WAPELISTINA WAANDAMANA KUPINGA UKATILI WA ISRAELI.


Wapalestina wa maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wamefanya maandamano makubwa ya kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mwandishi wa shirika la habari la IRIB ameripoti kuwa, jana Ijumaa mamia ya wananchi wa Palestina walifanya maandamano katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wakiutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi wanazoporwa Wapalestina.

Waandamanaji hao walipiga nara dhidi ya ya Israel na wametangaza uungaji mkono wao kwa muqawama na Intifadha ya kupambana na utawala wa Kizayuni.

Wanajeshi wa Israel waliwavamia na kuwashambulia kwa risasi waandamanaji hao na kujeruhi Wapalestina kadhaa.

Wakati huo huo mamia ya Wapalestina wamekusanyika mbele ya jengo la Shirika la Msalaba Mwekundu katika Ukanda wa Ghaza wakitaka kuachiliwa huru Wapalestina wenzao wanaoshikiliwa mateka na utawala wa Kizayuni.

Hivi sasa kuna karibu Wapalestina elfu saba wanaoshikiliwa mateka na utawala wa Kizayuni wa Israel katika jela za kuogofya za utawala huo dhalimu.

MISRI: MAANDAMANO YA WANANCHI TISHIO KWA SERIKALI.


Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetaka polisi kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kuzima kwa njia yoyote ile, maandamano ya wananchi wanaopinga hatua ya Rais Abdel Fattah el-Sisi kumpa visiwa viwili vya nchi hiyo Mfalme Salman wa Saudi Arabia.

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema kuwa, kufuatia amri hiyo, polisi wameimarisha doria katika kila kona na barabara kubwa, kwa lengo la kuzuia maandamano hayo ya wananchi. Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita, Wizara hiyo ya Mambo ya ndani ya Misri ilionya juu ya kuendelezwa maandamano hayo ya kupinga kitendo cha rais wa nchi hiyo cha kuipa Saudia visiwa viwili vya Sanafir na Tiran vilivyoko katika Ghuba ya Aqaba.

Jana pia maandamano makubwa yalifanyika katika maeneo tofauti ya Misri, ambapo polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Inafaa kuashiria hapa kwamba, hivi karibuni serikali ya majenerali wa kijeshi ya Misri imeipa serikali ya Saudia visiwa hivyo viwili vya Bahari Nyekundu kwa madai kuwa, upimaji mipaka uliofanywa umeonyesha kuwa, tangu awali visiwa hivyo vilikuwa katika maji ya Saudia, suala ambalo limetajwa na Wamisri kuwa ni usaliti. Tayari vyama na harakati za kisiasa nchini Misri kwa pamoja vimelaani vikali udhaifu wa Rais Abdel Fattah el-Sisi mbele ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia.

UISLAMU NA UKRISTO UMEWATIA UJINGA WAAFRIKA.


Pamoja na uislamu wangu, lakini sitaweza kubeza au kudharau mila na desturi yangu ya kiafrika.

Kuna watu wana mawazo kitumwa, kikoloni, na kijinga, kwao wao uafrika na mila zake ni ushenzi na dalili ya kutokusoma na kustaharabika.

Mtu anabeza na kumdharau na kumuona mshenzi au shirikina mvaa hirizi, lakini anamuona mstaharabu na mwenye maana sana mtembea na bible au quran kwapani. Hivi anayekwenda kuomba kanisani apate kazi ana tafauti gani na yule anayekwenda mzimuni kufanya hivyo pia?

Hivi mchungaji anaposema na kutabiri juu ya kesho au anapoona mambo yako ya rohoni ana tafauti gani babu au bibi yangu wa mzimuni anayetabiri kwa mizimu? Kwanini utabiri wa mzimuni uitwe ramli na ushetani lakini utabiri wa kanisani uitwe maono na utukufu? Kwanini?

