WAASI WA UGANDA WASHAMBULIA MASHARIKI YA DRC.

WAASI WA UGANDA WASHAMBULIA MASHARIKI YA DRC.

Watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya waasi wa Uganda kufanya mashambulizi kwenye maeneo hayo.

Mtandao wa habari wa Africa Time umezinukuu duru za kijeshi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zikitangaza kuwa, wanajeshi wawili wa nchi hiyo waliuawa jana Jumanne baada ya waasi wa ADF wa Uganda kufanya mashambulizi katika mji wa Opita, kaskazini mwa mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo na wanajeshi wengine wanne wamejeruhiwa. Hata hivyo duru hizo hazikusema chochote kuhusu hasara walizopata waasi katika mapigano hayo.

Waasi wa Uganda wanaoipinga serikali ya Rais Yoweri Museveni wako mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 1995 hadi hivi sasa. Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Kongo pamoja na serikali ya nchi hiyo wanaamini kuwa waasi hao wa Uganda wamefanya mauaji ya raia 550 katika eneo la Beni huko Kivu Kaskazini tangu mwezi Oktoba 2014 hadi hivi sasa.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetumbukia kwenye machafuko na mashambulio ya waasi kwa miaka 20 sasa. Jeshi la Kongo pamoja na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa hadi sasa wameshindwa kudhibiti vitendo hivyo vya waasi na kuwaletea amani na usalama wakazi wa maeneo hayo.

KABURI LA PAMOJA LA WATU 350 LAGUNDULIKA KASKAZIN MWA NIGERIA.

KABURI LA PAMOJA LA WATU 350 LAGUNDULIKA KASKAZIN MWA NIGERIA.

Karibu miili 350 ya Waislamu imepatikana ikiwa imezikwa kwa siri katika kaburi la umati kaskazini mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kano, Muhammad Namadi Musa, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Wafuasi wa Dini Mbalimbali amesema kugunduliwa kaburi hili la umati ni ushahidi wa wazi kuwa mamia ya Waislamu waliuawa Desemba mwaka jana wakati jeshi la Nigeria lilipowashambulia Waislamu wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria katika jimbo la Zaria.

Katika tukio hilo, jeshi la Nigeria liliwafyatulia risasa wafuasi wa harakati hiyo inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye sasa anashikiliwa na jeshi la nchi hiyo akiwa na majeraha na risasi mwilini.

Siku ya Jumatatu mwanaharakati mmoja maarufu wa nchini Uingereza alikosoa vikali ukimya wa jamii ya kimataifa juu ya mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu nchini Nigeria.

Masoud Shajareh mkuu wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) yenye makao yake London amesema ni miezi kadhaa sasa imepita tangu kujiri mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu nchini Nigeria ambapo hadi sasa ukatili huo haujachunguzwa.

IRAN YASEMA UWEZO WAKE MKUBWA WA KIJESHI SIO TISHIO, BALI WA KIJIHAMI NA FYOKOFYOKO ZA AINA YOYOTE.

IRAN YASEMA UWEZO WAKE MKUBWA WA KIJESHI SIO TISHIO, BALI WA KIJIHAMI NA FYOKOFYOKO ZA AINA YOYOTE.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) linaendelea na mazoezi makubwa ya kijeshi katika eneo la kusini mashariki mwa nchi.

Luteka hiyo iliyopewa jina la Mtume Mtukufu SAW imeanza Jumanne katika mkoa wa Sistan na Baluchestan ambapo pia kumezinduliwa ndege mpya isiyo na rubani au drone ilioyotengenezwa hapa nchini na yenye uwezo mkubwa.

Drone hiyo ijulikanayo kama Hamasa inatumika kwa mara ya kwanza katika mazoezi ya jeshi baada ya uundwaji wake kutangazwa miaka miwili iliyopita. Drone hiyo ina uwezo mkubwa wa kazi za upelelezi na kurusha makombora mbali na kuwa na uwezo wa kuruka juu sana. Drone zingine zilizotengenezwa nchini Iran zinazotumika katika luteka hiyo ni pamoja na Mohajer, Ababil na Shahed.

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema mazoezi hayo ya siku tatu yatafanyika pia katika mikoa ya Kerman, Khorasan Kusini na Hormozgan.

Hivi karibuni pia vikosi vya ulinzi vya Iran vilifanya mazoezi na kufanyia majaribio zana za kisasa za kujihami. Machi 9 IRGC ilifanyia majaribio yaliyofana makombora mawili ya balistiki ya Qader-H na Qader-F. Machi nane pia Iran ilifanya majaribio yaliyofana ya kombora la Qiam.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi si tishio kwa nchi yoyote bali ni kwa ajili ya kujihami.

RUSSIA YASEMA UVAMIZI WA MAREKANI HUKO LIBYA NDIO CHANZO CHA KUVURUGIKA NCHI HIYO YA AFRIKA.

