WHO: %80 YA WAKAZI WA MJINI WANAVUTA HEWA CHAFU.

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonya kuwa hali ya uchafuzi wa hewa inazidi kuwa mbaya duniani kote huku zaidi ya asilimia 80 ya wakaazi wa miji mikubwa wakivuta hewa chafu na kuongeza hatari ya kupatwa na saratani ya mapafu na maradhi mengine hatari.

Ripoti hiyo ya WHO imebainisha kuwa wakaazi wa mijini katika nchi masikini ndio wanaoathiriwa zaidi na kufafanua kwamba ni asilimia mbili tu ya miji katika nchi za kipato cha chini na cha kati ambayo watu wake wanavuta hewa inayokidhi viwango vya shirika hilo la kimataifa la afya. Kiwango hicho ni asilimia 44 katika miji ya nchi tajiri.

Ripoti ya Shirika Afya Duniani imezingatia utafiti iliofanya katika miji 795 ya nchi 67 katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 hadi 2015.

Kwa kuzingatia kiwango cha mada zenye madhara kama sulfeti na kaboni nyeusi, WHO imegundua kuwa hewa inachafuka zaidi katika maeneo ya nchi zinazoendelea hususan katika Mashariki ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia.

Utafiti huo wa shirika la Afya Duniani umeonesha kuwa India ina miji 15 kati ya 30 duniani yenye hewa chafu zaidi.

Mji wa Zabol ulioko mashariki mwa Iran ndio wenye hewa chafu zaidi ukifuatiwa na miji ya Gwalior na Allahabad ya India na Riyadh na Jubail ya Saudi Arabia

MUUAJI WA MTU MWEUSI APIGA MNADA SILAHA YAKE.

George Zimmerman, muuaji wa Trayvon Martin, kijana wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika ametangaza kuwa anaipiga mnada kwenye mtandao wa intaneti silaha aliyomuulia kijana huyo.

Zimmerman, mlinzi wa kizungu ambaye tarehe 16 Februari mwaka 2012 alimpiga risasi na kumuua Trayvon Martin pasina kuwa na silaha yoyote na kisha akafutiwa shtaka hilo hivi sasa ameamua kuipiga mnada silaha yake hiyo.

Kwa mujibu wa Zimmerman mwenyewe, silaha hiyo amerejeshewa na Wizara ya Sheria ya Marekani ambayo iliichukua kutoka kwake wakati kesi yake ilipokuwa ikiendelea na baada ya kufutiwa mashtaka.

Mnada wa kuiuza silaha hiyo umeanza jana Alhamisi na bei ya kuanzia imetajwa kuwa ni dola elfu tano.

Mauaji ya Trayvon Martin ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17 na hatimaye kufutiwa mashtaka George Zimmerman kulizusha wimbi kubwa la machafuko na malalamiko katika kila pembe ya Marekani; na maandamano makubwa yakafanyika nchini humo na katika baadhi ya nchi za kigeni kulalamikia ubaguzi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

SOMALIA YAKOSOA MPANGO WA KENYA KUFUNGA KAMBI ZA DADAAB.

Serikali ya Somalia imekosoa azma ya Kenya ya kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab yenye mamia ya maelfu ya wakimbizi na haswa raia wa Kisomali.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema kufungwa kwa kambi hiyo hakutakua na tija nyingine ghairi ya kuwasukuma wakimbizi hao kujiunga na makundi ya kigaidi kama vile al-Shabab. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kuwatimua wakimbizi hao wakati huu ambapo nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iko mbioni kuhakikisha kuwa inarejesha usalama, uthabiti na kuimarisha taasisi zake, kutayumbisha zaidi usalama wa kanda hiyo. Kambi ya Dadaab ina wakimbizi wapatao 350,000, aghalabu yao wakiwa ni raia wa Kisomali.

Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kuitaka serikali ya Kenya kufikiria upya mpango wake wa kufunga kambi hiyo huku ukisisitza kuwa, usalama wa maelfu ya wakimbizi wa Kisomali na raia wa Sudan Kusini kwa takriban robo karne umekuwa ukitegemea ukarimu wa Kenya na nia yake ya kutaka kuonyesha mfano bora katika eneo wa kutekeleza wajibu wake wa kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF nalo limetoa taarifa likisema kuwa, kutekelezwa kwa uamuzi huo kutawaweka maelfu ya wakimbizi hatarini. Licha ya mashirika mbalimbali ya kimataifa kuendelea kuitaka Kenya ifikirie upya uamuzi wake wa kutaka kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab, serikali ya Nairobi imesisitiza kwamba, inalazimika kuifunga kambi hiyo ya wakimbizi kutokana na mzigo mzito wa kiusalama, kiuchumi na masuala ya kimazingira.

