NDONDO SI CHURURU

NDONDO SI CHURURU.                                  
 1
Ndondondo sio chululu, najua maneno yao,
Waona wamefaulu, ati silingani nao,
Tena waniita mbulu, nisitie guu kwao,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.

2
Nasemwa mvaa moja, mi kauka nikuvae,
Kutoka kwangu si haja, tuli nyumbani nikae,
Ati tafanya kiroja, kiasi wanikatae,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
3
Nami nitajikusuru, nitalima na miraba,
Kikubwa sitakufuru, tamuomba mungu baba,
Hata hivyo nashukuru, ninachopata si haba,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
4
Huwezi kupata kenda, bila kuanza moya,
Sijitii mbio kwenda, nachelea vunja taya,
Lolote waweza tenda, kwa paka hupati paya,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
5
Sikitaki cha kuiba, kilijaze tumbo langu,
Silipendi la kahaba, lisonisha hamu yangu,
Maovu hayawi tiba, kutibu kichomi changu,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.
6
Ingawa sijakinai, cha mtu sikitamani,
Hata niwe na nishai, sirukii cha jirani,
Nina dhiki sikatai, na mungu yupo jueni,
Nakubali si chururu, haba mwanzo wa kibaba.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania

MAAFISA 50 WAPIGWA STOP KUSAFIRI



















KAZI INAENDELEA
--------------------------------------
Raisi Magufuli amezuia maafisa 50 waliokuwa wasafiri kwa ajili
ya kwenda kushirika kwenye ziara ya Jumuiya ya Madola.
Badala yake ameruhusu maafisa wanne tu na kuokoa jumla ya
sh milioni 700 ambazo zingetumika kulipia posho za safari na
kugharamia ticket za ndege.
Chanzo:Nipashe

LOHA Patli Kamar Lambe Baa

 





Hii nyimbo inapatikana katika filamu inayoitwa LOHA, moja ya filamu maarufu na nzuri ya kihindi hata sasa. Ilichezwa mwaka 1987.



AGIZO LA RAIS LATEKELEZWA, VITANDA 500

Maagizo aliyotoa rais jana yatekelezwa leo,
Vitanda 500 na magodoro 500 vinashushwa Hospitali ya taifa muhimbili, hii ni baada ya rais kusema fedha zilizotengwa kwaajili ya sherehe jana Dodoma zitumike kwaajili ya kununua vitanda muhimbili.

REJEA HABARI HII.

Wabunge wamechangisha shilingi milioni 250 kutoka bank mbalimbali kwa ajili ya sherehe yao ya jana usiku.
Baada ya muheshimiwa Magufuli kupata habari hizo, akaagiza kwamba party ya leo usiku itumia shiling milioni kumi au kumi na tano tu. Pesa inayobakia ipelekwe Hospitali ya muhimbili ikanunue vitanda ili wagonjwa wasilale chini. Huu ni mwanzo mzuri, im begining to become proud of my president.








SIDHARAU, KAZI NI KAZI.

SIDHARAU, KAZI NI KAZI.
                                   
Uza dagaa mchele, piga na kibakubaku,
Wala hupigi kelele, puyanga huko na huku,
Mkeo apike mle, mwidu sitamani kuku.
Sidharau kazi yako, mie sikufai kitu.

Piga debe kwa matatu, mchana hata usiku,
Kwa mbwembwe uite watu, kwa taxi na tukutuku,
Wana wapate viatu, sisaahu na mabuku,
Sidharau kazi yako, mie sikufai kitu.

Lima shamba bila haya, sisononeke moyoni,
Kwa ngiri hupati paya, msufi hauna buni,
Sitegemee cha mbuya, wala sikitumaini,
Sidharau kazi yako, mie sikufai kitu.

Wizi si kazi jamani, utapeli wafaani?
Si kitamu ulimini, cha kuiba kwa jirani,
Hakistiri maungoni, cha kupora madukani,
Kazi ile ya halali, yenye kufaa jamii.


Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania

IWEJE KIMBUNGA KILE, KISHINDWE ZUA PAA.

IWEJE KIMBUNGA KILE,
KISHINDWE ZUA PAA.                                                            

1.
Msije dhani natunga, wala sisemi uwongo,
Nimekiona kimbunga, kimetikisa mjengo,
Samani zilijigonga, haukupona mlango,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
2.

