WATU 13 WAFA CONGO DRC KWA MAPIGANO KATI YA SERIKALI NA WAASI.


Watu wasiopungua 13 wamepoteza maisha katika mapigano baina ya jeshi la serikali na kundi la wanamgambo eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Duru za usalama nchini humo zimeripoti kuwa, katika mapigano hayo watu 12 waliouawa ni wanamgambo, na mwingine mmoja ni askari wa serikali. Aidha jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeongeza kuwa, mbali na idadi hiyo kuuawa, wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa ripoti, mapigano hayo yamejiri katika eneo la Biakato, mashariki mwa nchi hiyo na kwamba wanamgambo hao ni wanachama wa kundi la Mai-Mai. Mwishoni mwa mapigano hayo askari wa serikali walifanikiwa kudhibiti silaha za wanamgambo hao waliokimbia na kuacha silaha zao hizo. Jeshi la serikali pia limetangaza kuhitimisha shughuli za wanamgambo wa waasi katika eneo hilo la Biakato.

Ni miaka 20 sasa tokea eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lianze kushuhudia hujuma za wanamgambo wanaoipinga serikali ya Kinshasa, huku wahanga wakuu wakiwa ni raia wa kawaida.

DAESH WATUMIA SILAHA ZA SUMU HUKO IRAQ.


Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, wametumia silaha za kemikali katika maeneo ya raia kaskazini wa Iraq.

Shambulizi hilo limefanywa katika eneo la Abu Shit wanapoishi idadi kubwa ya Wakurdi katika viunga vya mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq ambapo magaidi hao wametumia maguruneti yenye silaha hizo zilizopigwa marufuku. Kwa mara kadhaa sasa wanachama wa kundi hilo la kitakfiri wamekuwa wakitumia silaha zenye gesi ya sumu katika maeneo ya raia wa kawaida na kuua idadi kubwa ya watu. Katika hatua nyingine, Abdul-Muhsin al-Abbasi, mmoja wa makamanda wa jeshi la Iraq ametangaza kuwa, askari wa nchi hiyo kwa kushirikiana na wapiganaji wa kujitolea, wamefanikiwa kukomboa vijiji kadhaa vya mkoa wa al-Anbar, magharibi mwa nchi.

Katika operesheni hizo, jeshi la Iraq limemuua kiongozi wa ngazi za juu kabisa wa kundi la Daesh aliyekuwa akiitwa Yassin al-Khalifawi, maarufu kwa jina la Da'fasah, akiwa pamoja na viongozi wengine wa genge hilo la kigaidi. Aidha askari wa Iraq pia wamedhibiti silaha na zana kadhaa za kijeshi zilizokuwa zikitumiwa na matakfiri hao maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, ndege za kijeshi za Uturuki kwa mara nyingine tena zimefanya mashambulizi kadhaa ndani ya ardhi ya Iraq katika maeneo ya wapiganaji wa Kundi la PKK ambao wamekuwa wakipambana na wapiganaji wa Daesh nchini humo. Hii si mara ya kwanza kwa ndege za Uturuki kuvuka mipaka yake na kutekeleza hujuma zake nje ya nchi hiyo, suala ambalo limekuwa likilaaniwa na serikali kuu ya Baghdad.

MAHAKAMA KENYA YAFUTA KIFUNGU CHA MATUSI KATIKA SHERIA YA MTANDAO YA NCHI HIYO.


