TETEMEKO LINGINE LIMETOKEA JAPANI.

TETEMEKO LINGINE LIMETOKEA JAPANI.

Tetemeko lignine la ardhi lenye nguvu ya 7.3 kwenye vipimo vya Richter limetokea nchini Japan na kuuwa watu 19 na kusababisha uharibifu mkubwa hayo ni kwa mujibu wa mamlaka nchini humo.  

Tetemeko hilo  lilikukumba kisiwa cha Kyushu ndani ya siku mbili, na kusa sababisha kuporomoka kwa majengo, barabara, mifumo ya maji na umeme.
Wanajeshi 20,000 wametumwa kusaidia juhudi za uokoaji lakini jitihada za uokoaji zimetatizwa na mitetemeko mingine midogo midogo.

Hivi majuzi lilitokea tetemeko Kumamoto hukohuko Japan na kuleta uharibufu na kuua watu, hili sasa lingine, nchi ya Japan inakumbwa na majanga haya kwa mara na kupelekea nchi hiyo kuwa na sheria kali za ujenzi.

GAVANA HUKO MAREKANI ALIGIZA HELKOPTA KUBEBA WALLETI YAKE.


Helikopta ya polisi ilitumwa kuchukua pochi ya gavana wa jimbo moja nchini Marekani, safari iliyogharimu $4,000 (£2,800), uchunguzi umebaini.

Kisa hicho kilitokea mwishoni mwa 2014.
Gavana wa Alabama Robert Bentley aliondoka Tuscaloosa kuelekea kwenye nyumba yake ya ufukweni, mwendo wa saa tano hivi ukitumia gari, lakini akasahau pochi yake.

Aliwataka maafisa wake wa usalama kwenda kuchukua pochi hiyo. Maafisa hao walitumia helikopta hiyo ya polisi, rekodi za safari za ndege zimeonesha.
Bw Bentley anakabiliwa na shinikizo za kumtaka ajiuzulu kutokana na sakata ya unyanyasaji wa kingono.

Lakini anasema hakuagiza ndege itumiwe kwenda kuchukua pochi.
"Niliwaomba tu waende wakachukue pochi yangu, sikuwaambia watumie njia gani,” gavana huyo ameambia mtandao wa AL.com.

„Sikuwaambia watumie helikopta. Ni lazima uwe na pochi yako kwa sababu za kiusalama. Mimi ni gavana. Na ni lazima niwe na pesa. Ni lazima ningenunua kitu cha kula. Na nilihitaji vitambulisho vyangu.”

Tovuti ya AL.com inasema safari hiyo ya helikopta iligharimu mlipa kodi takriban $4,000 (£2,800).

IRAN YAJITAMBA KUWA NA JESHI IMARA NA LENYE NGUVU.

IRAN YAJITAMBA KUWA NA JESHI IMARA NA LENYE NGUVU.

Luteni Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Iran amesema kuwa, jeshi hilo liko imara katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Brigedia Jenerali Kiumars Heidari akisema hayo wakati huu wa kukaribia Siku ya Jeshi nchini Iran.

Ameongeza kuwa, jeshi la Iran halizembea hata sekunde moja kuulinda Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba kusimama kwake huko imara kunathibitishwa na jinsi jeshi hilo lilivyo na fakhari ya kutoa mashahidi 48 elfu katika njia ya haki.

Brigedia Jenerali Kiumars Heidari ameongeza kuwa, jeshi la Iran lina tofauti kubwa na majeshi ya nchi nyingine duniani na kusisitiza kuwa, leo hii jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limekuwa mtetezi mkubwa wa wanyonge na watu wanaodhulumiwa duniani na limesimama imara kukabiliana na waistikbari na mabeberu na ndio maana linapendwa na linakubalika.

Ikumbukwe kuwa kesho Jumapili inayosadifiana na tarehe 17 Aprili ni siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa ratiba tofauti.

MALALAMIKO YA WAZIMBABWE KWA SIASA ZA MUGABE.


Wananchi wa Zimbabwe wamefanya maandamano kulalamikia siasa za Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo.
Karibu wafuasi elfu mbili wa chama cha upinzani cha MDC cha Morgan Tsvangirai wamefanya maandamano mjini Harare kulalamikia siasa za Rais Robert Mugabe. Akizungumza mbele ya wafuasi wake Tsvangirai amesisitiza kuwa, Mugabe ameshindwa kutatua mgogoro wa nchi hiyo na kwamba wananchi wa Zimbabwe wanaamini kuwa, serikali yake haina njia nyingine ila kuporomoka tu.