Hewa ikawa mchanga, vumbi ndani ya jengo,
Watu wakatangatanga, kama wanasaka fungo,
Si pakazuka kisanga, fupa kapewa mapengo,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
3.

Uhodari wa kuchunga, na kupeta kwa ungo,
Sima imejaa chenga, umethibiti urongo,
Mtoto kapewa mwanga, shetwani ataka pungo,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
4.

Miti ilipoanguka, mwenyewe nikanong’ona
Paa lililotoboka, hivi leo litapona?
Bora lipate dondoka, kwani halifai tena,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
5.

Mwenzenu niliboboka, dua mbaya nikaomba,
Paa lipate dondoka, tuezeke upya nyumba,
Mzigo hautafika, kamba hizi za mgomba,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
6.

Pepo zimezoa nguo, hadi za maungoni,
Juba na mitandio, haikubaki mwilini,
Watu wakaanza mbio, za kujistiri jamani,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
7.

Ni sharia kuchutama, zinapokuvuka nguo,
Juha aweza inama, aende kim-binuo,
Tangu zama ni hekima, kuyastiri maeneo,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
8.

Chui wamekuwa ndama, kenge amekuwa swila,
Mla wali kala sima, aliyemacho kalala,
Shilingi haikuzama, meli ikawa chakula,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
9.

Nyoka kapata miguu, jongoo kapata macho,
Wajaenda lango kuu, moyoni hawana kicho,
Watateta na mkuu, tena pasina kificho,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?
10.

Lile sikio la kufa, si limepata mganga,
Moto umeshika sofa, hando liko na mchanga,
Hino yangu falsafa, kwa hoja nimeijenga,
Iweje kimbunga kile, kishindwe kuzua paa?

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5.)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0784845394/0762845394
Morogoro Tanzania

MCHAFUA WATU, HUCHAFUKA.

MCHAFUA WATU, HUCHAFUKA.                                                            
Kojoa ukojoavyo, hautafika mbinguni,
Na ufanye ufanyavyo, tone la mwisho guuni,
Wende mbio utakavyo, baya hurudi nyumbani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

Boboka ubobokavyo, mkono wangu shavuni,
Sitaonekana ovyo, mithili ya majinuni,
Sitashuka upendavyo, labda nipande thamani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

Chafua uchafuavyo, pasi na haya usoni,
Tabaki vile nilivyo, sichafuki asilani,
Dunia ndivyo ilivyo, hayana budi jamani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

We fusa ufusavyo, sikimbii mwangu ndani,
Sitaacha hivyohivyo, nitauchoma ubani,
Harufu ndivyo ilivyo, takuganda maungoni,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

We dhani udhaniavyo, sina baya mtimani,
Waelewa ndivyo sivyo, ungauliza nadhani,
Ninakujua ulivyo, hunipi tabu fatani,
Kila mchafua watu, huishia kuchafuka.

Dotto Chamchua Rangimoto (Njano5)
255762845394/255784845394
Mzalendo.njano5@gmail.com


SASA HAMSINI RASI, HAMSINI MAJINUNI.






















