MSUKUMA HABARI YAKO.
MSUKUMA HABARI YAKO.
1
Mpemba sabalheri, unaionaje hali,
Kwangu mie ni buheri, namshukuru Jalali,
Usiwe na munkari, lijibu langu suali,
Kwanini wapenda shari, kama vile hauswali?
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
2
Mgogo habari yako, salamu zangu pokea,
Hapa nina swali lako, lile ulilo zoea,
Kuomba silika yako? jibu ninalingojea,
Lini unarudi kwako? Dom ulipotokea?
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
3
Mtumbatu nampenda, wenzangu naweka wazi,
Mtu huyu hana inda, tena hana utalazi,
Mwaminifu kama kunda, akiwa na laazizi,
Sishangae akikonda, sababu ya mkumbazi.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
4
Mmakunduchi mpole, si mwepesi kuchukia,
Tena hapendi kelele, na fujo kuzisikia,
Aenda huku na kule, kuti ajitafutia,
Ila mvivu kwa shule, umande aukimbia,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
5
Mzaramo sikupati, zinduka silale doro,
Uwate tupu kibeti, isifike yako soro,
Wapenda kichenipati, watoto wakosa karo,
Unalitunza kabati, nguo waweka kwa poro,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
6
Msukuma simsemi, ila ukweli nampa,
Sio kwamba hajitumi, tatizo ni zake pupa,
Pombe ageuza maji, huku nguo azitupa,
Akifika kwenye lami, anayavua malapa.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
7
Mnyakyusa kwa vioja, hakuna wa kumpata,
Fulusi anazifuja, kama vile aokota,
Aagizia mapaja, jikoni yalo tokota,
Anywa supu kwa mrija,soda kwake tarumbeta,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
8
Mhaya apenda sifa, tena kupita kiasi,
Aweza lalia fafa, kibanda chake cha nyasi,
Pia asiwe na sofa, masikini si mkwasi,
Atatamba sio lofa, ana kasri Parisi
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
9
Mhehe si mchokoze, hasa yule wa Kalenga,
Tena simgombeze, usimfanyie ngenga,
Hujui na nikujuze, mwepesi wa kujinyonga,
Kosa lake mueleze, maneno ukiyachunga.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
10
Mkuriya ana nini, leo nataka ukweli,
Kila siku gazetini, mara lile mara hili,
Kumwaga damu mwilini, kwake yeye ni sahali,
Ana tatizo rasini, kiasi aitwe nduli,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
11
Mluguru kwa kulima, mwenzenu nampongeza,
Gimbimaji na mlima, kuchemsha anaweza,
Wali wake kama sima, wallahi hutaongeza,
Atasema kwa heshima, mkono umeteleza,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
12
Mchaga toka Machame, aongoza ubahili,
Yu tayari akuchome, kikubwa apate dili,
Asemwa ni gumegume, ati ni yake asili,
Kama mate umteme, kiumbe huyu katili,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
13
Mha atege sikio, nisemalo asikie,
Anajua kwenda mbio, lengo lake litimie,
Afanye watu fagio, njia wamsafishie
Apate mafanikio, awaacha wajifie.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
14
Mkwere ana maneno, huyasema rejareja,
Kwa mithali na mifano, huzichanganya lahaja,
Kesha maliza matano, weye huna hata moja,
Vile bila ndoano, ajipatia kangaja,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
15
Mnyamwezi kwa ushamba, nadhani atia fora,
Avae apige pamba, utacheka kama jura,
Akiwa alima shamba, anaruka kama chura,
BASATA wakimbamba, 'taungana na Snura.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
16
Mdigo yule wa Tanga, asifika kwa kupika,
Uchungu wote wa chunga, kirahisi inalika,
Kwa mapenzi ndio nanga, ukizama hutatoka,
Ukikutoka ujinga, nguo anaziloweka,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
17
Mpare wa milimani, analima tangawizi,
Anashangaza jamani, chai yake ya mluzi,
Haipiki na majani, yaani hata mizizi,
Wanayo fikira gani, mjue sijamaizi,
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
18
Mfipa kwake Mpanda, Mpimbwe na Sumbawanga,
Kibeku anakipanda, anapaa akiwanga,
Hufanya analopenda, kwa tunguri na usinga,
Akitaka kukuwinda, anakuchinjia ninga.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
19
Mmakonde mla panya, ati samaki mchanga,
Leo mimi nakukanya, ndugu yangu wa Nambunga,
Hebu jaribu kufanya, uvue japo mkunga,
Rohoni nimekusinya, natamani kukutenga.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
20.
Kaditama samahani, nyie nilio wakwaza,
Mimi ni wenu mtani, sio yule wa Vigwaza,
Natokea undambani, Ifakara si Muheza,
Msiweke mtimani, lengo si kuwachokoza.
Nang'ata na kupuliza, utani nawatania.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
whatspp/call 0622845394 Morogoro.
AZAM IMETINGA NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO.
Klabu ya Azam FC imetinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho nchini Tanzania baada ya kuifunga Mwadui kwa mikwaju ya penati 5 kwa 3.
Azam imefikia hatua hiyo baada ya dakika 120 kumalizika kwa timu hizo kufungana mabao 2-2.
Penati za Azam zimefungwa na Waziri Salum, Allan Wanga, Himid Mao, John Bocco na Agrey Moris huku Kelvin Sabato akikosa penati ya 4 kwa upande wa Mwadui.
KENYA NA TANZANIA ZAKAMATA GARI TATU ZA WIZI.