Mahakama Kuu jijini Nairobi imeamua kwamba Kifungu cha Sheria ambacho kimekuwa kikitumiwa kuwafungulia mashtaka watu kuhusiana na ujumbe kwenye simu na mitandao ya kijamii Kenya ni haramu.
Jaji wa Mumbi Ngugi alisema kifungu hicho, cha kutumia vibaya kifaa cha mawasiliano, kinakiuka katiba.
Kifungu hicho nambari 29 katika Sheria ya Habari na Mawasiliano Kenya Nambari 3 ya 1998 hupendekeza faini ya Sh50,000 au kifungo cha miezi mitatu jela, au adhabu zote mbili, kwa mtu anayepatikana na hatia.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Mwanasheria Mkuu walikuwa wametetea sheria hiyo wakisema ililenga kulinda sifa za wengine.
Jaji Ngugi alisema maelezo ya kifungu hicho ni mapana sana na pia baadhi ya makosa yanayolengwa kwenye kifungu hicho yameangaziwa katika sheria nyingine.
Aidha, alisema hakijatimiza matakwa ya Kipengele 24 cha Sheria ambacho kinaeleza ni katika hali gani ambapo haki za kimsingi zinaweza kubanwa. Aidha, alisema kifungu hicho kinakiuka Kipengele nambari 33 cha Katiba.
“Iwapo lengo ni kulinda sifa za watu wengine, basi hilo limeangaziwa kwenye sheria ya kuwaharibia sifa watu wengine,” Jaji Ngugi alisema kwenye uamuzi wake.
Jaji huyo alitaja mfano wa kesi tofauti dhidi ya mwanablogu mmoja ambaye aliamriwa kulipa Sh5 milioni na mahakama baada ya kushtakiwa chini ya sheria za kuwaharibia watu sifa.
Jaji Ngugi alikuwa akitoa uamuzi katika ombi la mwanablogu Geoffrey Andare aliyekamatwa Aprili 2015 na kufunguliwa mashtaka ya kutumia vibaya kifaa cha mawasiliano kutokana na ujumbe alioandika kwenye mitandao ya kijamii.
Mlalamishi alipinga mashtaka hayo akisema sheria hiyo inabana uhuru wa kujieleza mtandaoni.
Jaji alisema DPP hawezi kuendelea na kesi hiyo kwa msingi wa sheria hiyo.
Wakenya mtandaoni wamefurahia hatua hiyo ya Jaji Ngugi na tangu jana jioni jina lake limekuwa likivuma kwenye Twitter.
Kuna wanaomsifu kwa kutetea uhuru wa wananchi kujieleza lakini wengine wanahisi kwamba amekuwa akiharamisha vifungu vingi sana vya sheria.
Mfano ni Stephen Wambua anayesema uamuzi wa jaji huyo unafaa kuwekwa kwenye kitabu cha rekodi za dunia cha Guiness Book of World Records.

MAJASUSI WA ISRAELI WAUAWA GAZA.


Majasusi watano wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamehukumiwa adhabu ya kifo katika Ukanda wa Gaza.

Afisa mmoja wa mahakama ya Palestina amesema kuwa Mahakama Kuu ya Kijeshi ya Ukanda wa Gaza imewahukumu kifo wakazi watatu wa eneo hilo na wengine wawili wa kambi ya al Nasirati baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa maslahi ya Israel.

Hukumu hiyo imetolewa siku chache baada ya majasusi wengine kadhaa wa Israel kunyongwa katika eneo hilo la Ukanda wa Gaza.

Kabla ya shambulizi lolote dhidi ya watu wa Gaza, Israel imekuwa ikipokea habari za kijasusi kuhusu maeneo ya wapigania ukombozi wa Kipalestina kutoka kwa vibaraka wake katika eneo hilo na baadaye kushambulia eneo hilo linalozingirwa.

Vilevile ripoti zinasema kuwa, magari yanayotolewa kama zawadi au msaada na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa maafisa wa makundi ya mapambano ya Palestina yamegundulika kuwa na zana makhsusi za kufuatilia nyendo zao na kwamba Israel inatumia zana hizo kuwaua kigaidi viongozi na wanaharakati wa Palestina.

WANA NDOA WENYE SARATAN HUISHI MAISHA MAREFU ZAIDI KULIKO WASIO NA NDOA.

