SOMALIA NA AU WAJIPANGA KUPAMBANA NA UGAIDI.

Somalia na Umoja wa Afrika wanapanga kuwa na mikakati mipya ya usalama ili kuzuia matishio ya ugaidi nchini Somalia.

Mwakilishi maalum wa mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika nchini Somalia Bw Francisco Madeira amefanya mazungumzo na naibu waziri mkuu wa Somalia Bw Mohamed Omar Arte kuhusu mambo muhimu ya operesheni za usalama.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Africa imesema, kwenye mkutano huo, maofisa hao wawili walijadili kuhusu jinsi majeshi ya serikali ya Somalia na tume ya Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM yanavyoweza kuratibu na kushirikiana kulishinda kundi la Al Shabaab.

RIYAD MAHREZ AWA MWAFRIKA WA KWANZA KUSHINDA TUZO YA PFA.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Algeria anayeichezea klabu ya Leicester City ya Uingereza Riyad Mahrez ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya PFA 2015/2016 (Professional Footballers Association).

Riyad Mahrez ametangazwa kushinda tuzo hiyo mbele ya wachezaji kama Mesut Ozil wa Arsenal, Jamie Vardy wa Leicester City, Harry Kane wa Totenham Hot Spurs, N’golo Kante wa Leicester City na Dimitri Payet wa West Ham United.
PFA ni tuzo za wachezaji bora wa kulipwa.

CRYSGAL PALACE IYAKUTANA NA MANCHESTER KOMBE LA FA.

Crystal Palace itakutana na Manchester United katika fainali ya kombe la FA mwaka 2016, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Watford City.

Yannick Bolasie aliongoza Palace kabla ya Troy Deeney kusawazisha kunako dakika ya 55, lakini Conor Wickham alifunga bao la pili na la ushindi kwenye dakika ya 61.

WABUNGE TISA WAPEWA SIKU 30 KUICHUNGUZA LUGUMI.


















WABUNGE TISA WAPEWA SIKU 30 KUICHUNGUZA LUGUMI.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana mjini Dodoma baada ya kikao cha kamati hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa PAC Mh.Aeshy Hilary amesema uamuzi wa kuundwa kamati hiyo umekuja kufuatia kutoridhishwa na ripoti hiyo pamoja na kuwepo kwa changamoto katika taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliyowasilishwa na Jeshi la Polisi.

Mh. Hilary alisema kuwa majukumu ya kamati hiyo yatakayoongozwa na Mwenyekiti wake Mh. Josephat Asunga ni k...uwa kamati hiyo ndogo itafanya uchunguzi kwa muda wa siku 30 sambamba na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ameongeza kuwa uchunguzi huo utafanywa kwa mtindo wa kikachero na ule wa kushtukiza, ili kukwepa hali ya kuandaliwa kwa mazingira ya kuficha ukweli.

GAIDI MWANDAMIZI WA AHRAR AL SHAM AUAWA HUKO SYRIA.











GAIDI MWANDAMIZI WA AHRAR AL SHAM AUAWA HUKO SYRIA.

Kamanda mwandamizi wa kundi la kigaidi la Ahrar al-Sham lenye mafungamano na mtandao wa kimataifa wa al-Qaeda ameuawa katika hujuma ya bomu iliyolenga ngome za kundi hilo katika mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria.
Majid Hussein al-Sadeq pamoja na magaidi wengine watatu waliuawa katika shambulio la jana Jumamosi dhidi ya mji wa Binnish, unaohesabiwa kuwa moja ya ngome za magaidi hao, yapata kilomita 10 kaskazini mashariki mwa mkoa wa Idlib.
Julai mwaka jana, kamanda mwingine mkuu wa kundi la kigaidi la Ahrar al-Sham kwa jina Abu Abdu Rahman Salqin aliuawa katika shambulio jingine la bomu katika eneo la Abu Talha, mkoani Idlib.
Kwa muda mrefu sasa serikali ya Syria imekuwa ikisisitiza kuwa magaidi nchini humo wanapata misaada ya fedha na silaha kutoka nchi za Magharibi hasa Marekani na waitifaki wake katika eneo hili ambao ni Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na utawala haramu wa Israel. Karibu watu nusu milioni wameshapoteza maisha tokea magaidi waanzishe kampeni ya kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad wa Syria mwaka 2011.
Hii ni katika hali ambayo, Steffan de Mistura, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesema watu wapatao laki nne wamepoteza maisha kutokana na vita vya zaidi ya miaka mitano vilivyoikumba nchi hiyo ya Kiarabu.

ALIYEMTUSI MTUME MUHAMMAD(S.A.W) AUHUKUMIWA KIFO MAURITANIA.


Mahakama ya Rufaa ya Mauritania imepasisha hukumu ya kifo dhidi ya mwandishi aliyemvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).

