NINI MAANA YA UKIMYA WA JOHN MNYIKA??

Na Charles Francis M,

Kwa muda mrefu sasa naibu katibu mkuu wa Chadema bara, ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kibamba, ndugu John Mnyika amekuwa kimya katika majukwaa ya kisiasa. Mnyika kwa nafasi yake kama naibu katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani, lakini pia kwa nafasi yake ya ubunge na "mtindo" wake wa kuibua hoja na kueleza bila kuogopa, hakustahili kuwa kimya!

Kimya hiki kimeibua hoja nyingi sana lakini hoja kuu nne zimekuwa zikijadiliwa sehemu mbali mbali. Hoja hizi zinaonekana kila moja kwa nafasi yake kubeba aina fulani ya ukweli. Hoja hizi ni pamoja na:

1. UJIO WA LOWASSA NA AGENDA YA UFISADI.

Ikumbukwe kwamba wakati wa mchakato wa kumpata mgombea Urais ndani ya chama cha Chadema, mpasuko mkubwa ulitokea mara baada ya Lowassa kujiunga na Chadema na kupewa ridhaa ya kuwa mgombea wa Urais. Ina aminika kwamba baada ya Lowassa kuingia Chadema ile agenda ya Ufisadi "ikazikwa" rasmi maana agenda ile kwa kiasi kikubwa ilimlenga Lowassa, hivyo kuhamia kwake kukawa pigo na mpasuko kwa Chadema.

Hali inaonekana kumkera John Mnyika na hivyo kuamua kutozungumzia suala lolote linalo husu chama au Lowassa mwenyewe. Ikumbukwe pia tangu Lowassa ajiunge na Chadema, ni naibu katibu mkuu (Zanzibar) pekee ambaye amekuwa akizungumzia ujio wa Lowassa na siyo Mnyika kama ambavyo "protocol" ya uongozi ilitaka! Ujio wa Lowassa unaonekana kukifanya chama hicho kipoe na kikose agenda mbadala ya kusimamia ikilinganishwa na kasi ya serikali ya sasa.

2. AFYA YA JOHN MNYIKA.

Kundi la pili wana hoja kwamba kwa sasa John Mnyika inawezekana akawa ni mgonjwa na hivyo kukosa muda wa kuwa majukwaani au kuonekana katika medani za kisiasa kama ilivyo zoeleka! Suala hili haliko wazi sana, siyo chama wala Mnyika mwenyewe walio zungumza juu ya suala hili.

3. MIPANGO NA MIKAKATI YA "SIRI".
Kuna kundi lingine wana imani kwamba ukimya wa John Mnyika ni mkakati wake wa "siri" ili aibuke na hoja nzito ya kitaifa kukinusuru chama chake au ni mkakati wake binafsi wa kujijenga kisiasa na kuondoa aina ya siasa hasa za chama chake ambazo zimekuwa zikitafsiriwa kama siasa za "vurugu" "mihemko" na matukio!

4. CHAMA KUENDESHWA "NDIVYO SIVYO"
Kundi lingine lina amini kwamba John Mnyika hapendezwi na mwenendo wa chama chake kuwa kama mali ya watu wachache. Kundi hili wana amini kwamba Chadema ina endeshwa na watu wachache ambao maamuzi yao hayapingwi na ukipinga unaitwa "MSALITI". Watu wa kundi hili wana amini kwamba Chadema ya sasa haina mashiko, inapoteza mwelekeo na kujisahihisha kwake ni vigumu kwa mfumo huu wa maamuzi ya watu wachache na "hasa mwenyekiti". Kundi hili wana amini pia siasa za "harakati" zimekwisha poteza mwelekeo, kwa sasa ni siasa za "utendaji".

Ukimya wa John Mnyika bado ni kitendawili kwa wengi, ukimya wake unataka kufanana na ule alio anza kuonyesha Dk Slaa kipindi cha uchaguzi mpaka alipo tangaza kujiondoa Chadema. Wapo wanao amini kwamba Mnyika anataka kufanya "maamuzi" MAGUMU.

Haya yote yanabaki kuwa nadharia tu, ni maoni na mawazo ya watu! Ukweli anao John Mnyika mwenyewe, je wewe unaona mtazamo gani kati ya hii ni sahihi??

"Caytano Maytano"

Charles Francis M.

RAIS MUSEVEN ATAZAMIWA KUAPISHWA, KIZZA YUKO SERO.

Katika hali ambayo Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda anatazamiwa kuapishwa wakati wowote tokeo sasa, kinara wa upinzanai nchini humo Dakta Kizza Besigye anaendelea kuzuiliwa katika jela ya Nalufenya wilayani Jinja eneo la Karamoja.