Alikadhalika yule mwenye kutambika katika mizimu ama miungu ya kwao anaonekana ni mtu wa kizamani au mtu anaye ishi maisha ya kijima, maisha kale, lakini yule anayekesha msikitini au kanisani ndio mjanja na mtu aliyestaharibika. Eeh Afrika yangu, nalia uafria wangu, hivi kuna tafauti gani kati ya kukesha msikitini na kukesha mzimuni?

Kuna tafauti gani ya kwaya na mapambio ya kumsifu Yesu na madogori au lewa za kwetu? Hivi nini hasa tafauti? Kama tafauti ni moja, hizi kwaajili ya Yesu na zile kwaajili ya Mizimu, lakini lengo na matarajio ni yaleyale. Anayekwenda mzumuni kuomba baraka hana tafauti na mwenda kanisani kuomba baraka. Kama tafauti ni moja kanisani anaombwa Yesu na mzimuni anaombwa mzimu, lakini matarajio ni yaleyale.

Kwa jinsi waafrika tunavyo zipamba, na kuzipigania dini za kigeni imepita kiasi wenye dini zao watuone wajinga, wapumbavu, na watu tusio kuwa na asili wala kwetu. Waafrika wa nchi ya AFRIKA YA KATI wameuana kisa uislamu na ukristo, huko Nigeria hakuna salama kisa uislamu na ukristo, hivi ninyi waafrika ni wapi wazungu wanapigana vikumbo sababu ya uafrika? kwanini sisi tuwe tunajipendekeza kwao kwa kiwango hiki?

Sema msemavyo, lakini hakuna anayepinga hapa kuwa ukristo ni utamaduni wa kizungu, Yesu katiwa mle tu ili watu wengi wavutike, pia uislamu utamaduni wa kiarabu na uyaudi wenyewe wayaudi. Kama Afrika tungetawaliwa na mchina au mhindu, sasa hivi tungekuwa mabudha au wahindu, yaani, ni bendera fuata upepo, ng'ombe ambaye kitoweo kwetu angekuwa Mungu wetu na tungejitoa muhanga kupambana na wala ng'ombe, sisi tunafuata matakwa ya wanao tutawala.

Wewe huna utamaduni wako kiasi ukubali kujitoa mhanga kisa dini? kiasi udharau uafrika wako na utamaduni wako? Nilisikitika sana Mzee Kingunge alivyokwenda kuwakilisha dini za jadi bunge la katiba watu katika mitandao walimdhihaki kwa maneno ya hovyo kabisa, lakini wakati huohuo katika bunge hilo kulikuwa na mashekhe na mapadri walio wakalisha dini zao na hakuna yeyote aliyethubutu kuwasumbua, tena watanzania wa dini hizi mbili walitamani bunge la katiba lijae mashekhe na mapadri kama vile tunaenda kuandika MSETO WA QURAN NA BIBLIA.

Pia naomba mjue hakuna uhusiano wowote kati ya mauaji ya vikongwe, albino na mambo ya kufananayo na dini za asili au tambiko za mzimuni. Hiyo ni sawa na Padri au Shekhe kuwa shoga kisa ukauhukumu uislamu au ukristo wote kwa kosa moja la ushoga. Na hata ukichunguza dini za uslamu na ukristo zimepoteza maisha ya watu wengi sana hadi kukufikia wewe, wapo waliotolewa sadaka na Mungu wa kikristo ili ukristo ukufikie, kwa hivyo utagundua dini zote zina historia mbaya ya kutoa kafara za ajabu na kutoa adhabu za kuua, kafara na adhabu ambazo kwa wakati wetu huu ni kinyume cha utu na ubinadamu.

Acheni dharau, acheni ujinga, acheni ulimbukeni, acheni upumbavu!