SASA HAMSINI RASI, HAMSINI MAJINUNI
                                               
1.
Niko na wino chupani, na ujiti mkononi,
Naandika ya moyoni, yalo nifika jamani,
Sikuwahi kuamini, kuna viumbe majini,
Visasili vya zamani, ndivyo nilivyodhani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni
2.
Naanzia mwishoni, nilipokaa jamvini,
Fatma bint Subiani, akipandishwa rasini,
Niliketi kitangani, na chano kiko pembeni,
Lewa iko kilingeni, yanapungwa malohani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
3.
Mloketi upenuni, na wa mbali sogeeni,
Muingie uwanjani, tuyapunge malohani,
Kiti apate amani, imtoke mitihani,
Alisema hadharani, Kachiki bint Ngonyani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
4.
Kachiki bint Ngonyani, aso mjua ni nani,
Wanasiasa nchini, na wauzaji sokoni,
Hufika kwake nyumbani, wapate ndele usoni,
Anaishi Magomeni, pale Kilosa Mjini,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
5.
Mshike vya mikononi, vilaji vya malohani,
Kitezo na zafarani, na udi wa malohani,
Manenane na ubani, na uvumba wa majini,
Shime viwepo chanoni, ni muhimu si utani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
6.
Maji ya zamda chupani, sanamaki ya kusini,
Uzire, giligilani, na vizimba vya barani,
Mafuta ya asumini, na mkongojo wa jini,
Ada za bint Sultani, visikose kitangani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni
7.
Rabi Mola Sultani, Muumba wa mitihani,
Raha, dhiki na huzuni, majaliwa ya Manani,
Ameumba mashetani, kwa siku ya ushetani?
Kaweka mwiba njiani, ili umchome nani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
8.
Niwe na mbawa tisini, nipae hata mbinguni,
Na nifike arshini, nitabaki kuwa chini,
Kudura haiwi chini, huwa juu tambueni?
Upatalo duniani, limeandikwa zamani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
9.
Fatma mwana wa jini, ndio wangu mtihani.
Kwani niko shubuani, sijui nifanye nini,
Habanduki ubavuni, wala hatoki rasini.
Nifanyeje wenzanguni, initoke mitihani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
10.
Nimezama vitabuni, kazi za wanazuoni,
Biblia na furukani, maandishi ya zamani,
Naitafuta yakini, iliyopo vitabuni.
Hukumu yake n’ nini, sijaipata jamani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
10.
Fatma wewe ni nani, na hasa wataka nini?
Vilaji vipo chanoni, sema sasa ya moyoni,
Au nichore baoni, nijue ya ghaibuni?
Wewe ni wa baharini, au wale wa barani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
11.
Haya sasa sogeeni, msikie ya moyoni,
Ninayo mengi mtimani, yalo nifika zamani,
Sitochora ubaoni, kusema ya kifuani,
Haya yangu ya nguoni, wa kuyasema jirani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
12.
Ninayo mengi mtimani, yalo nifika zamani,
Nilikuwa darasani, mwaka ule wa huzuni,
Nikapigwa kichogoni, kiza nikawa sioni,
Kisunzu tele mwilini, puu nikabwagwa chini.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
13.
Kabla sijabwagwa chini, nilimuuliza jirani,
Aliyenipiga nani, cha mno hasa ni nini?
Nimewakera nini, hata nipigwe kichwani.
Wakanicheka jamani, nikaihisi tafrani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
14.
Dotto uko na nini? Akanishika begani,
Aliyekupiga nani? amekupiga na nini?
Una mawazo gani? Una wazimu kichwani?
Akaiomba amani, nisiizue tafrani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
16.
Nilipoanguka chini, Nikawa niko ndotoni,
Niko mwenyewe njiani, nchi ya ughaibuni,
Nakimbizwa na manyani, wenye mawe mikononi,
Nikasemea moyoni, Lile si Joka jamani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
17.
Joka hili joka gani? Mwenye kipembe kichwani,
Ana shanga shingoni, pete tano mkiani,
Mwale wa moto machoni, moshi watoka puani,
Akazichochea kuni, kwa kuungana na nyani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
18.
Nilisoma vitabuni, habari ya maluuni,
Mwenye kipembe kichwani, ndiye huyo maluuni?
Aliyezua tafrani, duniani na mbinguni,
Ana matobo kichwani, hana jema asilani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
19.
Mwenye pembe kichwani, alifukuzwa mbinguni,
Akashuka duniani, kama Amiri jeshini,
Watu hawaelewani, kisa huyu punguani,
Nilo soma vitabuni, leo dhahiri machoni,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
20.
Mwenye kipembe kichwani, likaungana na nyani,
Loo! niko hatarini, kutolewa duniani.
Na hawa mahayawani, watia ndimi puani,
Nikamuomba Manani, anitoe hatarini.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