UN YAITAKA SUDAN KUSINI KUFUATILIA JINAI ZA NGONO.

Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ukatili wa Kingono Katika Migogoro ameutaka uongozi mkuu wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya Sudan Kusini utekeleze ahadi ulizotoa za kufuatilia jinai za ukatili wa kingono zilizofanywa nchini humo.

Akikamilisha safari yake ya siku nne mjini Juba hapo jana, Zainab Hawa Bangura, ameeleza mbele ya waandishi wa habari kuwa kutekelezwa kwa mafanikio makubaliano ya amani kutahitaji kuhakikisha kuwa jinai za ukatili wa kingono zinafuatiliwa, kufahamika na kuripotiwa na kushughulikiwa katika vyombo vyote vya sheria vya serikali ya mpito.

Mwakilishi huyo Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ukatili wa Kingono Katika Migogoro amebainisha kuwa ahadi hizo zimo kwenye taarifa ya pamoja ambayo waliisaini yeye na Rais Salva Kiir Oktoba 11 mwaka 2014 na pia kwenye taarifa ya upande mmoja iliyotolewa Desemba 18 mwaka 2014 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa hivi sasa wa nchi hiyo Riek Machar.

Bi Bangura amesisitiza kuwa licha ya ahadi hizo na hatua zilizopigwa katika utekelezaji lakini jinai za ukatili wa kingono zimeendelea kufanywa katika muktadha wa mgogoro wa nchi hiyo.

Katika safari yake ya siku nne nchini Sudan Kusini iliyotokana na mwaliko wa serikali ya Juba, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ukatili wa Kingono Katika Migogoro amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Salva Kiir, Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar na maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. Bi Zainab Hawa Bangura amefanya mazungumzo pia na makundi ya wanawake yanayotoa huduma kwa manusura wa ukatili wa kingono, jumuiya ya utoaji huduma za kibinadamu na jopo la wanadiplomasia walioko nchini humo.

IRAN HAITAPELEKA MAHUJAJI WAKE SAIDIA MWAKA HUU.

Waziri wa Utamaduni na Miongozi ya Kiislamu wa Iran amesema, viongozi wa Saudi Arabia wanaendelea kukwamisha juhudi za Waislamu wa Iran za kwenda kutekeleza amali ya Hija mwaka huu.

Ali Jannati amesema hayo leo Alkhamisi wakati alipoonana na Ayatullah Sayyid Abdul Karim Mousavi Ardebili, mmoja wa maulamaa wakubwa na marjaa taqlidi wa mjini Qum, kusini mwa Tehran na kuongeza kuwa, takriban miezi minne imepita sasa tangu Iran ianze juhudi za kufuatilia namna wananchi wake watakavyokwenda kutekeleza amali ya Hija mwaka huu, lakini viongozi wa Saudia wanaendelea kukataa mapendekezo ya Iran katika masuala kama vile viza, usafiri wa anga na kudhaminiwa usalama wa mahujaji wa Iran, hasa kutokana na kuwa hakuna ubalozi wa Saudia nchini Iran.

Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran amesema, hadi hivi sasa viongozi wa Saudia hawajatoa ahadi zozote kuhusiana na suala la viza bali wanachotaka wao ni mahujaji wa Iran kwenda kuomba viza nchi nyingine, suala ambalo linaonesha wazi kuwa mazingira ya kuweza Waislamu wa Iran kwenda kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu hayapo.

Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran ameelekea mjini Qum kwa ajili ya kuonana na marajii na maulamaa wakubwa wa kidini mjini humo.

MASHINDANO YA QURAN YAANZA LEO IRAN.

Baada ya Dk Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kufungua duru ya 33 ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu jana Jumatano, mashindano hayo yameanza rasmi leo.

Mashindano hayo yameanza kwa kuchuanishwa washindanaji wa kuhifadhi Qur'ani nzima na qiraa na uhakiki wa Qur'ani.