Utafiti wa Marekani waonesha ndoa inasaidia kurefusha wagonjwa wa saratani

Utafiti uliotolewa katika jarida la Saratani la Marekani umeonesha kuwa wagonjwa wa saratani waliofunga ndoa wanaweza kuishi maisha marefu zaidi kuliko wale wasiofunga ndoa.
Watafiti kutoka taasisi ya kinga ya saratani ya jimbo la California ya Marekani na chuo kikuu cha California walitafiti watu wazima laki 8 hivi waliothibitishwa kupata saratani kutoka mwaka 2000 hadi 2009, na kufuatilia hali zao hadi kufikia mwaka 2012.
Matokeo yameonesha kuwa kiwango cha vifo cha wagonjwa wasiofunga ndoa ni juu kuliko waliofunga ndoa. Kati ya wagonjwa wa kiume, kiwango cha vifo cha wagonjwa wasiofunga ndoa ni asilimia 127 ya kile cha waliofunga ndoa; kwa upande wa wagonjwa wa kike, ni aislimia 119 ya kile cha waliofunga ndoa.

Watafiti wamesema, chanzo cha tofauti hiyo hakiwezi kuelezwa kwa hali ya kiuchumi ya wagonjwa, kama vile kama amenunua bima ya kiafya ama anaishi katika sehemu yenye hali nzuri ya kiuchumi.

Pia wamesema, uungaji mkono wa kijamii ni nguvu muhimu ya kurefusha maisha ya wagonjwa wa saratani. Hivyo ndoa inaleta athari nzuri kwa afya za wagonjwa hao. Watafiti wanashauri kuwa madaktari wanapowatibu wagonjwa wasiofunga ndoa, wanatakiwa kuuliza katika mtandao wao wa kijamii kama kuna mtu anayeweza kutoa msaada katika afya na saikolojia au la.

WAISLAMU UFARANSA WAZIDI KUBAGULIWA.


Utafiti mpya unaonesha kuwa, Waislamu nchini Ufaransa, wanazidi kubaguliwa kiasi kwamba wana nafasi ndogo sana ya kupata kazi ikilinganishwa na raia wengine wa nchi hiyo ya Ulaya.

Taasisi ya utafiti ya Montaigne imeripoti kuwa, fursa ya Waislamu ya kuweza kupata kazi wakati wa mahojiano ni ndogo sana ikilinganishwa na raia wa dini nyinginezo wa Ufaransa.

Serikali ya Ufaransa ambayo hadi hivi sasa imeshindwa kupambana na wimbi la fikra na misimamo mikali dhidi ya jamii ya Waislamu, imeanzisha kampeni maalumu inayojulikana kwa jina la "Uwezo Kwanza" ili kukabiliana na ubaguzi hasa katika sekta ya kuajiri watumishi wa umma. Kampeni hiyo inayoanza leo Jumanne inatarajiwa kudumu kwa muda wa siku 15.

Waziri wa Kazi wa Ufaransa, Myriam El Khomri amesema, ubaguzi wanaofanyiwa Waislamu nchini Ufaransa hauna uhusiano wa moja kwa moja na siasa za uajiri za serikali, lakini baadhi ya wakati kunachukuliwa misimamo nchini humo ambayo inawaathiri Waislamu.

Taasisi ya Montaigne ilianzishwa mwaka 2000 mjini Paris na wajumbe wa taasisi hiyo ni viongozi wa ngazi za juu wa mashirika, vyuo vikuu na wajumbe wa jamii ya kimataifa. Taasisi hiyo ya utafiti inafanya kazi ya kutathmini siasa za serikali ya Ufaransa, masuala ya kiuchumi pamoja na mifungamano ya kijamii.

Ufaransa ina karibu Waislamu milioni tano ikiwa ndiyo nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu barani Ulaya.

WAKRISTO WAJIFUNZA UISLAMU KATIKA MAKANISA HUKO MAREKANI.


Licha ya kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani, baadhi ya makanisa ya nchi hiyo yameamua kuitisha vikao mbalimbali vya kujifunza na kuutambua vizuri Uislamu.
Shirika la habari la RASA liliripoti jana Jumatatu kwamba, makanisa ya mji wa Albuquerque katika jimbo la New Mexico huko Marekani, wameandaa ratiba maalumu za kuutambulishwa Uislamu kwa wafuasi wa dini nyinginezo hususan Wakristo.