Robert Mugabe ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 92, amekuwa rais wa Zimbabwe tangu mwaka 1980. Hali yake tete ya kiafya imepelekea kuzuka maneno mengi kuhusu mtu wa kurithi kiti chake. Kumekuwa na dhana kuwa, Mugabe anafanya mpango wa kumrithisha kiti hicho mkewe, Grace Mugabe. Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Machi, Mugabe alikanusha uvumi huo na kusisitiza kuwa, rais ajaye wa Zimbabwe lazima achaguliwe kwa njia za kidemokrasia.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, matamshi hayo ya Mugabe yanaashiria azma yake ya kuendelea kuwa rais wa Zimbabwe hadi mwisho wa maisha yake. Katika hali ambayo duru za kisiasa za nchi hiyo zinafuatilia kwa karibu sana hali ya kiafya ya Mugabe, baadhi ya duru hizo zinaamini kuwa, hatua ya Mugabe ya kushindwa kuainisha mrithi wake itazidi kuitumbukiza katika mgogoro nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Hivi sasa hali ya kiuchumi ya Zimbabwe ni ya mgogoro kiasi kwamba baadhi ya ripoti zinaonesha kuwa Zimbabwe ndiyo nchi maskini zai

MAKUMI YA RAIA WAMETIWA MBARONI KWA MAANDAMANO KUMPINGA RAIS WA GAMBIA.


Makumi ya raia wametiwa mbaroni nchini Gambia katika maandamano yaliyofanyika jana ya kumpinga Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo.
Jana maelfu ya wananchi wa Gambia walifanya maandamano wakimpinga Rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh.

Maandamano hahayo yalikandamizwa na vikosi vya usalama huku makumi ya waandamanaji wakitiwa mbaroni. Habari kutoka Gambia zinasema kuwa, maandamano hayo ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

Waandamanaji wakiwa wamebeba mabango na maberamu walipiga nara wakipinga sera za Rais huyo na kutoa wito wa kufanyika mageuzi ya kisiasa.

"Wananchi wa Gambia Wanataka Mageuzi ya Kisiasa" ni moja ya maandishi yaliyoonekana katika maberamu yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao. Baadhi ya waandamanaji hao wamesema kuwa, Rais jammeh ndio sababu ya hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili nchi hiyo.

Baadhi ya waandamaji waliotiwa mbaroni wanaripotiwa kupigwa na kuteswa na vikosi vya usalama baada ya kutiwa mbaroni.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, Rais Yahya Jammeh aliyekuwa nchini Uturuki kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC amekatisha safari yake yake hiyo na kurejea Gambia.

Rais Jammeh amekuwa akiongoza Gambia kwa mkono wa chuma tangu mwaka 1994.

UNICEF: BOKOHARAM INAWATUMIA KINGONO WASICHANA WA CHIBOK

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, anayehusika na masuala ya magharibi na katikati mwa Afrika amesema kuwa, wasichana wanaoshikiliwa na kundi la Boko Haram wanabakwa na kudhalilishwa kijinsia na wanamgambo wa kundi hilo.

Manuel Fontaine amesema hayo leo na kuongeza kuwa, wanawake na wasichana wanaotoroka kutoka mikononi mwa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu, wameelezea namna wanachama wa kundi hilo walivyokuwa wakiwabaka na kuwalazimisha kutenda vitendo vya ngono bila ya wao kupenda. Kwa mujibu wa wasichana hao, makamanda wa genge hilo walikuwa pia wakiwapatia mafunzo ya kujiripua kwa mabomu. Hii ni katika hali ambayo, ripoti zilizotolewa mwezi Mei mwaka jana zilieleza kuwa, robo tatu ya mashambulio yaliyofanywa na kundi la Boko Haram kuanzia mwaka 2014, yalifanywa na watoto wadogo waliopatiwa mafunzo na magaidi hao.

Ni miaka miwili sasa imepita tangu magaidi hao walipowateka nyara wasichana wa shule moja ya serikali katika mji wa Chibok, kaskazini mashariki mwa Nigeria, huku jamii ya kimataifa ikitaka kuachiliwa huru mara moja wasichana hao.

WAPELISTINA WAANDAMANA KUPINGA UKATILI WA ISRAELI.


Wapalestina wa maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wamefanya maandamano makubwa ya kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mwandishi wa shirika la habari la IRIB ameripoti kuwa, jana Ijumaa mamia ya wananchi wa Palestina walifanya maandamano katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wakiutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi wanazoporwa Wapalestina.

Waandamanaji hao walipiga nara dhidi ya ya Israel na wametangaza uungaji mkono wao kwa muqawama na Intifadha ya kupambana na utawala wa Kizayuni.

Wanajeshi wa Israel waliwavamia na kuwashambulia kwa risasi waandamanaji hao na kujeruhi Wapalestina kadhaa.

