RWANDA: HATUJA WATIMUA WAKIMBIZI.


Serikali ya Rwanda imekanusha madai kwamba, imewafukuza kutoka nchini humo wakimbizi kutoka Burundi.

Taarifa ya serikali ya Rwanda imesisitiza kwamba, haijawafukuza wakimbizi kutoka Burundi na kwamba wanaofukuzwa kutoka nchini humo ni raia wa Burundi wasio na vibali vya kuishi nchini humo.

Gavana wa jimbo la kusini mwa Rwanda ambako zaidi ya raia 1000 kutoka Burundi wamekwishatimuliwa ameziambia duru za habari kwamba, wanaofukuzwa walitakiwa kupata vibali vya kuendelea kuishi nchini humo na kisha warejee ikiwa watapenda.

Hivi karibuni Gavana wa mji wa Kirundo wa Burundi ambao uko katika mpaka wa nchi hiyo na Rwanda alisema kuwa, Rwanda imewatimia wakimbizi 1,300 wa Burundi ambao walitakiwa kurejea katika kambi za wakimbizi au kuondoka nchini humo. Melchior Nankwahomba alisema wale waliokataa kwenda katika kambi za wakimbizi walikuwa wakiondolewa kwa nguvu na maafisa wa Rwanda.

Makumi kwa maelfu ya Warundi walikimbilia Rwanda tangu ghasia zilipoanza nchini mwao mwaka mmoja uliopita, kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa kuwania Urais kwa muhula wa tatu mfululizo hatua ambayo ililalamikiwa na wapinzani waliosema ilikiuka katiba na makubaliano ya amani ya Arusha Tanzania.

Burundi imekuwa ikiituhumu Rwanda kwamba, inaingilia masuala yake ya ndani, madai ambayo yanakanushwa na serikali ya Kigali.

KENYA YAPATA PIGO LINGINE, BAADA YA BOMBA LA MAFUTA, SASA RELI.


Rwanda imetangaza kuwa itajenga njia ya reli ya kisasa aina ya SGR kupitia Tanzania badala ya Kenya ikisema kuwa njia ya Tanzania itahitaji bajeti ya chini ikilinganishwa na Kenya.

Akihutubia waandishi wa habari hapo jana, waziri wa fedha wa Rwanda Claver Gatete, aliongeza kuwa itachukua muda kidogo kujenga reli hiyo kupitia Tanzania badala ya Kenya.

Utafiti uliofanywa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeonyesha kuwa njia ya Tanzania itagharimu Rwanda kati ya dola milioni 800-900 huku njia ya Kenya ikigharimu dola bilioni moja. Njia hiyo ya reli itakayotoka Dar es Salaam-Isaka-Kigali/Keza-Musongati (DIKKM) itakamilishwa mwaka wa 2018 na inatarajiwa kugharimu nchi husika jumla ya dola bilioni 5.2.

KISO CHAKO HUKISHIKI

Ufanye uende mbio, kaskazi mashariki,
Ubebe na kuku kwio, kwa ndumba unihiliki,
Yote yawa kifagio, kwa uwezo wa Maliki,
Jalali sio babio, elewa sihadhiriki.
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Mja kalisha kalio, hazina pato shiriki,
Fanya uweke fungio, huta zuia riziki
Waja angua kilio, useme na hizo chuki,
Mola wangu kimbilio, wallahi sifedheheki,
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Nimegundua mwenzio, tabasamu lako feki,
Watia kinukajio, kwa chips na mishikaki,
Umepaka kipambio, sumu nipate fariki,
Rabi kahuluku "sio" ndio mana sianguki
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Ulo nalo kusudio, fahamu halisomeki,
Uweke na kikingio, kiso chako hukishiki,
Ingia kwa kitubio, umrudie Razaki,
Jalali kaumba "ndio" kwahivyo sitetereki.
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Wanisema kwa wenzio, vile isivyo stahiki,
Mithili ya kisusio, mdomoni sikutoki,
Neno mwenziwe sikio, halichomi si mkuki,
Mungu tanipa tulio, hakika sibabaiki.
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Umeshika mchinjio, na bado haushutuki,
Chakughuri kilalio, kiumbe hauzinduki,
Punguza matamanio, dunia haibebeki,
Rabi nipe kifutio, nifute zako falaki
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Alokupa mtwangio, na kinu simdhihaki,
Kuna siku ya chungio, kiumbe huiepuki,
Hivyo situpe dekio, kesho haitabiriki,
Hapa pana zingatio, wajibu nduguye haki,
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
0622845394 Morogoro

ISRAELI YAFANYA MASHAMBULIZI UKANDA WA GAZA.


Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kwa kushirikiana walowezi wa Kizayuni wenye chuki za kidini na kitaifa, wamefanya mashambulizi katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya Wapalestina.

Shirika la habari la WAFA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walioko katika mpaka unaotenganisha Ukanda wa Ghaza na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, leo asubuhi wamevunja makubaliano ya kusimamisha vita kwa kuwashambulia wakulima wa Kipalestina, mashariki mwa Khan Yunus na kusini mwa eneo hilo, na kuwazuia kuingia kwenye mashamba yao.

Aidha leo asubuhi, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wamewashambulia kwa risasi wakulima wa Kipalestina mashariki mwa eneo la al Shujaiyya, katika Ukanda wa Ghaza.

Hadi sasa hakuna habari zozote zilizotangazwa kuhusu hasara iliyosababishwa na mashambulizi hayo ambayo ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusimamisha vita.

Wakati huo huo walowezi wa Kizayuni leo wamezivamia nyumba za Wapalestina katika mji wa al Khalil wa kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Licha ya walowezi hao wa Kizayuni kusaidiwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika uvamizi huo, lakini Wapalestina wamesimama kidete kukabiliana nao, jambo ambalo limezusha mapigano baina ya pande hizo mbili.

WANANCHI WA YEMEN WASISITIZA KUPAMBANA NA MAREKANI.


Imam wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa jana huko San'a, mji mkuu wa Yemen amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wataendelea kusimama kidete kupambana na wavamizi wa nchi yao.

Televisheni ya al Maseera ya Yemen imetangaza habari hiyo leo Jumamosi na kumnukuu Sheikh Abdul Majid al Houthi akiwaonya wanajeshi wa Marekani walioivamia ardhi ya Yemen kwamba wananchi wa nchi hiyo kamwe hawataruhusu hata shibri moja ya ardhi ya nchi yao ikaliwe na wavamizi.

Imam wa Sala ya Ijumaa ya San'a ameongeza kuwa, Marekani ina lengo la kuigawa vipande vipande nchi ya Yemen, lakini wananchi wa nchi hiyo wataendelea kuwa kitu kimoja mbele ya njema za Marekani.

Siku chache zilizopita, duru za habari za Yemen zilitangaza habari ya kuingia helikopta 15 aina ya Apache na helikopta 5 aina ya Black Hawk za jeshi la Marekani katika kambi ya jeshi la anga ya al Anad, kusini mwa Yemen.

Siku ya Jumamosi ya wiki iliyopita pia, wanajeshi 200 wa Marekani waliingia katika Ghuba ya Aden sambamba na kuwasili manowari ya kivita ya Marekani katika ghuba hiyo.

Imam wa Sala ya Ijumaa ya mjini San'a amesema, uvamizi huo wa Wamarekani nchini Yemen ulitabiriwa tangu zamani na wananchi wa nchi hiyo na ndio maana kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa waendelea kukabiliana na wavamizi wa nchi yao.

BODABODA WANNE WAFA KWENYE MAANDAMANO HUKO CONGO DRC


Watu wanne wameripotiwa kuuawa katika maandamano ya waendesha pikipiki dhidi ya askari wa barabarani, huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Maandamano hayo yaliyoitishwa kwa ajili ya kulalamikia miamala mibaya ya polisi wa barabarani, yalifanyika katika barabara kuu ya eneo la Mambasa katika mkoa wa Orientale, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Waandamanaji hao wanawatuhumu polisi kwamba wanachukua kiasi kikubwa cha fedha sawa na faranka 2000 kwa pikipiki moja ili kuruhusiwa kupita kwenye moja ya vizuizi kwenye eneo hilo, kiwango ambacho wanadai ni kikubwa kulingana na kipato chao.