WAAFRIKA TUNA MAMBO.                                           
1.
Mwajua mimi sijambo, namshukuru manani,
Nimeamka kitambo, shafika kibaruani,
Ila kuna kubwa jambo, kuuliza natamani,
Hivi nyie hamjambo? Mliopo kisimani.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
2.
Mambo yakiwa si mambo, siweke fundo moyoni,
Kubwa sicheke utumbo, kwa maini ya jirani,
Sitaki ule makombo, kwa hamu ya biriani,
Bure taitwa mtambo, mwenye wazimu rasini.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
3.
Kuna mambo ya mkumbo, kuyafuata acheni,
Mambo mengine urimbo, mchunge siwanaseni,
Kijana kimbie ng'ambo, nchini abaki nani?
Mwisho apigwe taimbo, kwa bata za ghaibuni.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
4.
Memkumbuka Setembo, babu yangu wa moyoni,
Aliniusia mambo, kuwa'mbia natamani,
Rijali haumwi tumbo, wala chango kinenani,
Hakika hafanyi tambo, bila vitendo jueni,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
5.
Nawasema wa kiambo, hata wale wa mjini.
Mlioamkia tembo, mloiota ndotoni,
Hamkuogeshwa jimbo, wakati wa utotoni,
Sawa mfanye utumbo, subuhi mko hewani,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
6.
Twasisitiza kimombo, kiswahili taabani,
Vizuri kuiga mambo, si kila kitu jamani,
Sawa kuacha kiyombo, kwa suti za Marekani,
Kukiabudu kimombo, ni wazimu jueni.
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
7.
Kanisani kuna mambo, pia na msikitini,
Tuna itukana gombo, nalia utamaduni,
Miungu kutoka ng'ambo, Ulaya na Arabuni,
Imetupiga kikumbo, jadi haina thamani,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
8.
Tufani yapiga sambo, istizai yafaani,
Mjue twaenda kombo, naomba zindukeni,
Sote tumelewa tembo, kutoka ughaibuni,
Sasa ni wana wa kambo, baba wa kijerumani
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
9.
Nimesema kimafumbo, hilo kwanza lijueni,
Maneno haya si shombo, ukutani andikeni,
Msiyafiche kwa rambo, hadharani yawekeni,
Jeuri ataka fimbo, awekwe sawa jamani,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.
10.
Nimeliza la mgambo, lengo mtoke shimoni,
Ninawaita kwa wimbo, wahafidhina njooni,
Mwanagenzi nina mambo, majagina nifunzeni,
Naomba nifunge gombo, nilosema yashikeni,
Nawambia si utani. waafrika tuna mambo.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0622845394/0762845394
Morogoro Tanzania.

KOREA KASKAZINI YASHINDWA KUFYATUA MAKOMBORA YAKE YA MASAFA YA WASTANI.


Jaribio la Korea Kaskazini kufyatua kombora la masafa ya wastani kwa jina “Musudan” katika pwani yake ya mashariki, limeshindwa, hayo ni kulingana na, maafisa wa Marekani na Korea Kusini

Shughuli hiyo ilikuwa ikifanyika siku ambayo ni ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taifa la Korea Kaskazini Kim Il-sung.

Shirika la habari la Korea Kusini Yonhap, likinukuu duru za serikali, limesema kombora hilo lilikuwa aina ya kombora la Musudan, ambalo kitaalamu hujulikana kama BM-25.

Makombora hayo yanaweza kufika umbali wa kilomita 3,000 na kufikia kambi ya majeshi ya Marekani iliyopo kisiwa cha Guam katika bahari ya Pasifiki. Hata hivyo hayawezi kufika Marekani bara.

Hayo ni makombora ya masafa ya wastani, makombora yake ya masafa marefu yanaweza kufika Marekani, hii ina maanisha Korea Kaskazini inaweza kumchapa Mmarekani bila kuhitaji msaada wa uwanja au bahari ya nchi yeyote na Marekani.

Kama mtakumbuka, Marekani ilipigana vita Iraq kwa msaada wa nchi kama Jordan ambazo zilitoa anga na viwanja kwaajili ya matumizi ya kijeshi kwa wamarekani, kama si msaada huo vita ya Iraq isingekuwa nyepesi kwa Marekani.

Marekani na Korea Kusini ndio wanasema hilo Jaribio la Kaskazini limefeli, lakini huwez jua, bado hatuna taarifa kutoka kaskazini, sababu hii huenda ni propaganda tu za Marekani Korea Kusini.

Tusubiri Tuone.


