ISRAELI YAFANYA MASHAMBULIZI UKANDA WA GAZA.


Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kwa kushirikiana walowezi wa Kizayuni wenye chuki za kidini na kitaifa, wamefanya mashambulizi katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya Wapalestina.

Shirika la habari la WAFA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walioko katika mpaka unaotenganisha Ukanda wa Ghaza na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, leo asubuhi wamevunja makubaliano ya kusimamisha vita kwa kuwashambulia wakulima wa Kipalestina, mashariki mwa Khan Yunus na kusini mwa eneo hilo, na kuwazuia kuingia kwenye mashamba yao.

Aidha leo asubuhi, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wamewashambulia kwa risasi wakulima wa Kipalestina mashariki mwa eneo la al Shujaiyya, katika Ukanda wa Ghaza.

Hadi sasa hakuna habari zozote zilizotangazwa kuhusu hasara iliyosababishwa na mashambulizi hayo ambayo ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusimamisha vita.

Wakati huo huo walowezi wa Kizayuni leo wamezivamia nyumba za Wapalestina katika mji wa al Khalil wa kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Licha ya walowezi hao wa Kizayuni kusaidiwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika uvamizi huo, lakini Wapalestina wamesimama kidete kukabiliana nao, jambo ambalo limezusha mapigano baina ya pande hizo mbili.

WANANCHI WA YEMEN WASISITIZA KUPAMBANA NA MAREKANI.


Imam wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa jana huko San'a, mji mkuu wa Yemen amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wataendelea kusimama kidete kupambana na wavamizi wa nchi yao.

Televisheni ya al Maseera ya Yemen imetangaza habari hiyo leo Jumamosi na kumnukuu Sheikh Abdul Majid al Houthi akiwaonya wanajeshi wa Marekani walioivamia ardhi ya Yemen kwamba wananchi wa nchi hiyo kamwe hawataruhusu hata shibri moja ya ardhi ya nchi yao ikaliwe na wavamizi.

Imam wa Sala ya Ijumaa ya San'a ameongeza kuwa, Marekani ina lengo la kuigawa vipande vipande nchi ya Yemen, lakini wananchi wa nchi hiyo wataendelea kuwa kitu kimoja mbele ya njema za Marekani.

Siku chache zilizopita, duru za habari za Yemen zilitangaza habari ya kuingia helikopta 15 aina ya Apache na helikopta 5 aina ya Black Hawk za jeshi la Marekani katika kambi ya jeshi la anga ya al Anad, kusini mwa Yemen.

Siku ya Jumamosi ya wiki iliyopita pia, wanajeshi 200 wa Marekani waliingia katika Ghuba ya Aden sambamba na kuwasili manowari ya kivita ya Marekani katika ghuba hiyo.

Imam wa Sala ya Ijumaa ya mjini San'a amesema, uvamizi huo wa Wamarekani nchini Yemen ulitabiriwa tangu zamani na wananchi wa nchi hiyo na ndio maana kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa waendelea kukabiliana na wavamizi wa nchi yao.

BODABODA WANNE WAFA KWENYE MAANDAMANO HUKO CONGO DRC


Watu wanne wameripotiwa kuuawa katika maandamano ya waendesha pikipiki dhidi ya askari wa barabarani, huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Maandamano hayo yaliyoitishwa kwa ajili ya kulalamikia miamala mibaya ya polisi wa barabarani, yalifanyika katika barabara kuu ya eneo la Mambasa katika mkoa wa Orientale, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Waandamanaji hao wanawatuhumu polisi kwamba wanachukua kiasi kikubwa cha fedha sawa na faranka 2000 kwa pikipiki moja ili kuruhusiwa kupita kwenye moja ya vizuizi kwenye eneo hilo, kiwango ambacho wanadai ni kikubwa kulingana na kipato chao.

Aidha madereva hao wa pikipiki (maarufu kama bodaboda) wametaka pia kuachiliwa huru pikipiki kadhaa ambazo zinashikiliwa na jeshi hilo la polisi wa barabarani katika eneo hilo. Katika kumaliza maandamano hayo, polisi hao wa barabarani walifyatua risasi kuwalenga waandamanji. Kiongozi wa eneo hilo la Mambasa, Alfred Bongwalanga amethibitisha kutokea machafuko hayo na watu wanne kuuawa.

Bongwalanga amesema kuwa, zaidi ya madereva 500 wa pikipiki walishiriki katika maandamano hayo. Baadhi ya vyombo vya habari vimesema kwamba, kulikuwa kumeshuhudiwa moto kwenye kituo kimoja cha polisi, kabla ya polisi kudhibiti eneo la PK51 katika mji huo wa Mambasa.

RWANDA YAKANUSHA KUHUSIKA NA MACHAFUKO YANAYO ENDELEA BURUNDI.

Serikali ya Rwanda imetoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma dhidi yake kwamba, imekuwa ikichochea machafuko katika nchi jirani ya burundi.