Aidha madereva hao wa pikipiki (maarufu kama bodaboda) wametaka pia kuachiliwa huru pikipiki kadhaa ambazo zinashikiliwa na jeshi hilo la polisi wa barabarani katika eneo hilo. Katika kumaliza maandamano hayo, polisi hao wa barabarani walifyatua risasi kuwalenga waandamanji. Kiongozi wa eneo hilo la Mambasa, Alfred Bongwalanga amethibitisha kutokea machafuko hayo na watu wanne kuuawa.

Bongwalanga amesema kuwa, zaidi ya madereva 500 wa pikipiki walishiriki katika maandamano hayo. Baadhi ya vyombo vya habari vimesema kwamba, kulikuwa kumeshuhudiwa moto kwenye kituo kimoja cha polisi, kabla ya polisi kudhibiti eneo la PK51 katika mji huo wa Mambasa.

RWANDA YAKANUSHA KUHUSIKA NA MACHAFUKO YANAYO ENDELEA BURUNDI.

Serikali ya Rwanda imetoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma dhidi yake kwamba, imekuwa ikichochea machafuko katika nchi jirani ya burundi.

Rais Paul Kagame wa Rwanda amekanusha madai dhidi ya nchi yake kwamba, inawasaidia waasi wa Burundi kama ilivyokuja katika ripoti ya siri iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Kagame amesisitiza kuwa, nchi yake haiwasaidii kwa namna yoyote ile waasi wa Burundi au kuhusika na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo jirani. Rais Kagame amebainisha kwamba, machafuko ya ndani nchini Burundi chimbuko lake ni masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Imeelezwa katika ripoti ya siri iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia waasi wa Burundi wanaotaka kuiangusha serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Ripoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inaeleza kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia kifedha, kimafunzo na hata kilojistiki waasi hao wanaopigana dhidi ya serikali ya Bujumbura.

Imeelezwa kuwa, Rwanda inafanya hivyo ili kuiondoa madarakani serikali ya Rais Nkurunziza.

Lambert Mende Omalanga ambaye ni msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia anaamini kuwa, serikali ya Rwanda imewapatia fedha waasi wa Rais Joseph Kabila ili kuwaimarisha.

Mende Omalanga amesema kuwa, Rwanda imekuwa ikiwapatia fedha wanachama wa kundi la zamani la waasi wa M23 ambao walisambaratishwa Novemba mwaka 2013 na kwa sasa baadhi yao wanaishi uhamishoni katika nchi za Rwanda na Uganda.

Ripoti ya siri ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyopelekwa katika Baraza la Usalama imefichua kwamba, waasi wa Burundi walioko mashariki mwa DRC wamekiri kwamba, katikati mwa mwaka jana walipatiwa mafunzo na watoaji mafunzo ambao baadhi yao walikuwa ni wanajeshi wa Rwanda.

Ripoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inakinzana na matamshi ya hivi karibuni ya viongozi wa Magharibi. Viongozi hao walidai kwamba, serikali ya Rwanda ilisimamisha himaya yake kwa waasi wa Burundi tangu mwaka jana.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, wameipatia serikali ya Rwanda ushahidi unaoonesha juu ya kuweko ushirikiano wa siri kati yake na waasi wa Burundi na wa Congo DR. Aidha serikali ya Burundi ikishirikiana na jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kuwa, ina nyaraka zinaoonesha juu ya kuweko harakati za siri za Shirika la Kiintelijensia la Rwanda. Pamoja na hayo serikali ya Rwanda imeendelea kukana kuhusika kwa namna yoyote ile na machafuko ya jirani yake Burundi.

Burundi ilitumbukia katika rangaito na mchafukoge Aprili mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuidhinishwa na chama chake cha CNDD-FDD kuwania kiti cha Urais kwa mara ya tatu mfululizo.

Licha ya kuweko upinzani wa asasi za kiraia nchini Burundi na hata za kieneo na kimataifa, Nkurunziza alishiriki katika uchaguzi huo na kuibuka na ushindi na hivyo kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.