Shirika la Habari la Kimataifa la Qur'ani (IQNA) limeripoti kuwa, Mahakama ya Rufaa ya mji wa Nawadibo huko kaskazini magharibi mwa Mauritania imepasisha hukumu ya kifo dhidi ya mwandishi Muhammad Sheikh Ould Amkhtir wa nchi hiyo kwa sababu ya kuandika makala iliyomvunjia heshima na kumtusi Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) hapo mwaka 2014.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mauritania ambaye aliomba kutolewe hukumu ya kifo dhidi ya mwandishi huyo amesema kuwa kunyongwa kwake kutakuwa somo kwa wale wote wanaothubutu kumvunjia heshima Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Kuchapishwa kwa makala ya mandishi Muhammad Sheikh Ould Amkhtir hapo mwaka 2014 kulisababisha maandamano makubwa kote Mauritania ambayo hayakutulia ila baada ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi ya mwandishi huyo.

UMOJA WA ULAYA HAUTAMBUI UMILIKI WA ISRAELI KWA MIINUKO YA GOLAN.


Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, umoja huo hauutambui rasmi umiliki na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa miinuko ya Golan ya Syria.

Federica Mogherini amesisitiza kuwa, Umoja wea Ulaya hautambui ukaliaji mabavu wa Israel dhidi ya ardhi za Palestina baada ya vita vya mwaka 1967 na kuongeza kuwa, huu ni msimamo wa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa umoja huo.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema hayo siku chache baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kudai kwamba, miinuko ya Golan ya Syria ni sehemu ya ardhi ya utawala huo.

Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu alinukuliwa hivi karibuni akidai kwamba, miinuko hiyo ya Golan daima itakuwa sehemu isiyotenganishika na utawala huo.

Utawala ghasibu wa Israel uliikalia kwa mabavu sehemu ya miinuko ya Golan ya Syria mwaka 1967 katika vita vyake na Waarabu. Mwaka 1981, utawala huo wa kimabavu uliiunganisha sehemu hiyo na ardhi unazozikalia kwa mabavu, hatua ambayo hakuna wakati ilitambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa.

WATU 13 WAFA CONGO DRC KWA MAPIGANO KATI YA SERIKALI NA WAASI.


Watu wasiopungua 13 wamepoteza maisha katika mapigano baina ya jeshi la serikali na kundi la wanamgambo eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Duru za usalama nchini humo zimeripoti kuwa, katika mapigano hayo watu 12 waliouawa ni wanamgambo, na mwingine mmoja ni askari wa serikali. Aidha jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeongeza kuwa, mbali na idadi hiyo kuuawa, wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa ripoti, mapigano hayo yamejiri katika eneo la Biakato, mashariki mwa nchi hiyo na kwamba wanamgambo hao ni wanachama wa kundi la Mai-Mai. Mwishoni mwa mapigano hayo askari wa serikali walifanikiwa kudhibiti silaha za wanamgambo hao waliokimbia na kuacha silaha zao hizo. Jeshi la serikali pia limetangaza kuhitimisha shughuli za wanamgambo wa waasi katika eneo hilo la Biakato.

Ni miaka 20 sasa tokea eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lianze kushuhudia hujuma za wanamgambo wanaoipinga serikali ya Kinshasa, huku wahanga wakuu wakiwa ni raia wa kawaida.

DAESH WATUMIA SILAHA ZA SUMU HUKO IRAQ.


Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, wametumia silaha za kemikali katika maeneo ya raia kaskazini wa Iraq.

Shambulizi hilo limefanywa katika eneo la Abu Shit wanapoishi idadi kubwa ya Wakurdi katika viunga vya mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq ambapo magaidi hao wametumia maguruneti yenye silaha hizo zilizopigwa marufuku. Kwa mara kadhaa sasa wanachama wa kundi hilo la kitakfiri wamekuwa wakitumia silaha zenye gesi ya sumu katika maeneo ya raia wa kawaida na kuua idadi kubwa ya watu. Katika hatua nyingine, Abdul-Muhsin al-Abbasi, mmoja wa makamanda wa jeshi la Iraq ametangaza kuwa, askari wa nchi hiyo kwa kushirikiana na wapiganaji wa kujitolea, wamefanikiwa kukomboa vijiji kadhaa vya mkoa wa al-Anbar, magharibi mwa nchi.

Katika operesheni hizo, jeshi la Iraq limemuua kiongozi wa ngazi za juu kabisa wa kundi la Daesh aliyekuwa akiitwa Yassin al-Khalifawi, maarufu kwa jina la Da'fasah, akiwa pamoja na viongozi wengine wa genge hilo la kigaidi. Aidha askari wa Iraq pia wamedhibiti silaha na zana kadhaa za kijeshi zilizokuwa zikitumiwa na matakfiri hao maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, ndege za kijeshi za Uturuki kwa mara nyingine tena zimefanya mashambulizi kadhaa ndani ya ardhi ya Iraq katika maeneo ya wapiganaji wa Kundi la PKK ambao wamekuwa wakipambana na wapiganaji wa Daesh nchini humo. Hii si mara ya kwanza kwa ndege za Uturuki kuvuka mipaka yake na kutekeleza hujuma zake nje ya nchi hiyo, suala ambalo limekuwa likilaaniwa na serikali kuu ya Baghdad.