WATU ZAIDI 69 WAMEKUFA KATIKA MLIPUKO PAKISTAN.

WATU ZAIDI 69 WAMEKUFA KATIKA MLIPUKO PAKISTAN.

Zaidi ya watu sitini na tisa wamekufa na wengine kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea kwenye eneo la wazi la kupumzikia lenye shughuli nyingi katika mji wa Lahore nchini Pakistan.

Polisi wanasema mlipuaji mwenye kujitoa mhanga alijilipua karibu na eneo la kuchezea watoto mahali wazazi walipokuwa wamejikusanya ambao baadhi yao walikuwa wakisherehekea siku kuu ya Pasaka.

Wengi ya waliokufa na kujeruhiwa katika tukio hilo ni watoto. Tayari kundi la Talbani la Pakistan la Jamaat ul Ahrar limekiri kuwa ndilo linalohusika na shambulizi hilo. Msemaji wa kundi hilo amesema walikusudia kuwalenga jamii ya wakristo waliopo katika mji huo.

Afzal ni mmoja ya wakazi wa mji wa Lahore yeye alikuwa ni miongoni mwa waliosaidia kuwasaidia majeruhi baada ya mlipuko kutokea.

" Nimewabeba zaidi ya watoto ishirini ambao walipelekwa hosptalini. Nilisaidia kubebe miili mitatu na kupakia kwenye gari la polisi. Wakati mlipuko ulipokuwa unatokea watoto walikuwa wakicheza kwenye uwanja huo wa wazi. Leo jamii ya wakristo walimaliza mfungo na kusherehekea Pasaka. Wakristo wengi walifika hapa katika tukio hili. Siwezi kuelezea jinsi tukio hilo la kusikitisha lilivyokuwa."

Naye Tariq Fatimi ambaye ni mshauri wa Waziri Mkuu wa Pakistani ameiambia BBC kuwa tukio hilo ni la kinyama bila kujali ni nchi gani imelengwa.

" Hata kama shambulizi hilo limetokea Peshawar au Lahore au Brussels au Paris au London, Sisi sote tunapaswa kuwa pamoja kwa sababu huu ni uhalifu ambao hauathiri nchi moja pekee, au jamii moja lakini inaathiri wanadamu wote."

PADRI ATIMULIWA KWA KULAWITI VIJANA ITALIA.

Padri wa Kikatoliki atimuliwa kwa kuwalawiti vijana Italia 

Padri mmoja wa Kanisa Katoliki mjini Milan nchini Italia amesimamishwa kazi baada ya kubainika kuwa amekuwa akimhonga kijana mmoja barobaro ili afanye naye ulawiti.

Askofu Mkuu wa Kanisa hilo katika eneo la Muggiano mjini Milan, Kadinali Angelo Scola amesema kuwa amemsimamisha kazi Padri Alberto Paolo Lesmo wa kanisa hilo, kwa tuhuma za kumhadaa kijana aliyekuwa mraibu wa mihadarati kati ya mwaka 2009 na 2011 na kisha kufanya naye tendo la liwati.

Kadinali huyo amesema: “Ni majuzi tu tumegundua kuwa Padri Lesmo alikuwa anafanyiwa uchunguzi na vyombo vya dola kuhusu uozo huo tangu mwaka 2013; hata hivyo tumeanzisha uchunguzi wetu juu ya tuhuma hizo, lakini kwa sasa tumemvua Upadri na kumsimamisha kazi.”

Madai ya liwati na visa vya kushiriki ngono na watoto wadogo sio mapya kwa Kanisa Katoliki, na katika miaka ya hivi karibuni, waathiriwa wa vitendo hivyo vichafu wamekuwa wakijitokeza hadharani na kufichua kashfa hizo.

Licha ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis kutoa dikrii ya kutaka kuchukuliwa hatua za kinidhamu maaskofu wanaoficha kashfa za kulawitiwa watoto wadogo na mapadri wa kanisa hilo, lakini visa hivyo vimekuwa vikiripotiwa kila uchao.

Miongoni mwa nchi ambazo zimerekodi idadi kubwa ya wakuu wa Kanisa Katoliki kugunduliwa kuwa wanawalawiti wavulana wadogo ni Marekani, Ireland, Uholanzi, Australia, Ufaransa, Ujerumani, Austria, Ubelgiji, Canada, Mexico na Poland.

ISRAELI KUSHIRIKIANA FBI KUDUKUA SIMU.

ISRAELI KUSHIRIKIANA FBI KUDUKUA SIMU.

Baada ya Shirika la Simu za Apple kukataa kushirikiana na Idara ya Polisi ya Upelelezi Marekani FBI katika kuifungua simu aina ya iPhone iliyotumiwa na mtu anayedaiwa kutekeleza mauaji San Bernardino, California mwaka jana, shirika moja la Kizayuni limepewa jukumu la kuifungua simu hiyo.

FBI imesema kuwa imepata njia ya kuifungua simu hiyo ambayo imefungwa na nywila ya siri. Shirika la mitandao ya intaneti la Cellebrite ambalo huunda programu za kiusalama za simu za mkononi, limesema linashirikiana na FBI kuidukua simu hiyo.