Kuendelea upinzani na maandamano kuliibua machafuko katika jiji la Bujumbura na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo.

Takwimu zinaonesha kuwa, watu 500 wameuawa na wengine karibu laki mbili na 60 elfu wamekuwa wakimbizi tangu nchi hiyo ilipotumbukia katika machafuko hayo.

Katika kipindi chote hiki tangu Burundi itumbukie katika mgogoro wa kisiasa, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakitoa indhari mara chungu nzima juu ya hatari ya nchi hiyo kutumbukia katika vita vya ndani na vya mauaji ya kimbari.

Katika mazingira kama haya ya kutia wasiwasi, himaya ya kifedha na kijeshi kwa makundi yanayofanya fujo nchini Burundi au katika nchi jirani ni sawa na kumwagia mafuta ya petroli moto unaowaka.

AMNESTY YATAKA UGANDA IMKAMATE RAIS OMAR AL BASHIR.


Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameitaka serikali ya Uganda kumkamata Rais Omar al-Bashir wa Sudan na kumkabidhi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kwa tuhuma za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yameitaka serikali ya Uganda kutekeleza wajibu wake wa kimataifa na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC, Rais wa Sudan ambaye alienda mjini Kampala kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais Yoweri Museveni.

Muthoni Wanyeki, Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na eneo la Maziwa Makuu amesema Uganda ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na hivyo, iwapo itafeli kumkabidhi Rais wa Sudan, itakuwa imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, baada ya kula kiapo hapo jana, Rais Museveni aliikashifu ICC na kusema kuwa mahakama hiyo imegeuka na kuwa chombo cha kuwadhalilisha viongozi wa Kiafrika huku ikiwasaza viongozi makatili wa nchi za Magharibi. Kauli ya Museveni iliwaghadhabisha wajumbe wa Marekani na Umoja wa Ulaya waliokuwa wamehudhuria sherehe za kuapishwa kwake katika Viwanja vya Kololo jijini Kampala na kuwafanya kuondoka kwenye hafla hiyo.

Itakumbukwa kuwa, serikali ya Afrika Kusini ilikataa kumkamata Rais Omar al-Bashir ambaye alishiriki mkutano wa viongozi wa Afrika uliofanyika mjini Johannesburg Julai mwaka jana. Aidha Kenya ilipuuza wito wa kumkamata na kumkabidhi kiongozi huyo kwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ICC anakotakiwa kujibu tuhuma za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu; alipohudhuria sherehe za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki mwaka 2013.

HIZBULLAH YACHUNGUZA KIFO CHA KAMANDA WAKE.


Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah imesema imeanzisha uchunguzi kubaini namna kamanda wake mwandamizi alivyouawa katika kile kilichotajwa kuwa hujuma ya jeshi la utawala wa Israel.

Taarifa ya Hizbullah imesema kuwa, harakati hiyo imeanzisha uchunguzi kubaini iwapo Mustafa Badruddin aliuawa katika hujuma ya anga ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika moja ya kambi za harakati hiyo karibu na uwanja wa ndege wa Damascus au la.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, uchunguzi wao unalenga kujua iwapo kamanda huyo mwandamizi aliuawa katika shambulizi la kombora au roketi, baada ya sauti kubwa ya kishindo kusikika jana katika kambi hiyo.

Ripoti za awali zilikua zimearifu kuwa Mustafa Badruddin, kamanda mwandamizi wa Hizbullah ya Lebanon aliuawa katika hujuma ya anga ya ndege ya utawala wa Israel.

Badruddin mwenye umri wa miaka 55 na ambaye alikua mkuu wa tawi la kijeshi la Harakati ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah, alikuwa akiongoza kikosi kinachoisaidia serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria kupambana na makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Kamanda huyo ambaye pia alikua mshauri wa Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah na mkuu wa kitengo cha kiintelijensia, alikua binamu ya Imad Mughniyah, kamanda mwandamizi wa zamani wa Hizbullah ambaye aliuawa na kitengo cha ujasusi cha utawala wa Israe Mossad, mwaka 2008 katika mji mkuu wa Syria.