AFIKISHWA KIZIMBANI KWA KUMTUKANA RAIS MAGUFULI FACEBOOK.




KUMAMOTO HALI BADO MBAYA.

KUMAMOTO HALI BADO MBAYA.

Watu tisa wamefariki baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuukumba mkoa wa Kumamoto kusini magharibi mwa Japan, huku zaidi ya watu 400 wakiwa wamekimbizwa hospitalini.

Tetemeko hilo lilikuwa na kipimo cha 6.4 katika vipimo vya Richter. Habari zinasema takriban watu 23,000 walitafuta hifadhi kwenye maeneo 350 mkoani humo.

NIGERIA YASISITIZA UDHARULA WA KUPAMBANA NA UGAIDI.

NIGERIA YASISITIZA UDHARULA WA KUPAMBANA NA UGAIDI.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imesisitiza udharura wa kuzidishwa ushirikiano unaohitajika kati ya nchi za eneo la magharibi mwa Afrika kwa ajili ya kupambana na kundi la Boko Haram.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, kundi la Boko Haram katika kipindi cha miezi iliyopita limepata pigo kubwa kutoka vikosi vya majeshi ya nchi za eneo la magharibi mwa Afrika lakini inasikitisha kuona kuwa, kundi hilo lingali linaendeleza hujuma za kigaidi.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imeongeza kuwa, maafisa usalama wa Nigeria, Chad na Niger hadi sasa wameshindwa kuratibu oparesheni za majeshi ya nchi hizo dhidi ya Boko Haram katika eneo hilo na hivyo kundi hilo limetumia vibaya nukta hiyo ya udhaifu.

Maafisa usalama wa nchi hizo tatu walikutana mwaka jana huko Abuja, Nigeria kwa lengo la kutathmini oparesheni zao za pamoja dhidi ya kundi la Boko Haram. Japokuwa kituo kikuu cha kundi la Boko Haram kiko huko kaskazini mashariki mwa Nigeria lakini kundi hilo limekuwa pia likifanya mashambulizi ya kigaidi katika nchi jirani.

Baadhi wa wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mapigano na mivutano ya ndani katika baadhi ya nchi za magharibi mwa Afrika kwa upande mmoja, na kutokuwepo uratibu baina ya nchi za eneo hilo kwa ajili ya kupambana kwa pamoja na magaidi hao ni miongoni mwa sababu za kutofanikiwa mapambano ya kuliangamiza kundi hilo.

Sisitizo la Nigeria juu ya udharura wa kuzidishwa ushirikiano baina ya nchi za magharibi mwa Afrika limetolewa huku kundi la Boko Haram likizidisha mashambulizi ya kigaidi katika nchi za eneo hilo licha ya jitihada zinazofanywa na najeshi ya nchi hizo za kukabiliana na wahalifu hao.

Katika kampeni zake za uchaguzi, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliahidi kuwa atakomesha uasi wa kundi la Boko Haram. Hata hivyo hadi sasa jeshi la Nigeria halijapata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya kundi hilo la kigaidi. Ni kutokana na hali hiyo ndipo weledi wa mambo wanaposisitiza kuwa, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano na uratibu wa pamoja kati ya nchi zote za magharibi mwa Afrika kwa ajili ya kung'oa mzizi wa kundi hilo la kigaidi.

Kundi la Boko Haram linaendelea kuwashikia mateka mamia ya wasichana wa shule waliochukuliwa na kundi hilo miaka miwili iliyopita. Jana Jumatano wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wataalamu wa haki za binadamu wa Afrika walitoa taarifa ya pamoja wakiashiria suala na kusema kuwa:

Imepita miaka miwili sasa ambapo wapiganaji wa kundi la Boko Haram wanaendelea kuwashikilia mateka wanafunzi wa kike wa shule ya Chibok na hadi sasa hakuna maendeleo ya aina yoyote ya kuweka wazi hali ya wanafunzi hao. Wataalamu hao wameitaka serikali ya Nigeria kuzidisha juhudi za kukomboa wasichana hao.