RUSSIA YASEMA UVAMIZI WA MAREKANI HUKO LIBYA NDIO CHANZO CHA KUVURUGIKA NCHI HIYO YA AFRIKA.

Serikali ya Russia imesema kuwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani huko Libya ni hatua iliyovuruga uthabiti wa nchi hiyo.
Serikali ya Russia imesema kuwa hatua ya Marekani na waitifaki wake ya kuivamia kijeshi Libya na kupelekea kung'olewa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi, imesababisha kugawanyika Libya.

Serikali ya Russia imeutaja uvamizi wa kijeshi wa Marekani huko Libya, kuwa ni pigo kubwa kwa nchi hiyo.

Rais Vladimir Putin wa Russia mara kadhaa alishawahi kutahadharisha kuhusu athari za kuvamiwa kijeshi Libya na kile kinachoshuhudiwa hivi sasa nchini humo.

Akizungumza kwenye mahojiano na televisheni ya Fox News ya Marekani, Rais Barack Obama wa nchi hiyo juzi Jumapili alisema kuwa athari za kuishambulia kijeshi Libya, zilikuwa ni kosa lake kubwa, japokuwa wakati huo alikuwa akidhani kwamba uvamizi huo ulikuwa sahihi. Rais Obama aliyatamka hayo wakati alipoulizwa swali kuhusu kosa kubwa zaidi alilowahi kufanya katika kipindi cha utawala wake.

Baada ya mapinduzi ya wananchi wa Libya na kung'olewa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi, baadhi ya nchi ziliyaunga mkono makundi ya kigaidi nchini humo, na kuzuia kuingia madarakani utawala wa kidemokrasia.

JIMMY CARTER: MAREKANI NI NCHI AMBAYO DAIMA IKO VITANI.

JIMMY CARTER: MAREKANI NI NCHI AMBAYO DAIMA IKO VITANI.

Sera za kijeshi na za kupenda vita za Marekani zinakosolewa kote duniani na hivi sasa hata wakuu wa nchi hiyo wameanza kukosoa sera hizo.

Jimmy Carter, rais wa 39 wa Marekani kutoka mwaka 1977 hadi 1981, katika mahojiano na jarida la Time amesema tokea kuanzishwa Umoja wa Mataifa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia hadi sasa, Marekani daima imekuwa vitani.

Rais huyo wa zamani wa Marekani ambaye aliwahi kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel, amesema tangu kumalizika Vita Vikuu Vya Pili vya Dunia Marekani imeanzisha vita katika nchi 30 duniani.

Matamshi ya rais wa zamani wa Marekani ni dalili ya wazi kuwa nchi hiyo haiwezi kutekeleza mipango yake ya kiuchumi na kisiasa pasina kuwepo vita.

Kwa hakika, Marekani katika muundo wake wa sasa iliibuka katika nusu ya pili ya karne ya 18 baada ya kupigana vita vya uhuru na Ufalme wa Uingereza. Tokea wakati huo nchi hiyo kimsingi imekuwa vitani. Marekani ilipigana vita na Uingereza mwaka 1812, kisha ikaingia vitani na Mexico mwaka 1846 na vita na Uhispania mwaka 1898. Kisha iliingia katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia mwaka 1917 na baada ya hapo ikaingia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilivyoanza mwaka 1941.

Baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Marekani iliendeleza sera zake za kichokozi na vita kwa kisingizio cha kutetea kile inachodai kuwa ni uhuru duniani. Hapa tunaweza kutaja baadhi ya vita ambavyo Marekani imejihusisha navyo tokea wakati huo ambavyo ni, Vita vya

MKUTANO JUU YA NJIA IPI LIPITE BOMBA LA MAFUTA UNAFANYIKA UGANDA.

MKUTANO JUU YA NJIA IPI LIPITE BOMBA LA MAFUTA UNAFANYIKA UGANDA.

Mkutano unaohusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Bahari ya Hindi ulianza jana katika mji mkuu wa Uganda Kampala.

Taarifa zaidi kutoka Uganda zinasema kuwa, mkutano huo unayashirikisha mataifa waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Kenya, Uganda na Tanzania- ambapo baada ya siku tatu maafisa wa serikali kutoka mataifa hayo wataamua iwapo bomba hilo linafaa kutoka Uganda na kupitia nchini Tanzania hadi Bandari ya Tanga au kupitia Kenya hadi Bandari ya Lamu au Bandari ya Mombasa.

Bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Uganda litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima eneo la ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Bomba la kutoka Hoima na kwenda Lokichar kisha hadi Lamu litakuwa na urefu wa kilomita 1,476.

Bomba la kutoa mafuta Lokichar kisha kupitia Hoima nchini Uganda na kufika Tanga litakuwa na urefu wa kilomita 2,028.

Hivi karibuni Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania iliwahakikishia Watanzania kuwa serikali ya nchi hiyo ina uhakika wa asilimia 98 wa kupata mradi wa ujenzi wa bomba hilo la mafuta kutoka Uganda kuelekea bandari ya Tanga, mradi ambao unapiganiwa pia na nchi jirani ya Kenya.