Rais Paul Kagame wa Rwanda amekanusha madai dhidi ya nchi yake kwamba, inawasaidia waasi wa Burundi kama ilivyokuja katika ripoti ya siri iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Kagame amesisitiza kuwa, nchi yake haiwasaidii kwa namna yoyote ile waasi wa Burundi au kuhusika na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo jirani. Rais Kagame amebainisha kwamba, machafuko ya ndani nchini Burundi chimbuko lake ni masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Imeelezwa katika ripoti ya siri iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia waasi wa Burundi wanaotaka kuiangusha serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Ripoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inaeleza kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia kifedha, kimafunzo na hata kilojistiki waasi hao wanaopigana dhidi ya serikali ya Bujumbura.

Imeelezwa kuwa, Rwanda inafanya hivyo ili kuiondoa madarakani serikali ya Rais Nkurunziza.

Lambert Mende Omalanga ambaye ni msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia anaamini kuwa, serikali ya Rwanda imewapatia fedha waasi wa Rais Joseph Kabila ili kuwaimarisha.

Mende Omalanga amesema kuwa, Rwanda imekuwa ikiwapatia fedha wanachama wa kundi la zamani la waasi wa M23 ambao walisambaratishwa Novemba mwaka 2013 na kwa sasa baadhi yao wanaishi uhamishoni katika nchi za Rwanda na Uganda.

Ripoti ya siri ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyopelekwa katika Baraza la Usalama imefichua kwamba, waasi wa Burundi walioko mashariki mwa DRC wamekiri kwamba, katikati mwa mwaka jana walipatiwa mafunzo na watoaji mafunzo ambao baadhi yao walikuwa ni wanajeshi wa Rwanda.

Ripoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inakinzana na matamshi ya hivi karibuni ya viongozi wa Magharibi. Viongozi hao walidai kwamba, serikali ya Rwanda ilisimamisha himaya yake kwa waasi wa Burundi tangu mwaka jana.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, wameipatia serikali ya Rwanda ushahidi unaoonesha juu ya kuweko ushirikiano wa siri kati yake na waasi wa Burundi na wa Congo DR. Aidha serikali ya Burundi ikishirikiana na jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kuwa, ina nyaraka zinaoonesha juu ya kuweko harakati za siri za Shirika la Kiintelijensia la Rwanda. Pamoja na hayo serikali ya Rwanda imeendelea kukana kuhusika kwa namna yoyote ile na machafuko ya jirani yake Burundi.

Burundi ilitumbukia katika rangaito na mchafukoge Aprili mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuidhinishwa na chama chake cha CNDD-FDD kuwania kiti cha Urais kwa mara ya tatu mfululizo.

Licha ya kuweko upinzani wa asasi za kiraia nchini Burundi na hata za kieneo na kimataifa, Nkurunziza alishiriki katika uchaguzi huo na kuibuka na ushindi na hivyo kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.

Kuendelea upinzani na maandamano kuliibua machafuko katika jiji la Bujumbura na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo.

Takwimu zinaonesha kuwa, watu 500 wameuawa na wengine karibu laki mbili na 60 elfu wamekuwa wakimbizi tangu nchi hiyo ilipotumbukia katika machafuko hayo.

Katika kipindi chote hiki tangu Burundi itumbukie katika mgogoro wa kisiasa, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakitoa indhari mara chungu nzima juu ya hatari ya nchi hiyo kutumbukia katika vita vya ndani na vya mauaji ya kimbari.

Katika mazingira kama haya ya kutia wasiwasi, himaya ya kifedha na kijeshi kwa makundi yanayofanya fujo nchini Burundi au katika nchi jirani ni sawa na kumwagia mafuta ya petroli moto unaowaka.

AMNESTY YATAKA UGANDA IMKAMATE RAIS OMAR AL BASHIR.


Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameitaka serikali ya Uganda kumkamata Rais Omar al-Bashir wa Sudan na kumkabidhi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kwa tuhuma za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yameitaka serikali ya Uganda kutekeleza wajibu wake wa kimataifa na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC, Rais wa Sudan ambaye alienda mjini Kampala kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais Yoweri Museveni.

Muthoni Wanyeki, Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na eneo la Maziwa Makuu amesema Uganda ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na hivyo, iwapo itafeli kumkabidhi Rais wa Sudan, itakuwa imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, baada ya kula kiapo hapo jana, Rais Museveni aliikashifu ICC na kusema kuwa mahakama hiyo imegeuka na kuwa chombo cha kuwadhalilisha viongozi wa Kiafrika huku ikiwasaza viongozi makatili wa nchi za Magharibi. Kauli ya Museveni iliwaghadhabisha wajumbe wa Marekani na Umoja wa Ulaya waliokuwa wamehudhuria sherehe za kuapishwa kwake katika Viwanja vya Kololo jijini Kampala na kuwafanya kuondoka kwenye hafla hiyo.

Itakumbukwa kuwa, serikali ya Afrika Kusini ilikataa kumkamata Rais Omar al-Bashir ambaye alishiriki mkutano wa viongozi wa Afrika uliofanyika mjini Johannesburg Julai mwaka jana. Aidha Kenya ilipuuza wito wa kumkamata na kumkabidhi kiongozi huyo kwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ICC anakotakiwa kujibu tuhuma za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu; alipohudhuria sherehe za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki mwaka 2013.

