Mama mzazi wa binti mmoja mkazi wa Dakawa wilaya ya Mvomero mkoani
Morogoro hivi karibuni alipokea ujumbe wa picha ya video katika simu
yake ya mkononi na haraka aliifungua akiwa na shauku ya kuitazama.
Lahaula!
Shauku yake ya kuitazama video hiyo aliyodhani ni sawa na nyingine za
matukio ambazo amekuwa akiziona zikisambazwa mitandaoni, iligeuka huzuni
na fedheha kubwa alipoona ikimwonyesha bintiye akidhalilishwa na
wanaume huku akilalamika asirekodiwe bila mafanikio.
Mama huyo
alijizoazoa haraka na simu yake akatimua mbio hadi Polisi kuripoti tukio
hilo lililolenga kumdhalilisha binti yake na kuifedhehesha familia
nzima. Hicho ndiyo kiini cha vijana 11 wa Dakawa kukamatwa ili waisaidie
Polisi kuhusu walioshiriki tukio hilo na walioisambaza video hiyo kwa
mama huyo na kwenye mitandao ya kijamii hasa WhatsApp.
Katika
video hiyo, wakati mwanamme mmoja akimdhalilisha huyo binti, mwingine
alikuwa akirekodi na baada ya kukamilisha tendo hilo lisilo na utu tena
bila huruma waliwatumia watu wengine katika eneo la Dakawa.
Mkuu
wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa aliliambia gazeti hili jana kuwa
miongoni mwa watu wa kwanza kuona video ile alikuwa mama wa msichana.
“Alikimbia polisi kwenda kutoa taarifa,”alisema Betty.
Baada ya
kufika Polisi, Betty alisema polisi walimwambia mama huyo hawawezi
kuandika maelezo hadi mhusika ambaye ni binti yake afike kituoni.
Walisema hivyo kwa sababu ni mtu mzima hivyo anatakiwa kutoa maelezo
mwenyewe. Saa chache baada ya kuandikisha maelezo yake, polisi
waliwakamata vijana wawili kwa tuhuma za kuhusika na unyama huo. Betty
alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi na leo watafikishwa mahakamani.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kwamba suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na kwamba
hadi jana watuhumiwa 11 walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda
Matei alisema tisa kati yao wanaoshikiliwa ni kwa kosa la kusambaza
picha za utupu huku vijana wawili ambao ni Zuberi Thabiti (30) na Iddy
Adamu (32) ni kwa kosa la kufanya mapenzi na msichana huyo kwa nguvu
huku wakirekodi.
Ilivyokuwa Akisimulia tukio
hilo, Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walifanya kitendo hicho
Aprili 28 mwaka huu majira ya saa 1.00 usiku katika nyumba ya kulala
wageni yenye jina la ‘Titii’ iliyopo Dakawa.
Kamanda Matei
alisema kuwa binti huyo aliitwa kwenye nyumba hiyo ya wageni na Thabiti
ambaye ni mkazi wa Mbarali wilaya ya Mbeya ambaye alikuwa na uhusiano
naye kimapenzi. Baada ya kuingia chumbani alimkuta pia Adamu mkazi wa
Makambako, Njombe ambao walimlazimisha kufanya mapenzi huku mmoja
akimrekodi picha za video na baadaye kuzisambaza kwenye mitandao
mbalimbali ya kijamii.
Wanaoshikiliwa kwa kosa la kusambaza
picha za utupu ni Rajabu Salehe (26), Said Athman (26), Musi Ngai (36),
Said Muhammed (24), John Peter (24), Hassan Ramadhan (27), Ramadhan Ally
(26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjone (30).
Wote ni wakazi wa Dakawa, Morogoro na wamevunja Sheria ya Makosa ya Mitandao, kifungu namba 14, kifungu kidogo (1) (a)
Kamanda
Matei alisema wakati wa tukio hilo watuhumiwa hao walimtisha binti huyo
kwa kisu ili asipige kelele wakati akidhalilishwa na walimtaka asitoe
siri hiyo vinginevyo watamuua.
Kamanda alisema wawili hao ni
marafiki wa msichana huyo na kwamba Thabiti ambaye ni mpenzi wa sasa wa
msichana huyo alipanga na Adamu ambaye ni mpenzi wake wa zamani
kumkomesha.
Alisema Thabiti alimwambia mpenzi wake wakutane
hotelini. Msichana alipofika aliwakuta chumbani huku Adamu akiwa
ameshika kisu na kamera. “Wakamlazimisha afanye vile na kumtishia kumuua
kama angekataa,”alisema Matei.
Hata hivyo, Betty alisimulia
kisa hicho na kusema watuhumiwa hao walifanya unyama huo kwa sababu ya
usaliti wa mapenzi. Alisema msichana alidaiwa kujihusisha kimapenzi na
dereva wa mpenzi wake.
Kwa mujibu wa Betty, baada ya mpenzi wake
kugundua alipanga njama ili kuwakomoa wote wawili. Alisema mpenzi wake
alimwambia wakutane hotelini na alipofika alimkuta Zuberi pamoja na
dereva wa mchumba wake hotelini.
“Akawambia wafanye kile kitendo
huku akirekodi video,”alisema Betty. “Nia yake ilikuwa kuwakomoa…kwa
nini atembee na dereva wake,”alisema Betty na kwamba baada ya hapo picha
hizo zilianza kusambaa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba
alisema hali hiyo inaonyesha jinsi maadili yanavyozidi kuporomoka katika
jamii.
“Hilo siyo kosa la kisheria peke yake ni udhalilishaji mkubwa,”alisema.
Dk
Hellen alisema licha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kukemea suala hilo ni vyema jamii
ikazingatia suala la maadili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Edda Sanga alisema vyama vya
kutetea haki za wanawake vinafanya mkutano wa pamoja kujadili suala
hilo.
“Leo (jana) tumekutana ili tujadili na kuja na tamko la
pamoja,”alisema Sanga na kuongeza kwamba jambo hilo halivumiliki kwa
sababu vitendo kama hivyo vinaendelea kujitokeza mara kwa mara.
- Imenukuliwa kutoka gazeti MWANANCHI