21.
Jasho likanimwaika, na miguu ikachoka,
Manyani wakanifika, Joka likanizunguka,
Hakika nilitishika, mwili ukatetemeka,
Mama nikamkumbuka, na yowe likanitoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
22.
Mkojo ukanitoka, bila mwenyewe kutaka,
Mwili wote ukachoka, nikahisi kuanguka,
Li Joka likajisuka, mwili akauzunguka,
Mwili ukasisimka, na woga ukanishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
23.
Sauti zikasikika, ya mifupa kuvunjika,
Nyani wakaongezeka, sijui walipotoka,
Wakawa wakinicheka, vile ninavyoteseka,
Tena wakirukaruka, duara wakizunguka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
24.
Miguu ilinyooka, ulimi ukanitoka,
Shingo ilivutika, koo likakabika,
Mwili ukatetemeka, baridi ikanishika,
Ningeweza kuanguka, ni joka lilonishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
25.
Roho iliangaika, nikahisi yanitoka,
Pumzi ziliathirika, kuruzo lilinitoka,
Mishipa ilipasuka, damu zikachuruzika,
Koo lilinikauka, na kiu ilinishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
26.
Mambo yaso kufika, masikio huyachoka,
Vigumu kuaminika, hadi yata’po kufika,
Kweli nimeona Joka, Baada ya kuzimika,
Hata nilipozinduka, kichwani hakunitoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
27.
Ndotoni nikiteseka, Kwa waja nilizimika,
Nyuso zilifadhaika, huku wakiangaika,
Wapo walonishika, wakisema pepo toka,
Visomo vilifanyika, ili nipate zinduka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
28.
Waliomba kwa Rabuka, ili nipate ponyeka,
Maneno yakanitoka, sauti ikachujika,
Mimi si mwenye kutoka, hapa ndio nimefika,
Fanyeni mnalotaka, katu si mwenye kutoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
29.
Watu waliongezeka, sauti iliwafika,
Dotto nataabika, joka limenizunguka,
Kumbe hovyo naboboka, na sauti zabadilika,
Macho yalinitoka, na shingo ilipindika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
30.
Mrembo aloumbika, sijui alipotoka,
Manyani wakatishika, ajabu wakatoweka,
Joka likafokafoka, na ndimi ilimtoka,
Kipembe kikatamka, mambo yasoelezeka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
31.
Hatua akairuka, haraka akanifika,
Vitisho vyote vya joka, Mrembo hakutishika,
Machoni alinishika, nikayafumba haraka,
Macho yalipofumbuka, nikawa nimezinduka.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
32.
Loo amezinduka, mmoja akasikika,
Damu zinamtoka, ulimi umechanika,
Taratibu kapashika, damu zinaponitoka,
Kumbe hapajachimbika, ni kama amechubuka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
33.
Kivivu nikainuka, tayari kwa kuondoka,
Nguo zilivyochafuka, rangi zilibadilika,
Nyumbani nilifika, si kama niloanguka,
Wale walonipeleka, wala hawakusumbuka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
34.
Wala sikupumzika, nyumbani nilipofika,
Ndugu walonizunguka, niliwatoa mashaka,
Jinsi nilivyoanguka, kuwaficha sikutaka,
Yale yaliyo nifika, wala sikuyafutika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
35.
Wala sikuyafutika, yote yaliyo nifika,
Kisunzu na kuanguka, kiza na kuzimika,
Habari za yule joka, na bint aloumbika,
Wale nyani walozuka, mwisho nilivyozinduka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
36.
Wote walifadhaika, huzuni iliwashika,
Hasa walipokumbuka, Bibi alivyoondoka,
Alianza kudondoka, na kisha akazimika,
Naye aliweweseka, na macho yalimtoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
37.
Kitu alichotamka, Bibi alipozinduka,
Nilizingirwa na Joka, na nyani walonicheka,
Mwanamke alipozuka, machoni akanishika,
Roho nahisi yatoka, akaaga na kuwatoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
38.
Bibi aliyependeka, ndivyo alivyowatoka,
Kifo chake cha mashaka, sasa wakakikumbuka,
Wenzangu hawakutaka, yaleyale kunifika.
Hatimaye wakatoka, nami nikapumzika.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
39.
Jinsi walivyotishika, wala hapakukalika,
Nyumbani wakaondoka, wote wamehamanika
Hofu iliyowashika, mganga wakamsaka,
Wallahi hawakutaka, yale yale kunifika.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.
40.
Majani ya mkirika, mizizi ya msanaka,
Buni zilizokauka, na mafuta ya mbarika,
Ndivyo vilivyotumika, mwili wangu kuzindika,
Lengo nipate epuka, matatizo kunifika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Dotto Chamchua Rangimoto.(Njano5.)
255762845394/255762845394
mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania.