Shirika la Cellebrite ambalo ni tawi la shirika la Sun Corp la Japan limesema linaweza kuunda programu mpya itakayowezesha kufunguliwa simu hiyo ya iPhone na hivyo kuhitimisha mvutano baina ya FBI na Apple.

FBI imekuwa ikilishinikiza shirika la Apple kufungua simu ya iPhone iliyokuwa ikitumiwa na mmoja kati ya waliotekeleza mauaji ya San Bernardino lakini Apple imekataa kufanya hivyo kwani huo utakuwa mwanzo wa kudukuliwa taarifa katika simu za watumiaji wa simu za iPhone.

Shirika la Apple limeishtaki FBI katika mahakama nchini Marekani lakini kesi hiyo ambayo ilikuwa imepangwa kusikilizwa Jumamosi iliyopita imeakhirishwa kufuatia ombi la serikali ya Marekani. Watetezi wa haki za binadamu wamelalamikia hatua ya kuakhirishwa kesi hiyo. Wiki mbili zilizopita pia, Rais Obama wa Marekani alisema anapinga kuundwa simu za mkononi ambazo maafisa wa serikali hawataweza kupata maelezo yaliyo ndani kila wanapotaka. Kwa m

VIONGOZI WA UPINZANI CONGO BRAZZAVILLE WAITISHIA KUANDAMANA NCHI NZIMA.

VIONGOZI WA UPINZANI CONGO BRAZZAVILLE WAITISHIA KUANDAMANA NCHI NZIMA.

Viongozi wa upinzani nchini Kongo Brazzaville wameitisha maandamano ya nchi nzima kupinga kuchaguliwa tena Rais Denis Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 72.

Viongozi watano wa upinzani nchini humo walioshindwa katika uchaguzi rais wa Jumapili iliyopita akiwemo Guy-Brice Parfit Kolelas aliyeibuka wa pili kwa kupata asilimia 15 ya kura na Jean-Marie Mokoko ambaye alishika nafasi ya tatu kwa asilimia 14 wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya nchi nzima mnamo Machi 29, kulaani kile walichokitaja kuwa ‘wizi wa kura na utumizi mbaya wa mamlaka.’

Wamewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi katika kila mji kupigania kile walichokiita kuhujumiwa haki zao za kidemokrasia na kushinikiza kuheshimiwa katiba.

Tume ya Uchaguzi nchini Kongo Brazzaville ilimtangaza Denis Sasso Nguesso kuwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi wa Machi 20 kwa kupata asilimia 60 ya kura zote halali zilizopigwa.

Nguesso ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30, Oktoba mwaka jana alibadilisha katiba na kuondoa kipengee kinachoweka ukomo wa vipindi viwili kwa Rais na kujiandalia mazingira ya kubakia madarakani.

RAIS ASSAD ALIPONGEZA JESHI LA SYRIA KWA KUUKOMBOA MJI WA PALMYRA.

RAIS ASSAD ALIPONGEZA JESHI LA SYRIA KWA KUUKOMBOA MJI WA PALMYRA.

Rais Bashar al-Assad wa Syria amelipongeza jeshi la nchi hiyo kwa kuukomboa mji wa kihistoria wa Palmyra kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Rais Assad ameyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wabunge wa Ufaransa mjini Damascus na kuongeza kuwa, kukombolewa mji huo ni mafanikio makubwa sana kwa taifa la Syria na kunaonyesha namna jeshi la nchi hiyo likishirikiana na makundi ya wananchi linavyoendelea kupata mafanikio na kuzidi kukomboa miji mbali mbali ambayo ilikuwa chini ya udhibiti wa matakfiri wa Daesh.

Wakati huo huo, jeshi la Syria limesema kuwa, baada ya kuukomboa na kuudhibiti mji wa Palmyra, sasa linajiandaa kusonga mbele kwa ajili ya kuikomboa mikoa ya Raqqah na Deir al-Zawr. Kamandi Kuu ya jeshi la Syria imepongeza kukombolewa mji huo wa kihistoria na kusema kuwa, huu ndio mwanzo wa kuporomoka kwa harakati za kundi la kigaidi na kitaifiri la Daesh nchini humo.

Itakumbukwa kuwa, Juni mwaka jana 2015, wanachama wa kundi la kitakfiri la Daesh walibomoa makaburi mawili ya kale ya Mawalii wa Allah katika mji wa kihistoria wa Palmyra mkoani Homs nchini Syria. Mkurugenzi wa Turathi za Kale nchini Syria, Maamoun Abdulkarim, alisema kuwa magaidi hao wa kitakfiri walilipua mabomu ndani ya majengo ya makaburi ya Mohammad bin Ali wa kizazi cha binamu yake Mtume Muhammad SAW na Nizar Abu Bahaaeddine, msomi mtajika wa Kiislamu kutoka Palmyra.

MAJESHI YA SYRIA YAUTEKA MJI WA PALMYRA.

MAJESHI YA SYRIA YAUTEKA MJI WA PALMYRA.