Wakati huo huo mamia ya Wapalestina wamekusanyika mbele ya jengo la Shirika la Msalaba Mwekundu katika Ukanda wa Ghaza wakitaka kuachiliwa huru Wapalestina wenzao wanaoshikiliwa mateka na utawala wa Kizayuni.

Hivi sasa kuna karibu Wapalestina elfu saba wanaoshikiliwa mateka na utawala wa Kizayuni wa Israel katika jela za kuogofya za utawala huo dhalimu.

MISRI: MAANDAMANO YA WANANCHI TISHIO KWA SERIKALI.


Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetaka polisi kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kuzima kwa njia yoyote ile, maandamano ya wananchi wanaopinga hatua ya Rais Abdel Fattah el-Sisi kumpa visiwa viwili vya nchi hiyo Mfalme Salman wa Saudi Arabia.

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema kuwa, kufuatia amri hiyo, polisi wameimarisha doria katika kila kona na barabara kubwa, kwa lengo la kuzuia maandamano hayo ya wananchi. Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita, Wizara hiyo ya Mambo ya ndani ya Misri ilionya juu ya kuendelezwa maandamano hayo ya kupinga kitendo cha rais wa nchi hiyo cha kuipa Saudia visiwa viwili vya Sanafir na Tiran vilivyoko katika Ghuba ya Aqaba.

Jana pia maandamano makubwa yalifanyika katika maeneo tofauti ya Misri, ambapo polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Inafaa kuashiria hapa kwamba, hivi karibuni serikali ya majenerali wa kijeshi ya Misri imeipa serikali ya Saudia visiwa hivyo viwili vya Bahari Nyekundu kwa madai kuwa, upimaji mipaka uliofanywa umeonyesha kuwa, tangu awali visiwa hivyo vilikuwa katika maji ya Saudia, suala ambalo limetajwa na Wamisri kuwa ni usaliti. Tayari vyama na harakati za kisiasa nchini Misri kwa pamoja vimelaani vikali udhaifu wa Rais Abdel Fattah el-Sisi mbele ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia.

UISLAMU NA UKRISTO UMEWATIA UJINGA WAAFRIKA.


Pamoja na uislamu wangu, lakini sitaweza kubeza au kudharau mila na desturi yangu ya kiafrika.

Kuna watu wana mawazo kitumwa, kikoloni, na kijinga, kwao wao uafrika na mila zake ni ushenzi na dalili ya kutokusoma na kustaharabika.

Mtu anabeza na kumdharau na kumuona mshenzi au shirikina mvaa hirizi, lakini anamuona mstaharabu na mwenye maana sana mtembea na bible au quran kwapani. Hivi anayekwenda kuomba kanisani apate kazi ana tafauti gani na yule anayekwenda mzimuni kufanya hivyo pia?

Hivi mchungaji anaposema na kutabiri juu ya kesho au anapoona mambo yako ya rohoni ana tafauti gani babu au bibi yangu wa mzimuni anayetabiri kwa mizimu? Kwanini utabiri wa mzimuni uitwe ramli na ushetani lakini utabiri wa kanisani uitwe maono na utukufu? Kwanini?

Alikadhalika yule mwenye kutambika katika mizimu ama miungu ya kwao anaonekana ni mtu wa kizamani au mtu anaye ishi maisha ya kijima, maisha kale, lakini yule anayekesha msikitini au kanisani ndio mjanja na mtu aliyestaharibika. Eeh Afrika yangu, nalia uafria wangu, hivi kuna tafauti gani kati ya kukesha msikitini na kukesha mzimuni?

Kuna tafauti gani ya kwaya na mapambio ya kumsifu Yesu na madogori au lewa za kwetu? Hivi nini hasa tafauti? Kama tafauti ni moja, hizi kwaajili ya Yesu na zile kwaajili ya Mizimu, lakini lengo na matarajio ni yaleyale. Anayekwenda mzumuni kuomba baraka hana tafauti na mwenda kanisani kuomba baraka. Kama tafauti ni moja kanisani anaombwa Yesu na mzimuni anaombwa mzimu, lakini matarajio ni yaleyale.

Kwa jinsi waafrika tunavyo zipamba, na kuzipigania dini za kigeni imepita kiasi wenye dini zao watuone wajinga, wapumbavu, na watu tusio kuwa na asili wala kwetu. Waafrika wa nchi ya AFRIKA YA KATI wameuana kisa uislamu na ukristo, huko Nigeria hakuna salama kisa uislamu na ukristo, hivi ninyi waafrika ni wapi wazungu wanapigana vikumbo sababu ya uafrika? kwanini sisi tuwe tunajipendekeza kwao kwa kiwango hiki?