WAZIRI MKUU WA ITALY YUKO JIJINI TEHRAN.

WAZIRI MKUU WA ITALY YUKO JIJINI TEHRAN.

Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi amewasili mjini Tehran mapema leo akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake.
Katika uwanja wa ndege, Waziri Mkuu wa Italia alilakiwa na Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara Muhammad Reza Neematzadeh.

Katika safari yake hiyo inayolenga kuinua na kustawisha kiwango cha uhusiano baina ya pande mbili baada ya kipindi cha vikwazo dhidi ya Iran, Matteo Renzi ameandamana na ujumbe wa watu 250 unaojumuisha maafisa wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake.

Imeelezwa kuwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Hassan Rouhani pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kustawisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa nchi mbili pamoja na kushiriki mashirika na wawekezaji wa Italia katika sekta ya uchumi na biashara ya Iran, ni miongoni mwa malengo ya safari ya Waziri Mkuu wa Italia hapa nchini.

Kabla ya safari yake hiyo, Matteo Renzi alisisitiza kuwa Italia imedhamiria kustawisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote na kufidia fursa yake iliyopoteza ya biashara na Iran katika kipindi cha vikwazo vilivyowekwa na Magharibi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Italia inakusudia kurejesha kiwango cha mabadilishano ya kibiashara na Iran cha mwaka 2010, ambacho ni cha yuro bilioni saba kwa mwaka.

FUAD MASUM: ILI IRAQ IWEZE KUPAMBANA NA MAGAIDI INAHITAJI MISAADA YA KIMATAIFA.

FUAD MASUM: ILI IRAQ IWEZE KUPAMBANA NA MAGAIDI INAHITAJI MISAADA YA KIMATAIFA.

Rais wa Iraq amesema kuwa, ili nchi hiyo iweze kupambana na ugaidi inahitajia himaya ta kimataifa.

Rais Fuad Masum amesema hayo mjini Baghdad katika mazungumzo yake na Jean-Yves Le Drian Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa na kutoa wito wa kuongezwa ushirikiano mpana zaidi wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama na Iraq katika vita dhidi ya ugaidi.

Kwa upande wake Salim al-Jabouri, Spika wa Bunge la Iraq amesema katika mazungumzo yake na Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa kwamba, vikosi vya Iraq vimefanikiwa kupata ushindi muhimu na kuweza kuikomboa miji na maeneo ya mkoa wa al-Anbar na Nainawa na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwatimua wanachama wa kundi la kigaidi ambalo ni tishio kwa ulimwengu mzima.

Katika safari yake hiyo nchini Iraq, Jean-Yves Le Drian Waziri wa Ulinzi wea Ufaransa ametangaza himaya ya nchi yake kwa Iraq katika vita dhidi ya ugaidi.

Kundi la kigaidi la Daesh liliyateka maeneo mengi ya kaskazini na magharibi mwa Iraq mwezi Juni mwaka 2014 ambapo sanjari na kutenda jinai nyingi dhidi ya wananchi wa nchi hiyo, limefanya uharibifu mkubwa katika maeneo ya kihistoria, kidini na turathi za kiutamaduni. Hata hivyo hivi sasa jeshi na vikosi vya wananchi huko Iraq vimefanikiwa kukomboa maeneo muhimu kutoka kwa kundi hilo la kigaidi na kila leo habari zinaonesha kuzidi kulemewa kundi hilo la kitakfiri.

WAMISRI WAJA JUU KWA RAIS WAO KUTOA VISIWA VIWILI KWA SAUDIA.

WAMISRI WAJA JUU KWA RAIS WAO KUTOA VISIWA VIWILI KWA SAUDIA.

Al Sisi akabiliwa na upinzani mkubwa wa Wamisri kwa hatua yake ya kuipatia Saudia visiwa viwili

Wananchi wa Misri kuanzia wale wa matabaka ya kawaida, wanaharakati hadi maafisa wa zamani na wanasiasa wameungana katika safu moja kuonyesha kukasirishwa kwao na uamuzi wa Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo wa kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vilivyoko katika bahari Nyekundu.

Serikali ya Misri Jumamosi wiki hii ilitangaza kuwa inaikabidhi Saudi Arabia mamlaka ya visiwa viwili vya kiistratejia kwa majina ya Tiran na Sanafir vinavyopatikana katika Ghuba ya Aqaba, baada ya Mfalme Salman wa nchi hiyo kuwasili mjini Cairo kwa ziara ya siku tano.

Tangazo hilo la kushtukiza limeamsha hasira na malalamiko ya Wamisri ambao walikuwa wakivitambua visiwa hivyo kuwa ni ardhi yao kwa miongo mingi.

Wanaharakati mbalimbali nchini Misri wametoa maoni yao wakisema kuwa Rais al Sisi anauza ardhi ya Misri kwa muitifaki tajiri kupitia mapatano ya udhalilishaji.