Vyombo vya habari na vilevile wanaharakati huko Syria vinasema vikosi vya serikali vimekamata na kuchukua tena udhibiti wa mji wa kale wa Palmyra uliokuwa mikononi mwa wanamgambo wa IS.

Majeshi ya serikali ya Syria yamekuwa yakipiga hatua kuteka maeneo yanayokaliwa na wapinzani wao na vilevile yaliyokuwa yametekwa na IS tangu majeshi ya Urusi yalipoingia Syira kuisaidia serikali ya Bashar al Asaad kwa mashambulizi makali ya angani .

Shirika la kutetea haki za binadamu la Syrian Observatory for Human Rights limesema bado kuna milio ya ufyatulianaji risasi upande wa mashariki mwa mji huo lakini wengi wa wapiganaji wa IS wamefurushwa na kulazimika kurudi nyuma

Tangu IS wauteke mji wa Palmyra mwezi Mei mwaka uliopita wameharibu mengi ya maeneo ya kumbukumbu za zamani jambo lililokemewa na jamii ya kimataifa.

Ushindi huo wa majeshi ya Bashar al Assad ni pigo kwa harakati za waasi na vilevile ni ushindi kwa mbinu za Urusi dhidi ya serikali za kanda zinazowafadhili waasi.

Dotto Rangimoto Chamchua
0622845394/0784845394

KUKIMBIA HUKINGA WATU NA SARATANI.

Utafiti mpya waonesha kuwa kukimbia kweli kunasaidia kukinga saratani

Jarida la Cell Metabolism limetoa ripoti ya utafiti ikionesha kuwa kukimbia kunaweza kuinua kiwango cha mfumo wa kinga, kuzuia uvimbe mpya uibuke mwilini na kupunguza ukuaji wa seli za saratani kwa asilimia zaidi ya 50.

Mtaalamu kutoka chuo kikuu cha Copenhagen Dkt Pernille Hojman na timu yake ya utafiti waliwatumia panya wanaopata saratani kupima mchango wa mazoezi ya kukimbia katika saratani za aina tano ikiwemo saratani ya ini, ya mapafu na ya ngozi.

Katika jaribio, watafiti waliwagawanya panya kwa vikundi viwili, panya wa kikundi kimoja walikimbia kilomita 4 hadi 7 kila usika, na panya wengine hawakukimbia. Matokeo yalionesha kuwa panya waliokimbia kila siku walizuia kuibuka kwa uvimbe mpya, na ukuaji wa seli za saratani ulipungua kwa asilimia 60.

Dkt Hojman amesema, wamethibitisha kwa mara ya kwanza mazoezi ya kukimbia yanaweza kudhibiti moja kwa moja kasi ya ukuaji wa uvimbe. Watafiti wamegundua kuwa kukimbia kunahimiza uzalishaji wa epinephrine, ambayo inaweza kuchochea mfumo wa kinga kuzalisha seli ya NK inayoweza kukinga saratani.

Lakini Dkt Hojman ametambua kuwa kuhusu wagonjwa wa saratani, mazoezi ya kukimbia bado yanahitaji utafiti mwingi zaidi kuthibitisha na si rahisi kujua wagonjwa wa saratani wanahitaji idadi gani ya mazoezi.

UFARANSA: MARUFUKU KUWEKA PICHA ZA WATOTO ZENU MTANDAONI.

UFARANSA: MARUFUKU KUWEKA PICHA ZA WATOTO ZENU MTANDAONI.

Je wajua mwanaKisima? Ngoja nikujuze sasa!

Wazazi wa Ufaransa wapigwa marufuku kuweka picha za watoto wao kwenye mitandao ya kijamii.

Ufaransa imeweka sheria mpya inayozuia wazazi kuweka picha za watoto wao kwenye mitandao ya kijamii bila idhini yao. Kwa mujibu wa sheria hiyo, kuweka picha ya mtoto kwenye mtandao wa kijamii ni kosa ambalo adhabu yake ni faini ya Euro elfu 45, au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja.

Polisi wa Ufaransa wana wasiwasi kuwa kuna uwezekano picha zinazowekwa kwenye mitandao ya kijamii zikatumiwa na wahalifu na kuwaathiri watoto.

Na watoto wengine huwa wanataka wazazi wao waheshimu faragha zao, na hawataki picha ziwekwe kwenye social media. Je, uliwahi kuweka picha ya mtoto wako kwenye mtandao wa jamii? Uamuzi wa wafaransa unafaa au umevuka mipaka na kuingilia wajibu na majukumu ya mzazi?

JESHI LA SOMALIA LIMEWAUWA ALSHABABI 60.

JESHI LA SOMALIA LIMEWAUWA ALSHABABI 60.

Jeshi la Serikali nchini Somalia limewauwa wanamgambo 60 wa kundi la kigaidi la Al- Shabaab na kuwakamata wengine 38 katika Somalia ya kati.
Hayo ni kwa mujibu wa Rais wa askari wa Galmudug Abdikarim Hussein Guled.

Guled amesema kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab wamepata kipigo kikubwa katika mikono ya vikosi vya Galmudug na aliapa kuendeleza mashambulizi dhidi ya wanamgambo hao mpaka waondolewe kutoka jimbo lote la Galmudug.