HIZBULLAH YACHUNGUZA KIFO CHA KAMANDA WAKE.


Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah imesema imeanzisha uchunguzi kubaini namna kamanda wake mwandamizi alivyouawa katika kile kilichotajwa kuwa hujuma ya jeshi la utawala wa Israel.

Taarifa ya Hizbullah imesema kuwa, harakati hiyo imeanzisha uchunguzi kubaini iwapo Mustafa Badruddin aliuawa katika hujuma ya anga ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika moja ya kambi za harakati hiyo karibu na uwanja wa ndege wa Damascus au la.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, uchunguzi wao unalenga kujua iwapo kamanda huyo mwandamizi aliuawa katika shambulizi la kombora au roketi, baada ya sauti kubwa ya kishindo kusikika jana katika kambi hiyo.

Ripoti za awali zilikua zimearifu kuwa Mustafa Badruddin, kamanda mwandamizi wa Hizbullah ya Lebanon aliuawa katika hujuma ya anga ya ndege ya utawala wa Israel.

Badruddin mwenye umri wa miaka 55 na ambaye alikua mkuu wa tawi la kijeshi la Harakati ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah, alikuwa akiongoza kikosi kinachoisaidia serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria kupambana na makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Kamanda huyo ambaye pia alikua mshauri wa Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah na mkuu wa kitengo cha kiintelijensia, alikua binamu ya Imad Mughniyah, kamanda mwandamizi wa zamani wa Hizbullah ambaye aliuawa na kitengo cha ujasusi cha utawala wa Israe Mossad, mwaka 2008 katika mji mkuu wa Syria.

MAGAID WA DAESH WAUA WANAJESHI 17 WA IRAQ.


Takriban askari 17 wa jeshi la Iraq wameuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi  la Daesh katika mkoa wa Anbar, magharibi mwa nchi hiyo.

Duru za kijeshi zinaarifu kuwa, magaidi hao jana Alkhamisi walilishambulia kwa mabomu gari la kijeshi katika wilaya ya Jarayshi, yapata kilomita 10 kutoka Ramadi, makao makuu ya mkoa wa Anbar na kuua askari 17 wa jeshi la serikali.

Imearifiwa kuwa, lengo la hujuma hiyo ya magaidi wa Daesh ni kukata mawasiliano kati ya eneo la Ramadi na Tharthar, lililoko kilomita 120 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Baghdad ili kuwazuia wanajeshi wa Iraq kusonga mbele na kukomboa maeneo ambayo yanadhibitiwa na kundi hilo la kigaidi.

Aidha raia wawili waliuawa jana Alkhamisi katika hujuma tofauti ya kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la al-Obeidi, mashariki mwa Baghdad.

Hujuma za jana zimefanyika siku moja baada ya magaidi hao kutekeleza shambulizi jingine lililosababisha makumi ya watu kupoteza maisha.

Siku ya Jumatano, watu wasiopungua 64 waliuawa na wengine zaidi ya 85 kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea karibu na soko la Urayda katika kitongoji cha Sadr mashariki mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

RAIS WA GUINEA BISSAU AMFUTA KAZI WAZIRI MKUU.


Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amempiga kalamu Carlos Correia, Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kutangaza kuivunja serikali.

Akilihutubia taifa jana Alkhamisi, Rais Vaz alisema serikali ya Correia imeshindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliopo na kubuni taasisi zinazoendana na matakwa ya utawala wake.

Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amevitaka vyama vya siasa kushauriana na kumteua Waziri Mkuu mpya.

Correia alipewa jukumu la kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika mwezi Oktoba mwaka jana, akiwa ni kiongozi wa tatu kushikilia wadhifa huo ndani ya muda wa miezi mitatu. Correia kama wenzake wawili waliomtangulia, alitazamiwa na utawala wa Rais Vaz kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaotokota nchini humo unaodaiwa kuripuka kuanzia ndani ya chama tawala cha PAIGC.

Mapema mwezi Machi mwaka huu, Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioitembelea nchi hiyo kwa ajili ya kuchunguza hali ya mambo, umeyasema hayo wakati wa mazungumzo na Rais wa Guinea-Bissau, José Mário Vaz, Spika wa Bunge na viongozi wa vyama vya kisiasa.

Mgogoro wa kisiasa nchini Guinea-Bissau umekuwa mkubwa kiasi cha kufanya upatanishi wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kireno (CPLP) kushindwa kumaliza mivutano hiyo ya kisiasa

KAMANDA WA HEZBOLLAH AMEUAWA.

Kundi la wapiganaji la Hezbollah limesema kuwa kamanda wake wa juu,Mustafa Badreddine ameuawa katika shambulio la anga la Israel nchini Syria,Vyombo vya habari vimeripoti.Mustafa Badreddine anadaiwa kuhusika na mauaji ya Waziri mkuu wa Israel Rafiq Hariri mwaka wa 2005.