Besiye ambaye ni mkuu wa chama cha FDC alikamatwa jana Jumatano baada ya kujitokeza ghafla katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala. Haijabainika namna Besigye alivyowakwepa maafisa wa usalama ambao wamekuwa wakiizingira nyumba yake huko Kasangati wilayani Wakiso na kufululiza hadi katikati ya mji wa Kampala.

Kujitokeza kwake ghafla mjini Kampala kulivutia idadi kubwa ya wafuasi wake na hapo ndipo maafisa wa polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuutawanya mkusanyiko huo na kisha wakamkamata Besigye na kumpeleka hadi uwanja mdogo wa ndege wa Kololo na kisha kupelekwa hadi gereza la Nalufenyam wilayani Jinja.

Uwanja huo wa ndege ambao pia unajulikana kama Viwanja vya Sherehe vya Kololo, ni sehemu ambayo Rais Museveni anatazamiwa kula kiapo cha kulitumikia taifa kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Baada ya kukamatwa Dakta Besigye, chama chake cha FDC kilisambaza katika mitandao ya kijamii, kanda ya video inayoonyesha kinara huyo wa upinzani akiapishwa kama rais wa nchi na kusema kuwa kiapo cha leo cha Rais Museveni sio halali.

Rais Yoweri Museveni alishinda tena kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika Februari mwaka huu. Hata hivyo wapinzani nchini Uganda akiwemo hasimu wake mkuu Dakta Kizza Besigye wamekataa kutambua ushindi huo wakisisitiza kwamba, hakuchaguliwa kihalali.

Tayari viongozi wa mbai mbali wamefika katika Viwanja vya Kololo kushuhudiwa kuapishwa kwa Rais Museveni, wakimwemo Marais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Omar al-Bashir wa Sudan na Uhuru Kenyatta wa Kenya. Aidha Marais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete wamekwishafika katika uwanja huo.

KABILA KUENDELEA KUWA RAIS WA DRC HATA BAADA YA MUHULA WAKE KUPITA.

Mahakama ya Juu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema kuwa huenda Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo akasalia madarakani hata baada ya kumalizika muhula wake iwapo uchaguzi mkuu utakosa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Katika uamuzi wake jana Jumatano, mahakama hiyo ilisema katiba hairuhusu kuwepo ombwe la uongozi nchini na kwa msingi huo, iwapo uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu utakosa kufanyika kutokana na sababu yoyote ile, basi Rais Kabila hatakuwa na budi ila kuendelea kuwa uongozini hadi mgogoro huo upatiwe ufumbuzi.

Kabila anapaswa kuondoka madarakani Novemba 19 mwaka huu baada ya kumalizika duru ya pili ya urais.

Kwa miezi kadhaa sasa, jamii ya kimataifa imekuwa ikisisitizia umuhimu wa kufanyika uchaguzi mkuu katika tarehe iliyopangwa huko Kongo DR, huku waungaji mkono wa Rais Joseph Kabila wakitaka zoezi hilo lisogezwe mbele wakisisitiza kuwa mazingira ya sasa hayaruhusu kufanyika uchaguzi. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena katika uchaguzi ujao. Machi 31 mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2277 kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kupitia azimio hilo, Baraza la Usalama lilimtaka Rais Joseph Kabila kuhakikisha kuwa uchaguzi wa rais unafanyika katika muda uliopangwa.

DAESH LIMEUA WAITHIOPIA 16 LIBYA.

Kundi la kigaidi la Daesh limetoa kanda mpya ya video ya kuogofya inayoonyesha namna magaidi hao wanavyowaua kinyama raia wa Ethiopia nchini Libya.

Kanda hiyo ya video ya dakika 29 hivi inaonyesha namna magaidi hao wa Daesh ambao walikuwa wamefunika nyuso zao walivyowaua raia wa Ethiopia kwa kuwamininia risasi kichwani huku wakiwa wamefungwa mikono na kupigishwa magoti.

Baadhi ya raia 16 wa Ethiopia waliouawa na Daesh kwa kufyatuliwa risasi walikuwa wamefungwa chini ya miti na wengine wakauawa kwenye ufuo wa bahari. Habari zinasema kuwa, raia hao wa Ethiopia waliouawa na Daesh katika ardhi ya Libya ni waumini wa dini ya Kikristo.

Kabla ya kutekeleza ukatili huo, mmoja wa magaidi hao alisoma ujumbe unaosema: "Hawa ni wafuasi wa msalaba kutoka Kanisa la maadui huko Ethiopia, ambao wamekataa kulipa kodi ya kidini au kusilimu."