Ratiba hizo ambazo zimepata umaarufu wa jina la Hotuba za Wanawake Waislamu, wanawake wa tamaduni na dini tofauti wameamua kukusanyika katika makanisa na kujifunza, kuuliza maswali na kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu Uislamu ikiwa ni pamoja na kuhusiana na maisha ya Waislamu hususan wanawake Waislamu wa Marekani.

Imepangwa kuwa, ratiba kama hizo zifanyike pia katika makanisa mengine matatu ya jimbo hilo.

Chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka sana huko Marekani, suala ambalo limewafanya wafuasi wa dini nyinginezo hasa Wakristo wadadisi na wapate hamu ya kuujua zaidi Uislamu kutoka kwa Waislamu wenyewe.

WATU 38 WAFA KWA MAFURIKO HUKO AFGHANISTAN.


Watu wasiopungua 38 wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali iliyonyesha maeneo ya kaskazini mwa Afghanistan.

Maafisa wa serikali ya Afghanistan wamesema vifo hivyo vimeripotiwa katika mikoa ya kaskazini ya Takhar, Badghis na Samangan katika mafuriko yaliyoanza Jumapili usiku.

Mkurugenzi wa majanga ya kimaumbile katika mkoa wa Takhar, Abdul Razaq Zinda, amesema watu 13 wakiwemo watoto walifariki katika wilaya za Kalafgan na Bangi.

Aidha amesema, nyumba kadhaa hasa zile zilizojengwa kwa matofali ya udongo ziliharibiwa na mvua kali.

Msemaji wa polisi ya mkoa wa Badghis amesema watu 19 walifariki wilayani Muqur.

Mafuriko yameua pia watu wengine sita ambao ni wanawake watatu na watoto watatu mkoani Samangan na kubomoa nyumba zipatazo 20 na ekari zisizopungua tano za kilimo.

Mvua kali zimeukumba mji mkuu wa Afghanistan, Kabul lakini hakuna maafa makubwa yaliyoripotiwa.

ISRAELI YATETEA KITENDO CHAKE CHA KUKALIA MIUNUKO YA GOLAN YA SYRIA.


Licha ya kuweko upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya umiliki wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa eneo la miinuko ya Golan ya Syria unayoikalia kwa mabavu, lakini Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu amedai kuwa, miinuko hiyo ya Golan daima itakuwa sehemu isiyotenganishika na utawala huo.

Akizungumza siku ya Jumapili katika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika kwa mara ya kwanza katika eneo la miinuko ya Golan, Benjamin Netanyahu sanjari na kusisitiza juu ya mamlaka ya utawala huo kwa eneo hilo la Syria amesema kuwa, katu Israel haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya kimataifa.

Akiendelea na matamshi yake ya kichochezi kuhusiana na miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel Netanyahu ameitaka jamii ya kimataifa iutambue rasmi umiliki wa Israel kwa miinuko hiyo.

Utawala ghasibu wa Israel uliikalia kwa mabavu sehemu ya miinuko ya Golan ya Syria mwaka 1967 katika vita vyake na Waarabu. Mwaka 1981, utawala huo wa kimabavu uliiunganisha sehemu hiyo na ardhi unazozikalia kwa mabavu, hatua ambayo hakuna wakati ilitambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa.

Matamshi hayo ya Netanyahu anayatoa katika hali ambayo, hivi karibuni vyombo vya habari vya Israel vimeripoti mara kadhaa kuhusiana na kihoro na wasiwasi wa viongozi wa utawala huo juu ya kurejea eneo hilo katika milki ya Syria.

Sambamba na duru mpya ya njama za Israel za kutaka kujitanua na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Mashariki ya Kati, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imemwandikia barua Katibu