Shirika la habari la IQNA limeripoti kuwa, mashindano ya qiraa na kuhifadhi Qur'ani nzima yamefanyika katika kumbi za hoteli walizofikia washindanaji hao mbele ya majaji wa kimataifa ikiwa ni hatua ya mchujo wa kuchagua watu wa kuingia kwenye ukumbi mkuu wa mashindano.

Itakumbukwa kuwa nchi 75 zina wawakilishi wao katika mashindano hayo. Hayo yamesemwa na Sheikh Ali Mohammadi Mwakilishi wa Faqihi Mtawala na Mkuu wa Taasisi ya Wakfu ya Iran ambaye ameongeza kwamba, kutakuwa na washiriki 130 kutoka nchi 75 katika mashindano hayo.

Amesema kwa mara ya kwanza mashindano hayo yanafanyika katika Ukumbi Mkubwa wa Swala wa Imam Khomeini MA hapa jijini Tehran, ili kuwezesha idadi kubwa ya watu kujumuika katika mashindano hayo.

Sheikh Ali Mohammadi ameongeza kuwa, mashindano ya mwaka huu yatakuwa na washiriki kutoka mabara ya Afrika, Asia, Ulaya, Marekani na Pasifiki.

Mashindano hayo ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yanatarajiwa kumalizika siku ya Jumanne ya mwezi kumi Shaaban, sawa na tarehe 17 mwezi huu wa Mei.

MSEVEN AAPISHWA KUWA RAIS KWA KIPINDI CHA TANO MFULULIZO.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye lishinda katika uchaguzi wa mwezi Februari mwaka huu, leo Alkhamisi ameapishwa kuwa rais wa nchi hiyo kwa kipindi cha tano mfululizo.

Sherehe za kuapishwa Yoweri Museveni ambazo zimefanyika jijini Kampala, zimehuhudhuriwa na marais wa nchi kadhaa za Afrika akiwemo Rais Omar al Bashir wa Sudan.

Museveni (71) aliingia madarakani mwaka 1986 nchini Uganda na katika uchaguzi wa tarehe 18 Februari mwaka huu, ameshinda kwa asilimia 60.62 ya kura.

Wasimamiaji wa kimataifa wamesema kuwa uchaguzi wa Rais nchini Uganda ulifanyika katika anga ya vitisho na hofu iliyosababishwa na miamala mibaya ya serikali.

Daktari Kizza Besigye, mmoja wa wagombea wa upinzani amekataa matokeo hayo na kujitangaza mshindi.

Jana polisi wa Uganda walimtia mbaroni Dakta Besigye. Baada ya kukamatwa Besigye, chama chake cha FDC kilisambaza mikanda ya video katika mitandao ya kijamii, inayoonyesha kiongozi wao huyo akiapishwa kama rais wa Uganda na kusema kuwa kiapo cha leo cha Rais Museveni si halali.

SIMBA: YANGA NA NDANDA KUCHEZA TAIFA NI RUSHWA.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Jerry Muro amesema, Ndanda FC itakapoutumia Uwanja wa Taifa itamaanisha kwamba Ndanda FC watakuwa nyumbani na hata mapato katika mgao asilimia kubwa ataipata Ndanda hivyo haoni sababu ya wengine kuanza kuongea kwa kuona ni makosa katika mchezo huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba Zacharia Hans Pope amesema, mchezo huo ni sio halali kwani inaonekana ni rushwa ya waziwazi kwa timu hizo, kwani haiwezekani umfadhili mpinzani wako ambaye unashindana na ukategemea matokeo ya halali.

Yanga ambayo ndio bingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu wa 2015/16 wakiwa wamesalia mechi mbili mkononi itakutana na Ndanda F Jumamosi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo mara baada ya kukamilika kwa mchezo huo, Yanga watakabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

MSUKUMA HABARI YAKO.