Kuongezeka kwa mashambulizi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuimarika na kupanuka zaidi harakati za makundi ya kigaidi hususan katika bara la Afrika lenye utajiri wa maliasili, maeneo ya kistratijia na hitilafu nyingi za kikabila na kikaumu kumeyafanya mataifa na nchi hizo zikabiliwe na tishio kubwa la makundi kama Boko Haram na al Shabab.

Ukweli ni kwamba makundi ya kigaidi yanatishia usalama wa kimataifa na si bara la Afrika pekee, kwa msingi huo kuna udharura wa kuchukuliwa hatua za kimataifa za kukabiliana na janga hilo lisilojua mipaka ya nchi au bara makhsusi.

HUKO BURUNDI AFISA WA CNDD-FDD AUAWA

HUKO BURUNDI AFISA WA CNDD-FDD AUAWA

Afisa wa chama tawala nchini Burundi ameuawa kwa kupigwa risasi, katika kile kinachoonekana ni wimbi la makabiliano ya kulipiza kisasi dhidi ya serikali.

Damien Barindambi, mshirikishi wa wilaya katika eneo la Mutimbuza amesema Phocas Bakaza, mwanachama wa chama tawala CNDD-FDD aliuawa kwa kufyatuliwa risasi jana jioni viungani mwa mji mkuu Bujumbura. Amesema kuwa, watu wawili wamekamatwa kutokana na hujuma hizo zinazoaminika ni za kulipiza kisasi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 400 wamekwishauawa hadi sasa, tokea Burundi itumbukie kwenye mgorogoro wa wenye kwa wenyewe Aprili mwaka jana. Wizara ya Usalama wa Umma nchini Burundi imetangaza kuendelea machafuko katika maeneo tofauti ya nchi, ambapo watu 46 wameuawa tokea mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 pekee.

Mwaka mmoja umetimia tangu Burundi itumbukie katika hali ya mchafukoge mwezi Aprili mwaka jana, kufuatia hatua ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena urais katika uchaguzi uliopita nchini humo.

MAREKANI NA NCHI ZINAZO MILIKI SILAHA ZA NYUKULIA WAPOKONYWE KUKIDHI TAKWA LA KILIMWENGU.

MAREKANI NA NCHI ZINAZO MILIKI SILAHA ZA NYUKULIA WAPOKONYWE KUKIDHI TAKWA LA KILIMWENGU.

Kupokonywa silaha za nyuklia Marekani na nchi nyingine zinazomiliki sialha hizo ni takwa na hitajio kuu la fikra za waliowengi ulimwenguni.

Gazeti la Resalat linalochapishwa mjini Tehran limeandika leo katika uchambuzi wake kuwa, kupokonywa silaha za nyuklia ni takwa ambalo nchi zinazomiliki silaha za aina hiyo, zikiongozwa na Marekani; zina hofu kubwa kuhusiana na mpango wa kutaka kutekelezwa hatua hiyo.

Gazeti la Resalat limeandika kuwa, kuwepo mamia ya vichwa vya nyuklia ni hatari kwa maisha ya mamilioni ya watu duniani na kwamba suala la kupokonya silaha za nyuklia linapasa kuwekwa katika ajenda ya kazi ya nchi mbalimbali duniani ili kudhamini usalama wa kimataifa.

Gazeti hilo linalochapishwa hapa Tehran limeendelea kuandika kuwa, nchi zinazomiliki silaha haribifu na zilizopigwa marufuku katika hatua yao inayokinzana waziwazi katika kikao cha hivi karibuni cha G-7 huko Hiroshima Japan, zimetaka kuwepo dunia pasina na silaha za nyuklia, katika hali ambayo nchi hizo hazistahiki kuzungumzia suala la kupokonywa silaha za nyuklia ulimwenguni.

Gazeti la Resalat limeongeza kuwa, hatua ya madola yanayomiliki silaha za nyuklia ya kutekelezwa miamala ya kindumakuwili kwa kupuuza maghala ya silaha za nyuklia yanayomilikiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, imeutia kiburi utawala huo na hivyo kutoheshimu taasisi yoyote ya kimataifa ukiwemo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).