesa wiki ya kwanza ya mwisho wa mwezi au wiki ya pili hivyo inaonekana kugoma kwa wachezaji ni shinikizo kutoka kwa baadhi ya mashabiki ambao hawana nia nzuri na timu hiyo.

Pope amesema, msimu huu walikuwa na timu bora kuliko misimu yote ambayo ineweza kuchukua Ubingwa lakini anaamini mashabiki wasio na nia nzuri na timu ndio chanzo cha kuiharibu timu mpaka imefikia hatua iliyopo sasa.

Simba imesaliwa na michezo miwili ikiwa na pointi 59 huku ikiendelea kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

JUKWAA LA KIMATAIFA LA KIUCHUMI KWAAJILI YA AFRIKA LIMEANZA RWANDA.

Jukwaa la kimataifa la 26 la uchumi kwa ajili ya Afrika limeanza mjini Kigali, mji mkuu wa Rwanda. Jukwaa hilo la siku tatu linawashirikisha washiriki karibu 1200 kutoka nchi 70 za dunia chini ya kauli mbiu ya 'Uunganishaji wa Vyanzo vya Afrika Kupitia Mageuzi ya Dijitali.'

Jukwaa hilo limeandaliwa katika hali ambayo bei ya malighafi imepungua sana kwa kadiri kwamba kuna ulazima wa kuanzishwa uchumi wa pande kadhaa katika upeo mzima wa uchumi wa bara la Afrika. Oliver Cann, msemaji wa jukwaa hilo huku akiashiria kuwa hali ya hivi sasa ya uchumi wa Afrika si kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita amesisitiza kwamba hivi sasa kuna ufahamu mzuri kuhusiana na ulazima wa kuwepo uchumi wa pande kadhaa barani humo kwa lengo la kuzistawisha kiuchumi nchi za bara hilo.

Lengo la kupatikana uchumi kama huo ni kuziwezesha nchi hizo kutotegemea tu malighafi katika kuendesha uchumi wao. Amesema lengo jingine la kufanyika kikao hicho ni kuainishwa mbinu za ustawi wa baadaye kwa kutegemea teknolojia ya kisasa. Jukwaa la kimataifa la uchumi hufanyika kila mwaka huko Davos Uswisi likiwashirikisha viongozi wa kisiasa na kiuchumi kutoka pembe mbalimbali za dunia.

Jukwaa la kimataifa la uchumi kwa ajili ya Afrika pia kufikia sasa limefanyika katika nchi tofauti za bara hilo kwa lengo la kuchunguza njia mbalimbali za kuimarisha uchumi wa bara la Afrika ambao una mchango mdogo wa asilimia 3 tu katika uchaumi wa dunia. Inaonekana kuwa hivi sasa wawekezaji na wanauchumi wameamua kutumia teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kuleta mageuzi makubwa katika uchumi wa Afrika.

Wakati huohuo wataalamu wa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF walitabiri mwezi Aprili uliopita kwamba uchumi wa nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara ulipungua kasi kwa asilimia 3 mwaka uliopita. Kupungua kwa bei ya mafuta kuliacha athari kubwa katika uchumi wa nchi zinazouza nje mafuta za bara hilo kama Nigeria na Angola, na hivyo kuchangia katika kupungua kwa uchumi wa bara hilo.

Wakati huohuo kupungua kwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa hakujakuwa na athari kubwa katika uchumi wa nchi zinazoagiza bidhaa hiyo muhimu barani humo. Hii ni katika hali ambayo asilimia 95 ya pato la serikali ya Angola linatokana na uuzaji wa mafuta.

Mdororo katika uchumi wa Uchina na vilevile hali ngumu ya kiuchumi duniani ni jambo ambalo limepelekea nchi nyingi za bara la Afrika kukabiliwa na nakisi ya bejeti.