Polisi wa Kenya na wale wa Tanzania wamepata magari matatu ambayo yalikuwa yameibiwa nchini Kenya na kupelekwa mjini Moshi.Polisi kwenye kaunti ya Taita Taveta wanasema mojawepo wa magari hayo ni ya kampuni ya China inayojenga reli nchini Kenya ya Zong Miang Engineering Company .
Magari hayo matatu yalipatikana yametelekezwa bila mtu kwenye mji huo wa Moshi nchini Tanzania.
USAWA WA BAHARI HUKO NEW ZEALAND UTAINUKA KWA MM 30 KATIKA KARNE HII.
Usawa wa bahari kando ya New Zealand utainuka kwa milimita 30 hata mita moja ndani ya karne hii
Ripoti iliyotolewa na taasisi ya New Zealand inaonesha kuwa, kama utoaji wa hewa inayosababisha kuongezeka kwa joto duniani hakutapungua kwa kiasi kikubwa, joto litaendelea kuongezeka, na usawa wa bahari kando ya New Zealand utainuka kwa milimita 30 hata mita moja ndani ya karne hii.
Kuinuka kwa usawa wa bahari kutasababisha maji ya bahari kuingia kwenye fukwe nchini humo, na hivyo mafuriko yatatokea mara kwa mara wakati wa mvua kubwa. Hivi sasa watu wengi wanaishi pwani, na theluthi mbili ya watu wanaishi katika maeneo yaliyo kwenye hatari zaidi ya kukumbwa na mafuriko.
Mfano pwani ya Otago iliyoko kisiwa cha kusini cha nchi hiyo, tofauti kati ya urefu wa mawimbi yanayosababishwa na tufani yanayotokea kila baada ya miaka miwili na mawimbi makubwa yanayotokea kila miaka mia moja ni milimita 32 tu, hii inamaanisha kuwa kama usawa wa bahari ukiinuka kwa milimita 30, maafa ya mafuriko yaliyotokea kila miaka mia moja huenda yatatokea kila mwaka.
Licha ya hayo, wakati joto linapoendelea kuongezeka, mvua itapungua, kazi za ujenzi, uzalishaji viwandani na utoaji wa maji baridi zitakabiliwa na shinikizo kubwa. Wanyama na mimea ambayo sasa iko hatarini huenda vitatoweka.
Ingawa kuongezeka kwa joto duniani kutasababisha kupanda kwa bei ya bidhaa duniani, na kunufaisha maendeleo ya kilimo nchini humo, lakini pia kutaleta athari nyingi mbaya, na kuhatarisha usalama wa chakula.
TFDA YANASA VIPODOZI HARAMU TANI 15.
Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini TFDA imenasa vipodozi vya magendo tani 15 vyenye thamani ya shilingi milioni 400 mjini Dar es Salaam.
Bidhaa hizo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye ghorofa mbili zilizoko eneo la Karioakoo mjini humo.
Meneja wa TFDA Emmanuel Alphone amesema vipodozi hivyo vimeingizwa bila ya idhidi ya mamlaka husika.
Watu wanane wamekamatwa na kuhojiwa kuhusiana na bidhaa hizo na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
SOMALIA NA AU WAJIPANGA KUPAMBANA NA UGAIDI.
Somalia na Umoja wa Afrika wanapanga kuwa na mikakati mipya ya usalama ili kuzuia matishio ya ugaidi nchini Somalia.
Mwakilishi maalum wa mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika nchini Somalia Bw Francisco Madeira amefanya mazungumzo na naibu waziri mkuu wa Somalia Bw Mohamed Omar Arte kuhusu mambo muhimu ya operesheni za usalama.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Africa imesema, kwenye mkutano huo, maofisa hao wawili walijadili kuhusu jinsi majeshi ya serikali ya Somalia na tume ya Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM yanavyoweza kuratibu na kushirikiana kulishinda kundi la Al Shabaab.
RIYAD MAHREZ AWA MWAFRIKA WA KWANZA KUSHINDA TUZO YA PFA.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Algeria anayeichezea klabu ya Leicester City ya Uingereza Riyad Mahrez ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya PFA 2015/2016 (Professional Footballers Association).
Riyad Mahrez ametangazwa kushinda tuzo hiyo mbele ya wachezaji kama Mesut Ozil wa Arsenal, Jamie Vardy wa Leicester City, Harry Kane wa Totenham Hot Spurs, N’golo Kante wa Leicester City na Dimitri Payet wa West Ham United.
PFA ni tuzo za wachezaji bora wa kulipwa.
CRYSGAL PALACE IYAKUTANA NA MANCHESTER KOMBE LA FA.
Crystal Palace itakutana na Manchester United katika fainali ya kombe la FA mwaka 2016, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Watford City.
Yannick Bolasie aliongoza Palace kabla ya Troy Deeney kusawazisha kunako dakika ya 55, lakini Conor Wickham alifunga bao la pili na la ushindi kwenye dakika ya 61.
WABUNGE TISA WAPEWA SIKU 30 KUICHUNGUZA LUGUMI.
WABUNGE TISA WAPEWA SIKU 30 KUICHUNGUZA LUGUMI.
Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana mjini Dodoma baada ya kikao cha kamati hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa PAC Mh.Aeshy Hilary amesema uamuzi wa kuundwa kamati hiyo umekuja kufuatia kutoridhishwa na ripoti hiyo pamoja na kuwepo kwa changamoto katika taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliyowasilishwa na Jeshi la Polisi.
Mh. Hilary alisema kuwa majukumu ya kamati hiyo yatakayoongozwa na Mwenyekiti wake Mh. Josephat Asunga ni k...uwa kamati hiyo ndogo itafanya uchunguzi kwa muda wa siku 30 sambamba na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).