KISA CHA MISHI, MAPENZI SI HESABU

KISA CHA MISHI, MAPENZI SI 
HESABU.     
                  
1.
Kwa jina naitwa Mishi, binti mwenye heshima,   
Mwenzenu ni mtumishi, nipo ofisi ya umma,
Kama hiyo haitoshi, mwanamke najituma,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
2.
Nina gari namiliki, mwenyewe sina dereva,
Ninayo nyumba Masaki, nina shamba Usariva,
Kwa fedha sibabaiki, nakula vilivyo iva,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
3.
Nina elimu si haba, UDSM nimesoma,
Shukurani zake baba, pongezi kwa wangu mama,
Kazi sasa yanibeba, umri nao wayoyoma,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
4.
Nimetafuta jamali, mwenzenu nataka mume,
Hata awe suruali, aso kitu kwa kuume,
Kikubwa awe rijali, simtaki gumegume,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
5.
Kila nilipo pakaa, matatizo hunipata
Tarasimu hazikufaa, kunikinga na matata,
Nikaja kata tamaa, huyo mtu sikumpata,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
6.
Penzi kiumbe habithi, mja naomba sikia,
Ninatendwa uhanithi, moyoni ninaumia,
Usije dhani hadithi, tena si tamthilia,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
7.
Sijui nianze mwisho, pale tulipogombana,
Na vile vyake vitisho, yaani vya kuachana,
Si lolote ni michosho, si ya leo si ya jana,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
8.
Vema nianzie mwanzo, pale tulipokutana,
Niwasimulie chanzo, mimi naye kushikana,
Mimi nilikuwa ponzo, alipogongwa kijana,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
9.
Ndipo ikanilazimu, mwili wake kuutibu,
Na ule umaamumu, ukamtoka taratibu,
Nikawa ninajihimu, kutazama matibabu,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
10.
Mgonjwa kawa mpenzi, bila hata kumaizi,
Akaanza kunienzi, taratibu kwa mapozi,
Nami nikawa mpanzi, sikuifanya ajizi,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
11.
Sijui nikawa wapi, sikuona mbalamwezi,
Nuru ilitoka vipi, na jua halichomozi,
Sijui dunia ipi, mapenzi kumbe uchizi,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
12.
Huyu Jamali muhibu, alikuwa yu chuoni,
Anasoma uhasibu, palepale Mlimani,
Bumu likileta tabu, humpiga kampani,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
13.
Sijiu ndio kudeka, au kuchuna jamani,
Mishi kile nakitaka, sina fedha mfukoni,
Ili nipate ridhika, nipatie wangu hani,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
14.
Nikakope kama sina, muhibu wangu apate,
Mwanafunzi kazi hana, niliwaza siku zote,
Kumbe mapenzi hakuna, kiumbe chuma ulete,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
15.
Pendo lake silipati, ubavuni hanitoki,
Pendo lake ni la chati, na kumuacha sitaki,
Nampenda kwa dhati, ila kwake sipendeki,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea..
16.
Kosa hakika si kosa, mbona atasema sana,
Ya zamani na ya sasa, wallahi yatajazana,
Mapenzi yananitesa, utulivu hata sina,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
17.
Huo wivu alonao, kama anipenda sana,
Situmii mitandao, uhuru mwenzenu sina,
Anipangia vikao, niende au hapana,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
18.
Kila siku twazozana, kama mafurusi sina,
Na leo tumegombana, sababu ni ndogo sana,
Akatalii uchina, nauli yenyewe hana,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
19.
Sina karma ya Mwasiti, mahaba ningeyavua,
Kama yangekua kiti, kalio ningeinua,
Nimezama katikati, mapenzi yaniumbua,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
20.
Kumuacha natamani, moyo wangu hautaki,
Hanipendi si utani, ila kwangu haondoki,
Anaruka kama Nyani, ubavuni habanduki,
Penzi halina kanuni, chunga usije kosea.
21.
Sijui niendelee, au hapa niishie,
Sasa twaenda uzee, yako mengi niwambie,
Naomba mtuombee, ndoa yetu itulie,
Shida ukizizoea, njia utajipatia.

Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5)
Mzalendo.njano5@gmail.com
784845394/764845394
Morogoro Tanzania