Afrika Kusini ambayo inahesabiwa kuwa moja ya nchi zenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika pia inakabiliwa na hali ngumu ya uchumi ambapo uchumi wake unatathminiwa kukuwa kwa asilimia ndogo sana mwaka huu. Mivutano ya kisiasa na upinzani dhidi ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo ni jambo ambalo linashirikiana na ukame na vilevile kupungua thamani ya sarafu ya taifa katika kupunguza ustawi wa uchumi wa nchi hiyo.

Mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na Elnino yamevuruga pakubwa sekta za kilimo katika nchi za mashariki na kusini mwa bara la Afrika, zikiwemo za Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Malawi. Kupungua kwa mazao ya kilimo nchini Zimbabwe na bei ya shaba katika soko la kimataifa ni masuala muhimu ambayo yameathiri uchumi wa nchi hiyo na Zambia ambayo huzalisha kiwango kikubwa cha shaba duniani.

Katika eneo la mashariki mwa Afrika ukame umeathiri sana Ethiopia kwa kiwango ambacho kilikuwa hakijawahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa iliyopita. Ni kwa kuzingatia suala hilo ndipo wataalamu wa IMF wakatabiri kwamba uchumi wa nchi hiyo utapungua kutoka asilimia 10 mwaka uliopita hadi asilimia 4.5 mwaka huu.

WHO: %80 YA WAKAZI WA MJINI WANAVUTA HEWA CHAFU.

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonya kuwa hali ya uchafuzi wa hewa inazidi kuwa mbaya duniani kote huku zaidi ya asilimia 80 ya wakaazi wa miji mikubwa wakivuta hewa chafu na kuongeza hatari ya kupatwa na saratani ya mapafu na maradhi mengine hatari.

Ripoti hiyo ya WHO imebainisha kuwa wakaazi wa mijini katika nchi masikini ndio wanaoathiriwa zaidi na kufafanua kwamba ni asilimia mbili tu ya miji katika nchi za kipato cha chini na cha kati ambayo watu wake wanavuta hewa inayokidhi viwango vya shirika hilo la kimataifa la afya. Kiwango hicho ni asilimia 44 katika miji ya nchi tajiri.

Ripoti ya Shirika Afya Duniani imezingatia utafiti iliofanya katika miji 795 ya nchi 67 katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 hadi 2015.

Kwa kuzingatia kiwango cha mada zenye madhara kama sulfeti na kaboni nyeusi, WHO imegundua kuwa hewa inachafuka zaidi katika maeneo ya nchi zinazoendelea hususan katika Mashariki ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia.

Utafiti huo wa shirika la Afya Duniani umeonesha kuwa India ina miji 15 kati ya 30 duniani yenye hewa chafu zaidi.

Mji wa Zabol ulioko mashariki mwa Iran ndio wenye hewa chafu zaidi ukifuatiwa na miji ya Gwalior na Allahabad ya India na Riyadh na Jubail ya Saudi Arabia

MUUAJI WA MTU MWEUSI APIGA MNADA SILAHA YAKE.

George Zimmerman, muuaji wa Trayvon Martin, kijana wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika ametangaza kuwa anaipiga mnada kwenye mtandao wa intaneti silaha aliyomuulia kijana huyo.

Zimmerman, mlinzi wa kizungu ambaye tarehe 16 Februari mwaka 2012 alimpiga risasi na kumuua Trayvon Martin pasina kuwa na silaha yoyote na kisha akafutiwa shtaka hilo hivi sasa ameamua kuipiga mnada silaha yake hiyo.

Kwa mujibu wa Zimmerman mwenyewe, silaha hiyo amerejeshewa na Wizara ya Sheria ya Marekani ambayo iliichukua kutoka kwake wakati kesi yake ilipokuwa ikiendelea na baada ya kufutiwa mashtaka.

Mnada wa kuiuza silaha hiyo umeanza jana Alhamisi na bei ya kuanzia imetajwa kuwa ni dola elfu tano.