Sema msemavyo, lakini hakuna anayepinga hapa kuwa ukristo ni utamaduni wa kizungu, Yesu katiwa mle tu ili watu wengi wavutike, pia uislamu utamaduni wa kiarabu na uyaudi wenyewe wayaudi. Kama Afrika tungetawaliwa na mchina au mhindu, sasa hivi tungekuwa mabudha au wahindu, yaani, ni bendera fuata upepo, ng'ombe ambaye kitoweo kwetu angekuwa Mungu wetu na tungejitoa muhanga kupambana na wala ng'ombe, sisi tunafuata matakwa ya wanao tutawala.

Wewe huna utamaduni wako kiasi ukubali kujitoa mhanga kisa dini? kiasi udharau uafrika wako na utamaduni wako? Nilisikitika sana Mzee Kingunge alivyokwenda kuwakilisha dini za jadi bunge la katiba watu katika mitandao walimdhihaki kwa maneno ya hovyo kabisa, lakini wakati huohuo katika bunge hilo kulikuwa na mashekhe na mapadri walio wakalisha dini zao na hakuna yeyote aliyethubutu kuwasumbua, tena watanzania wa dini hizi mbili walitamani bunge la katiba lijae mashekhe na mapadri kama vile tunaenda kuandika MSETO WA QURAN NA BIBLIA.

Pia naomba mjue hakuna uhusiano wowote kati ya mauaji ya vikongwe, albino na mambo ya kufananayo na dini za asili au tambiko za mzimuni. Hiyo ni sawa na Padri au Shekhe kuwa shoga kisa ukauhukumu uislamu au ukristo wote kwa kosa moja la ushoga. Na hata ukichunguza dini za uslamu na ukristo zimepoteza maisha ya watu wengi sana hadi kukufikia wewe, wapo waliotolewa sadaka na Mungu wa kikristo ili ukristo ukufikie, kwa hivyo utagundua dini zote zina historia mbaya ya kutoa kafara za ajabu na kutoa adhabu za kuua, kafara na adhabu ambazo kwa wakati wetu huu ni kinyume cha utu na ubinadamu.

Acheni dharau, acheni ujinga, acheni ulimbukeni, acheni upumbavu!

WAAFRIKA TUNA MAMBO.                                           
1.
Mwajua mimi sijambo, namshukuru manani,
Nimeamka kitambo, shafika kibaruani,
Ila kuna kubwa jambo, kuuliza natamani,
Hivi nyie hamjambo? Mliopo kisimani.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
2.
Mambo yakiwa si mambo, siweke fundo moyoni,
Kubwa sicheke utumbo, kwa maini ya jirani,
Sitaki ule makombo, kwa hamu ya biriani,
Bure taitwa mtambo, mwenye wazimu rasini.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
3.
Kuna mambo ya mkumbo, kuyafuata acheni,
Mambo mengine urimbo, mchunge siwanaseni,
Kijana kimbie ng'ambo, nchini abaki nani?
Mwisho apigwe taimbo, kwa bata za ghaibuni.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
4.
Memkumbuka Setembo, babu yangu wa moyoni,
Aliniusia mambo, kuwa'mbia natamani,
Rijali haumwi tumbo, wala chango kinenani,
Hakika hafanyi tambo, bila vitendo jueni,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
5.
Nawasema wa kiambo, hata wale wa mjini.
Mlioamkia tembo, mloiota ndotoni,
Hamkuogeshwa jimbo, wakati wa utotoni,
Sawa mfanye utumbo, subuhi mko hewani,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
6.
Twasisitiza kimombo, kiswahili taabani,
Vizuri kuiga mambo, si kila kitu jamani,
Sawa kuacha kiyombo, kwa suti za Marekani,
Kukiabudu kimombo, ni wazimu jueni.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
7.
Kanisani kuna mambo, pia na msikitini,
Tuna itukana gombo, nalia utamaduni,
Miungu kutoka ng'ambo, Ulaya na Arabuni,
Imetupiga kikumbo, jadi haina thamani,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
8.
Tufani yapiga sambo, istizai yafaani,
Mjue twaenda kombo, naomba zindukeni,
Sote tumelewa tembo, kutoka ughaibuni,
Sasa ni wana wa kambo, baba wa kijerumani
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
9.
Nimesema kimafumbo, hilo kwanza lijueni,
Maneno haya si shombo, ukutani andikeni,
Msiyafiche kwa rambo, hadharani yawekeni,
Jeuri ataka fimbo, awekwe sawa jamani,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
10.
Nimeliza la mgambo, lengo mtoke shimoni,
Ninawaita kwa wimbo, wahafidhina njooni,
Mwanagenzi nina mambo, majagina nifunzeni,
Naomba nifunge gombo, nilosema yashikeni,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0622845394/0762845394
Morogoro Tanzania.