Hii sio mara ya kwanza kwa kundi la kigaidi la Daesh kutekeleza unyama wa aina hii dhidi ya raia wa Ethiopia nchini Libya.

Mwezi uliopita wa Aprili, magaidi hao wenye misimamo ya mikali na hatari walitoa kanda nyingine ya video iliyoonyesha wakiua raia 30 wa Ethiopia wafuasi wa dini ya Kikristo kwa misingi hiyo hiyo eti ya kukataa kulipa kodi au kujiunga na Uislamu. Baadhi yao waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na wengine kwa kukatwa vichwa.

MAKAASISI 71 WA MAREKANI WATUHUMIWA KULAWITI WATOTO.

Dayosisi Kuu ya Kanisa Katoliki katika mji wa Baltimore jimboni Maryland nchini Marekani imefichua majina ya makasisi 71 wanaotuhumiwa kuwalawiti watoto wadogo.

Sean Caine, Msemaji wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo amesema tayari wamechapisha katika tovuti ya kanisa hilo majina ya makasisi hao wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya kuwadhulumu kimapenzi watoto wadogo.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwashajiisha waathiriwa wa vitendo vya ulawiti kujitokeza na kulizungumzia swala hili ikizingatiwa kuwa, kesi nyingi za liwati zinazohusisha viongozi wa Kanisa Katoliki zimekuwa zikifumbiwa macho huku wahusika wakikosa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Marekani, takriban makasisi 6,900 wa Kanisa Katoliki la Roma wanadaiwa kuwalawiti watoto wadogo 16,900 kati ya mwaka 1950 na 2011.

NI SAWA KWA MJAMZITO KUINUA VYUMA VIZITO KWA MAZOEZI?

Huyu ni mjamzito mwenye nguvu kubwa zaidi!

Bibi Emily Watson mwenye umri wa miaka 31 anayeishi nchini Marekani anapenda kufanya mazoezi ya viungo, hata baada ya kuwa na mimba, anaendelea kufanya mazoezi ya kunyanyua uzito kwa mara sita kila wiki. Watu wengi hawaungi mkono kitendo chake, wanasema kufanya mazoezi kupita kiasi kutaathiri vibaya mimba changa. Una maoni gani kuhusu kitendo cha mama huyu?

RAIS WA TAFF AZUNGUMZIA KIFO CHA KINYAMBE.

Akiongea na EATV Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Simon Mwakifwamba, amesema ameongea na baba mzazi wa marehemu na kuthibitisha kifo hicho, ambacho kimesababishwa kwa ugonjwa wa mapafu kujaa maji.

Mwakifwamba amesema taratibu za mazishi zinaendelea mkoani Mbeya ambako ndio nyumbani kwao marehemu, na wanaangalia kama kuna uwezekano wa wasanii wenzake kuhudhuria.
RIP Kinyambe

WALIOKUFA KWA BOMU BAGHDAD WAFIKIA 64

Idadi ya vifo kutokana na shambulizi la bomu lililotokea katika soko moja lililoko mashariki mwa mji mkuu wa Baghdad,Iraq,vimeongezeka hadi 64 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia 87,taarifa kutoka kwa Wizara ya Mambo ya ndani alisema.

Mlipuko huo mkubwa ulitokea asubuhi wakati gari lililokuwa limenaswa lililipuka katika soko maarufu katika ngome ya Shiite katika wilaya ya Sadr City,taarifa hiyo ilisema.

IRAN: HATUHITAJI RUHUSA YA MTU KUJIHAMI.

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa radiamali kuhusiana na matamshi ya msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani aliyotoa kuhusiana na mpango wa makombora wa Iran na kusema kuwa, taifa hili halihitaji kupata ruhusa ya mtu yeyote kwa ajili ya kujihami.

Ali Akbar Velayati amesema kuwa, baadhi ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama Russia inaamini kwamba, hatua hii ya Iran ya kufanya majaribio ya makombora haipingani na azimio la Baraza la Usalama.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa, Washington inayachukulia majaribio ya makombora ya balistiki ya Iran kwamba, ni hatua ya kichochezi na yenye lengo la kuvuruga uthabiti.

Iran hivi karibuni ilifanyia majaribio kombora la balistiki lenye uwezo wa kuruka masafa ya kilomita 2,000 na kulenga shabaha kwa ustadi mkubwa.

Nchi za Magharibi hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimekuwa zikikosoa majaribio ya makombora ya balisitiki Iran na kudai eti majaribio hayo yanakiuka azimio nambara 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa baada ya mapatano ya nyuklia ya Iran yaliyofikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.