Mauaji ya Trayvon Martin ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17 na hatimaye kufutiwa mashtaka George Zimmerman kulizusha wimbi kubwa la machafuko na malalamiko katika kila pembe ya Marekani; na maandamano makubwa yakafanyika nchini humo na katika baadhi ya nchi za kigeni kulalamikia ubaguzi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

SOMALIA YAKOSOA MPANGO WA KENYA KUFUNGA KAMBI ZA DADAAB.

Serikali ya Somalia imekosoa azma ya Kenya ya kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab yenye mamia ya maelfu ya wakimbizi na haswa raia wa Kisomali.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema kufungwa kwa kambi hiyo hakutakua na tija nyingine ghairi ya kuwasukuma wakimbizi hao kujiunga na makundi ya kigaidi kama vile al-Shabab. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kuwatimua wakimbizi hao wakati huu ambapo nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iko mbioni kuhakikisha kuwa inarejesha usalama, uthabiti na kuimarisha taasisi zake, kutayumbisha zaidi usalama wa kanda hiyo. Kambi ya Dadaab ina wakimbizi wapatao 350,000, aghalabu yao wakiwa ni raia wa Kisomali.

Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kuitaka serikali ya Kenya kufikiria upya mpango wake wa kufunga kambi hiyo huku ukisisitza kuwa, usalama wa maelfu ya wakimbizi wa Kisomali na raia wa Sudan Kusini kwa takriban robo karne umekuwa ukitegemea ukarimu wa Kenya na nia yake ya kutaka kuonyesha mfano bora katika eneo wa kutekeleza wajibu wake wa kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF nalo limetoa taarifa likisema kuwa, kutekelezwa kwa uamuzi huo kutawaweka maelfu ya wakimbizi hatarini. Licha ya mashirika mbalimbali ya kimataifa kuendelea kuitaka Kenya ifikirie upya uamuzi wake wa kutaka kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab, serikali ya Nairobi imesisitiza kwamba, inalazimika kuifunga kambi hiyo ya wakimbizi kutokana na mzigo mzito wa kiusalama, kiuchumi na masuala ya kimazingira.

UN YAITAKA SUDAN KUSINI KUFUATILIA JINAI ZA NGONO.

Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ukatili wa Kingono Katika Migogoro ameutaka uongozi mkuu wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya Sudan Kusini utekeleze ahadi ulizotoa za kufuatilia jinai za ukatili wa kingono zilizofanywa nchini humo.

Akikamilisha safari yake ya siku nne mjini Juba hapo jana, Zainab Hawa Bangura, ameeleza mbele ya waandishi wa habari kuwa kutekelezwa kwa mafanikio makubaliano ya amani kutahitaji kuhakikisha kuwa jinai za ukatili wa kingono zinafuatiliwa, kufahamika na kuripotiwa na kushughulikiwa katika vyombo vyote vya sheria vya serikali ya mpito.

Mwakilishi huyo Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ukatili wa Kingono Katika Migogoro amebainisha kuwa ahadi hizo zimo kwenye taarifa ya pamoja ambayo waliisaini yeye na Rais Salva Kiir Oktoba 11 mwaka 2014 na pia kwenye taarifa ya upande mmoja iliyotolewa Desemba 18 mwaka 2014 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa hivi sasa wa nchi hiyo Riek Machar.

Bi Bangura amesisitiza kuwa licha ya ahadi hizo na hatua zilizopigwa katika utekelezaji lakini jinai za ukatili wa kingono zimeendelea kufanywa katika muktadha wa mgogoro wa nchi hiyo.

Katika safari yake ya siku nne nchini Sudan Kusini iliyotokana na mwaliko wa serikali ya Juba, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ukatili wa Kingono Katika Migogoro amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Salva Kiir, Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar na maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. Bi Zainab Hawa Bangura amefanya mazungumzo pia na makundi ya wanawake yanayotoa huduma kwa manusura wa ukatili wa kingono, jumuiya ya utoaji huduma za kibinadamu na jopo la wanadiplomasia walioko nchini humo.