RAIS ASSAD ALIPONGEZA JESHI LA SYRIA KWA KUUKOMBOA MJI WA PALMYRA.

RAIS ASSAD ALIPONGEZA JESHI LA SYRIA KWA KUUKOMBOA MJI WA PALMYRA.

Rais Bashar al-Assad wa Syria amelipongeza jeshi la nchi hiyo kwa kuukomboa mji wa kihistoria wa Palmyra kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Rais Assad ameyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wabunge wa Ufaransa mjini Damascus na kuongeza kuwa, kukombolewa mji huo ni mafanikio makubwa sana kwa taifa la Syria na kunaonyesha namna jeshi la nchi hiyo likishirikiana na makundi ya wananchi linavyoendelea kupata mafanikio na kuzidi kukomboa miji mbali mbali ambayo ilikuwa chini ya udhibiti wa matakfiri wa Daesh.

Wakati huo huo, jeshi la Syria limesema kuwa, baada ya kuukomboa na kuudhibiti mji wa Palmyra, sasa linajiandaa kusonga mbele kwa ajili ya kuikomboa mikoa ya Raqqah na Deir al-Zawr. Kamandi Kuu ya jeshi la Syria imepongeza kukombolewa mji huo wa kihistoria na kusema kuwa, huu ndio mwanzo wa kuporomoka kwa harakati za kundi la kigaidi na kitaifiri la Daesh nchini humo.

Itakumbukwa kuwa, Juni mwaka jana 2015, wanachama wa kundi la kitakfiri la Daesh walibomoa makaburi mawili ya kale ya Mawalii wa Allah katika mji wa kihistoria wa Palmyra mkoani Homs nchini Syria. Mkurugenzi wa Turathi za Kale nchini Syria, Maamoun Abdulkarim, alisema kuwa magaidi hao wa kitakfiri walilipua mabomu ndani ya majengo ya makaburi ya Mohammad bin Ali wa kizazi cha binamu yake Mtume Muhammad SAW na Nizar Abu Bahaaeddine, msomi mtajika wa Kiislamu kutoka Palmyra.