1
Mpemba sabalheri, unaionaje hali,
Kwangu mie ni buheri, namshukuru Jalali,
Usiwe na munkari, lijibu langu suali,
Kwanini wapenda shari, kama vile hauswali?
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
2
Mgogo habari yako, salamu zangu pokea,
Hapa nina swali lako, lile ulilo zoea,
Kuomba silika yako? jibu ninalingojea,
Lini unarudi kwako? Dom ulipotokea?
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
3
Mtumbatu nampenda, wenzangu naweka wazi,
Mtu huyu hana inda, tena hana utalazi,
Mwaminifu kama kunda, akiwa na laazizi,
Sishangae akikonda, sababu ya mkumbazi.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
4
Mmakunduchi mpole, si mwepesi kuchukia,
Tena hapendi kelele, na fujo kuzisikia,
Aenda huku na kule, kuti ajitafutia,
Ila mvivu kwa shule, umande aukimbia,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
5
Mzaramo sikupati, zinduka silale doro,
Uwate tupu kibeti, isifike yako soro,
Wapenda kichenipati, watoto wakosa karo,
Unalitunza kabati, nguo waweka kwa poro,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
6
Msukuma simsemi, ila ukweli nampa,
Sio kwamba hajitumi, tatizo ni zake pupa,
Pombe ageuza maji, huku nguo azitupa,
Akifika kwenye lami, anayavua malapa.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
7
Mnyakyusa kwa vioja, hakuna wa kumpata,
Fulusi anazifuja, kama vile aokota,
Aagizia mapaja, jikoni yalo tokota,
Anywa supu kwa mrija,soda kwake tarumbeta,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
8
Mhaya apenda sifa, tena kupita kiasi,
Aweza lalia fafa, kibanda chake cha nyasi,
Pia asiwe na sofa, masikini si mkwasi,
Atatamba sio lofa, ana kasri Parisi
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
9
Mhehe si mchokoze, hasa yule wa Kalenga,
Tena simgombeze, usimfanyie ngenga,
Hujui na nikujuze, mwepesi wa kujinyonga,
Kosa lake mueleze, maneno ukiyachunga.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
10
Mkuriya ana nini, leo nataka ukweli,
Kila siku gazetini, mara lile mara hili,
Kumwaga damu mwilini, kwake yeye ni sahali,
Ana tatizo rasini, kiasi aitwe nduli,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
11
Mluguru kwa kulima, mwenzenu nampongeza,
Gimbimaji na mlima, kuchemsha anaweza,
Wali wake kama sima, wallahi hutaongeza,
Atasema kwa heshima, mkono umeteleza,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
12
Mchaga toka Machame, aongoza ubahili,
Yu tayari akuchome, kikubwa apate dili,
Asemwa ni gumegume, ati ni yake asili,
Kama mate umteme, kiumbe huyu katili,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
13
Mha atege sikio, nisemalo asikie,
Anajua kwenda mbio, lengo lake litimie,
Afanye watu fagio, njia wamsafishie
Apate mafanikio, awaacha wajifie.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
14
Mkwere ana maneno, huyasema rejareja,
Kwa mithali na mifano, huzichanganya lahaja,
Kesha maliza matano, weye huna hata moja,
Vile bila ndoano, ajipatia kangaja,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
15
Mnyamwezi kwa ushamba, nadhani atia fora,
Avae apige pamba, utacheka kama jura,
Akiwa alima shamba, anaruka kama chura,
BASATA wakimbamba, 'taungana na Snura.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
16
Mdigo yule wa Tanga, asifika kwa kupika,
Uchungu wote wa chunga, kirahisi inalika,
Kwa mapenzi ndio nanga, ukizama hutatoka,
Ukikutoka ujinga, nguo anaziloweka,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
17
Mpare wa milimani, analima tangawizi,
Anashangaza jamani, chai yake ya mluzi,
Haipiki na majani, yaani hata mizizi,
Wanayo fikira gani, mjue sijamaizi,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
18
Mfipa kwake Mpanda, Mpimbwe na Sumbawanga,
Kibeku anakipanda, anapaa akiwanga,
Hufanya analopenda, kwa tunguri na usinga,
Akitaka kukuwinda, anakuchinjia ninga.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
19
Mmakonde mla panya, ati samaki mchanga,
Leo mimi nakukanya, ndugu yangu wa Nambunga,
Hebu jaribu kufanya, uvue japo mkunga,
Rohoni nimekusinya, natamani kukutenga.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
20.
Kaditama samahani, nyie nilio wakwaza,
Mimi ni wenu mtani, sio yule wa Vigwaza,
Natokea undambani, Ifakara si Muheza,
Msiweke mtimani, lengo si kuwachokoza.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
whatspp/call 0622845394 Morogoro.